The House of Favourite Newspapers

Shinda Nyumba Awamu ya Pili… Leo Ndiyo Leo CCM Mwinjuma

DROO ya pili ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili inafanyika leo Ijumaa katika Viwanja vya CCM Mwinjuma, Mwananyamala Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Hii itakuwa ni droo ya pili baada ya ile ya kwanza iliyofanyika Februari 8, mwaka huu katika Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem ambako washindi watano walipatikana ambao walijishindia zawadi za pikipiki, televisheni kubwa, simu za kisasa, vyombo vya jikoni na vitu vingine vingi vidogovidogo.

Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho alisema jana kuwa mipango yote kwa ajili ya shughuli hiyo ya pili imekamilika na kilichobakia ni kusubiri saa nane mchana ifike ili shughuli ianze.

“Kama ilivyokuwa katika droo ya kwanza, washindi wa leo pia wataibuka na zawadi zilezile. Mshindi wetu wa kwanza ataondoka na pikipiki, pia atakuwepo mtu atakayejinyakulia televisheni kubwa, atapatikana pia msomaji mmoja atakayeondoka na simu ya kisasa ya mkononi na pia wa vyombo vya ndani,” alisema Mrisho.

Aliwataka wasomaji wote wa magazeti ya Global Publishers, ambayo ni Risasi, Amani, Uwazi, Ijumaa, Championi na Ijumaa Wikienda, kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo litakalofanyika katika viwanja hivyo vya CCM Mwinjuma, Mwananyamala A jijini Dar es Salaam.

“Tulisema pale mwanzo na leo ninarudia tena kuwa tutachezesha bahati nasibu hizi ndogo kila mwezi kabla ya kufanya ile kubwa ambayo mshindi wake atajinyakulia nyumba yenye thamani ya mamilioni ya shilingi.

“Tunafanya hivi ili kuonyesha ni kwa kiasi gani tunaguswa na mchango wa wasomaji wa magazeti yetu, kwani wao ndiyo wametufanya leo tuwe hapa tulipo, kwa hiyo kwa kuwa hatuwezi kumpa kila mmoja, tunafanya tukio kama hili ili wachache miongoni mwao, wawe wawakilishi wa shukurani zetu,” alisema.

Washindi hao wa droo ndogo ya kwanza walikuwa ni Andrew Mtunguja wa Muheza mkoani Tanga, Ambrosi Ligonja wa Mang’ula Morogoro, Evans Stanley wa Kunduchi, Said Mohamed na Gasto Peter wote wa Kimara jijini Dar es Salaam.

Bahati nasibu hiyo kubwa kabisa kuwahi kuchezwa na kampuni ya magazeti nchini, inadhaminiwa na Kilimanjaro Institute of Technology and Management iliyopo Mwenge kwa Mama Ngoma na Afrika Sana na British School ambayo ipo karibu na Kituo cha Daladala cha ITV, karibu na Kanisa la Lutheran.

Comments are closed.