The House of Favourite Newspapers

Serikali yafuta usajili wa magazeti 473

0

Nape-702x336Leo Serikali kupitia Wizara ya Habari iliyochini ya Nape Nnauye imesema kuwa imefuta usajili wa magazeti 473 kupitia tangazo lililochapishwa katika gazeti la serikali lenye namba 195, baada ya kutochapishwa kwa miaka mitatu mfululizo.

Magazeti hayo hayataruhusiwa kuchapishwa au kusambazwa kwa njia ya nakala ngumu au kielektroniki, ikiwa Mmiliki wa gazeti lililofutiwa usajili angependa kuendelea na biashara milango iko wazi kwa ajili ya kuwasilisha maombi mapya ya usajili kwa kufuata taratibu zilizopo.

Kwa mujibu wa takwimu za ofisi ya msajili wa magazeti Tanzania inayo magazeti na majarida 881 yaliyosajiliwa kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Nape Nnauye amesema kuwa wamiliki wa magazeti hayo wamevunja sheria na kwa mujibu wa kifungu 23(1) cha Sheria ya Magazeti ambacho kinampa mamlaka ya kuyafutia usajili, anayafungia magazeti hayo.

“Kuna magazeti yana miaka mitatu sasa bado hayajatolewa nakala mengine yalikuwa yanatoa na baadae yakaacha na mengine hayajatoa kabisa, haya yote natangaza kuanzia leo yamefutwa usajili wake,” alisema Waziri Nape.

Waziri Nape alisema kuanzia sasa hairuhusiwi kwa mtu yoyote kuchapisha nakala za magazeti yaliyofungiwa na kwa kufanya hivyo atakuwa amekiuka Sheria ya Magazeti sura ya 229, kifungu cha 6 na hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha Waziri Nape aliongeza kuwa kama kuna mmiliki wa magazeti ambayo yamefungiwa angependa kuendelea kuchapisha nakala za gazeti lake, milango ipo wazi kuwasilisha maombi mapya ya usajili kwa kufuata sheria zilizopo.

Magazeti-yaliyofungiwa

Leave A Reply