The House of Favourite Newspapers

Shigongo: Ukitaka Kuwa Salama, Shughulikia Kinga Yako ya Mwili

0

NI Jumamosi tulivu nikiwa naendelea na majukumu yangu ya kila siku. Moyo wangu umejawa na huzuni kutokana na vifo vya viongozi wetu wa nchi waliopoteza maisha ndani ya wiki hii.

Taifa bado lipo kwenye huzuni, vifo vya Maalim Seif Sharif Hamad, Balozi John Kijazi na Dk Servacius Likwelile vimeacha maumivu makali kwenye mioyo ya wengi.

 

 

Ndugu zangu, siku zote kifo huwa hakizoeleki, hata ungekuwa jasiri kiasi gani, unaposikia mtu wako wa karibu au mtu muhimu kwenye maisha yako amefariki dunia, lazima utaumia mno ndani ya moyo wako.

 

 

Wimbi la maradhi mbalimbali yanayosababisha vifo vya wapendwa wetu, lisisababishe hofu kwenye mioyo yetu. Tuendelee kumuomba Mungu wetu atuvushe salama katika kipindi hiki kigumu kwa sababu hakuna jambo linaloshindikana kwake.

 

 

Kwa namna ya kipekee kabisa, natoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu waliotangulia mbele za haki na tunawaombea huko waendako kwani safari yetu ni moja.

 

 

Nimewahi kuandika kwenye ukurasa huu na leo narudia tena, tunapopita katika wakati mgumu kama huu, njia nyingine mbali na kumuomba Mungu wetu, tunapaswa kuhakikisha kinga za miili yetu zinaongezeka ili tuwe na uwezo wa kupambana na maradhi mbalimbali yanayotunyemelea.

 

 

Nataka nikukumbushe kuhusu mambo ambayo unapaswa kuyaepuka katika kipindi hiki kwa sababu yanazorotesha kinga ya mwili. Ni muhimu sana ukazingatia hiki ninachokieleza hapa.

 

 

Kinga inayozungumziwa ni ule uwezo wa mwili kupambana na maambukizi ya vijidudu vinavyoweza kusababisha madhara katika mwili! Seli za mwili zinapambana na vijidudu vya maradhi na hatimaye kuvishinda.

 

 

Pengine kila mtu anatamani kuwa na kinga imara ya mwili, lakini ni wachache wanaojua ni mambo gani yanayoweza kuharibu kabisa kinga ya mwili wako na kukufanya uwe mwepesi kupata maambukizi.

Mambo yanayodhoofisha kinga ya mwili ni kama yafuatayo;

 

KUKOSA USINGIZI

Kukosa usingizi wa kutosha ni miongoni mwa mambo yanayochangia sana kushusha kinga ya mwili na hata unapopata maambukizi, inaweza kukuchukua muda mrefu zaidi kupona.

 

 

Hii ni kwa sababu, unapokuwa usingizini, mwili huzalisha hormone iitwayo cytokines ambaye kazi yake ni kuamsha mfumo wa kinga ya mwili. Kwa hiyo unapokosa muda wa kutosha wa kulala, maana yake ni kwamba homoni hiozi zitazalishwa kidogo au hazitazalishwa kabisa na kinga ya mwili itapungua.

 

 

MSONGO WA MAWAZO NA WASIWASI

Hofu, wasiwasi na msongo wa mawazo ni miongoni mwa vitu vinavotajwa kusababisha kupungua sana kwa kinga ya mwili. Unashauriwa kitaalamu kwamba unapotokewa na hali ya kuogopa kitu chochote ndani ya moyo wako au kuwa na wasiwasi, lazima ujitahidi kupambana na hali hiyo ili isikae ndani yako kwa zaidi ya dakika thelathini!

 

 

Utafiti wa kitaalamu unaonesha kwamba msongo wa mawazo, hasa ule usioisha, huchangia kuzorotesha kabisa kinga ya mwili kiasi cha kuufanya kukosa uwezo wa kujikinga dhidi ya maambukizi.

 

 

UKOSEFU WA VITAMIN

Inafahamika kwamba vitamin mbalimbali zina umuhimu mkubwa mwilini wa kupandisha kinga ya mwili, zikiwemo Vitamin C na Vitamin D.

 

 

Vyakula vyenye Vitamin C ni pamoja na machungwa, mapapai na matunda mengine ya jamii hiyo. Vitamin D inapatikana kwa wingi kwenye mayai, samaki, maziwa, ngano na kadhalika, lakini pia kuota jua la asubuhi au jioni ni chanzo kizuri cha Vitamin D.

