The House of Favourite Newspapers

Baada 167 Kufa Maji DRC, Wengine 30 Wafariki

USAFIRI wa majini umeendelea kuwa jinamizi kwa wasafiri nchini nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) baada ya ajali ya boti kugharimu maisha ya watu 30 huku wengine zaidi ya 300 hawajulikani walipo katika eneo la Inongo magharibi mwa nchi hiyo.

 

Ajali hiyo ambayo ni mwendelezo wa majanga ya majini nchini DRC imetokea usiku wa Jumamosi kwenye Siwa Mai-Ndombe, na bado mamia ya wale waliosafiri katika boti hiyo hawajapatikana mpaka sasa.

“Mpaka sasa tumeshapata maiti 30, wanawake 12, watoto 11 na wanaume saba,” Meya wa Inongo, Simon Wemba, ameliambia shirika la habari la kimataifa la AFP

 

“Idadi hiyo ya vifo ni ya muda huu, na yaweza kubadilika muda wowote,” Wemba amesisitiza, akiongeza kuwa ni vigumu kujua kwa hakika boti hiyo ilikuwa imebeba abiria wangapi na yawezekana ilikuwa imebeba wahamiaji haramu.

Wemba amesema kuwa kwenye ajali hiyo waliokolewa watu 183, chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni hali mbaya ya hewa.

Boti hiyo pia inaaminika kuwa ilipakia idadi kubwa ya walimu ambao walikuwa wanaelekea kupokea mishahara yao.

Janga la majini DRC

Ajali hiyo imetokea ikiwa ni mwezi mmoja tu toka watu 167 walipofariki kwenye ajali mbili za majini kwenye nchi hiyo. Ajali hizo zilimlazimu rais wa DRC, Felix Tshisekedi, kuamrisha kuwa abiria wote wa vyombo vya majini nchini humo wavalishwe maboya muda wote wa safari.

 

DRC ambayo ndiyo nchi kubwa zaidi barani Afrika, inategemea mito na maziwa kama njia za usafiri wa watu na mizigo na kuunganisha maeneo kadhaa ya nchi hiyo ambayo ni vigumu kufikika kupitia barabara.

Hata hivyo, usafiri huo umekuwa wa hatari kwa usalama, na licha ya serikali kuchukua hatua mbadala kutafuta ufumbuzi katika suala hilo bado hali si swari.

 

Ajali nyingi husababishwa na matatizo ya kiufundi ya vyombo vya majini pamoja kujaza watu na kupita kipimo.

Idadi ya vifo huwa kubwa sababu abiria hawavai maboya ya kujiokoa, lakini pia raia wengi wa nchi hiyo hawajui kuogelea.

Watu 27 walipoteza maisha baada ya boti  kuzama Septemba mwaka jana,  ambapo Julai walikuwa 26, Mei watu 50, Aprili watu 40,  wote wakiwa njiani kukimbia mapigano mashariki mwa nchi hiyo.

 

Majanga hayo ya majini pia yanatokana na serikali ya nchi hiyo iliyopo mji mkuu wa Kinshasa kushindwa kusimamia vizuri utekelezwaji wa sheria kutikana na maeneo mengi yenye mito na maziwa kuwa mbali na nchi hiyo kukumbwa wa mapigano.

 

Majanga Afrika Mashariki

Jumanne wiki iliyopita ilitimia miaka 23 tangu ajali ambayo inatajwa kuwa mbaya zaidi katika karne hii kutokea barani Afrika katika Ziwa Victoria nchini Tanzania.

Ni janga ambalo lilisababisha idadi kubwa ya vifo vya watu wapatao 1,000 baada ya meli ya Mv Bukoba kuzama.

Kwa miaka yote hiyo Tanzania imeendelea kukumbwa na majanga makubwa na madogo ya majini.

Mwaka jana, Septemba 2018 jumla ya watu 224 walifariki na watu wengine 41 wakiokolewa wakiwa hai katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere.

Mwaka 2011 na 2012 watu zaidi ya 250 walipoteza maisha kwenye Bahari ya Hindi baada ya kuzama kwa meli za MV Spice Islander na Mv Skagit.

 

Jumatatu iliyopita, Mei 20, 2019,  ajali ya majini ilitokea na kuua watu 16 huku wengine wakiwa hawajulikani walipo nchini Uganda.

Boti ilikuwa imebeba wacheza mpira 50 wakiwa na mashabiki wao magharibi mwa Uganda.

Mwaka 2016 , wachezaji 30 wakiwa na mashabiki wao walizama katika Ziwa Albert na watu 20 walifariki.

Mwaka 2018 watu 29 walifariki kufuatia ajali ya boti iliyotokea Ziwa Victoria, nchini Uganda.

 

Boti hiyo iliyokuwa na watu zaidi ya 90 waliokuwa wanaelekea kwenye sherehe, ilipata ajali katika kaunti (wilaya) ya Mpatta wilaya ya Mukono.

Mwaka 2014, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa takriban watu 98, wamekufa maji baada ya boti walimokuwa wanasafiria kuzama katika Ziwa Albert Magharibi mwa Uganda.

Boti iliyozama ilikuwa imebeba zaidi ya wakimbizi 100.

Aliyekuwa anaendesha boti hiyo alikamatwa na jeshi la polisi na inadaiwa kuwa alikuwa amelewa.

Comments are closed.