The House of Favourite Newspapers

Shinda Nyumba Yawavutia Wananchi wa Vijijini

0
Wasomaji wa magazeti ya Global katika Viwanja vya CCM Mwinjuma wakijaza kuponi dakika za lala salama kabla ya kucheshwa Bahati Nasibu hiyo.

BAHATI Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili inayoendeshwa na Kampuni ya Global Publishers, wachapishaji wa magazeti ya Ijumaa, Championi, Risasi, Amani, Uwazi na Ijumaa Wikienda ambayo awali ilichangamkiwa na wakazi wa mijini pekee, sasa imefika hadi vijijini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na chumba cha habari cha Global Publishers, wasomaji Marc Kambona, aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa Kijiji cha Longa mkoani Ruvuma, alisema ametambua uwepo wa bahati nasibu hiyo hivi karibuni baada ya kufika mjini Songea na kupata nakala ya Gazeti la Championi.

“Niliposoma ndipo nikagundua kuwa kumbe kuna hii bahati nasibu na kwamba ni ya pili, mimi binafsi nilikuwa sijui kama kuna kitu kama hiki na hata wanakijiji wenzangu hawakuwa wakijua, sasa nilipokwenda na gazeti na kuwaonyesha, nao wamehamasika na sasa kila mtu akiwa anakuja mjini anaagizwa asikose kuwabebea magazeti ya Global,” alisema.

Kambona alisema licha ya kila mmoja kuwa na nia ya kushinda nyumba, lakini hata hizo zawadi ndogondogo zinazotolewa, kwao zinawatosha kubadili maisha yao.

“Nyie huko zawadi kama pikipiki wanaziona ni ndogo, lakini kwa sisi huku mtu ukipata pikipiki ndiyo umetoka hivyo kimaisha, kwa hiyo watu hivi sasa wanagombea magazeti yenu ilimradi kila mtu ajaribu bahati yake,” alisema Kambona.

Lameck Suluja kutoka Kijiji cha Mudida wilayani Iramba mkoani Singida, naye alisema ameshtuka kusikia kuna bahati nasibu kubwa ya shinda nyumba, baada ya kwenda mjini na kununua gazeti la Ijumaa.

“Nilinunua gazeti baada ya kuvutiwa na habari iliyoandikwa pale mbele, sasa nasoma ndani nakuta eti kuna bahati nasibu ya nyumba, haki ya Mungu sikuwa najua, nimewaeleza vijana wenzangu pale kijijini wamedata, kila mtu sasa anataka kushiriki ili kujaribu bahati yake,” alisema.

Kama ilivyokuwa kwa Kambona, Suluja naye alisema wanakijiji wenzake wamehamasika, wakitaka nao kushiriki ili waweze kujishindia mojawapo ya zawadi zinazoshindaniwa. Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili imedhaminiwa na Kampuni ya Tecno Mobile, King’amuzi cha Ting, British School na Kilimanjaro Institute of Technology.

Leave A Reply