 

 

BAADHI YA DAWA ZA HOSPITALI

Baadhi ya dawa zinazotumika kutibu magonjwa mbalimbali kama mzio, arthritis, lupus na zile zinazotumika kwa watu waliopandikizwa viungo mbalimbali kwenye miili yao, zinatajwa kusababisha kushuka kwa kinga ya mwili.

 

 

Dawa nyingine zilizopo kwenye kundi la corticosteroids na zile zinazotumika kutibu tatizo la saratani, pia zinasababisha kushuka kwa kinga ya mwili.

 

 

KUTOKULA MBOGA ZA MAJANI NA MATUNDA

Ulaji wa mboga za majani na matunda, unatajwa kuwa chanzo cha uzalishaji mzuri wa seli nyeupe za damu ambazo ndizo zinazofanya kazi ya kuulinda mwili dhidi ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali.

 

 

Kwa kifupi, ulaji wa mbogamboga na matunda, husaidia kuimarisha kinga ya mwili, kwa hiyo inapotokea huli mbogamboga na matunda ya kutosha, matokeo yake ni kwamba kinga yako itashuka na kujiweka kwenye hatari ya kuambukizwa maradhi mbalimbali, ikiwemo virusi vya Corona!

 

 

ULAJI WA VYAKULA VYENYE MAFUTA

Inaelezwa kwamba ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi husababisha seli nyeupe za damu ambazo ndizo zinazohusika na kinga ya mwili kushindwa kufanya kazi yake vizuri.

 

 

Pia uwepo wa mafuta mengi tumboni huathiri utendaji kazi wa bakteria waliopo tumboni ambao kazi yao ni kupambana na maambukizi mbalimbali. Lakini pia ulaji wa vyakula vyenye mafuta, hukufanya kuwa na mwili mkubwa (obesity) ambao nao hukuongezea hatari ya kupata magonjwa mbalimbali.

 

 

KUKOSA HEWA SAFI YA KUTOSHA

Inaelezwa kwamba watu wenye tabia ya kujifungia au kukaa ndani kwa muda mrefu, hasa kwenye vyumba vyenye hewa nzito, wana hatari kubwa ya kushusha kinga za miili yao, kuliko wale wenye kawaida ya kutoka nje na kukaa mahali penye hewa safi.

 

 

Hii ni kwa sababu unapotoka nje na kukaa maeneo yenye hewa safi, unajiweka kwenye nafasi ya kuvuta kemikali iitwayo phytoncides ambayo hutolewa na mimea, ambayo inapoingia ndani ya mwili husaidia kuboresha kinga ya mwili.

 

 

UVUTAJI WA SIGARA

Uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako kwa sababu kemikali iliyopo kwenye sigara zote na bidhaa nyingine za tumbaku (nicotine), inapoingia mwilini huenda kushusha kinga ya mwili na kufanya iwe rahisi kwako kushambuliwa na magonjwa mbalimbali.

 

 

UNYWAJI WA POMBE KUPITA KIASI

Inaelezwa kitaalamu kwamba unapokunywa pombe kupita kiasi, unapunguza kasi ya mwili kupambana na maambukizi mbalimbali kwa muda wa saa ishirini na nne! Sasa ikitokea unakunywa kila siku, maana yake ni kwamba kinga yako itakuwa chini siku zote na kukuweka kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa mbalimbali.

 

 

Lakini pia unywaji wa pombe kupita kiasi, hufubaza uwezo wa seli za mwili kujitibu zenyewe na hiyo ndiyo sababu inayosababosha walevi wengi kuja kusumbuliwa na magonjwa ya ini, pneumonia, kifua kikuu na aina fulani ya saratani.

 

 

KUTOFANYA MAZOEZI

Inaelezwa kwamba watu wanaofanya mazoezi mara kwa mara, huwa na kinga imara kuliko wale wasiofanya mazoezi. Unapofanya mazoezi, unayafanya mapafu yako yaingize hewa safi ya kutosha na kutoa hewa chafu, lakini pia unaufanya moyo usukume damu kwenda kwenye sehemu zote za mwili na hivyo kufikisha vichocheo vinavyohusika na kinga ya mwili kila sehemu ya mwili wako.

Ahsanteni kwa kunisoma na Mungu awabariki sana.

Leave A Reply