The House of Favourite Newspapers

Simba Kama Wafalme Morocco

0

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, Simba SC tayari wapo Morocco kwa kambi ya takribani wiki mbili ambapo wanajiandaa na msimu wa 2021/22.Simba waliondoka Tanzania juzi Jumanne kupitia Dubai kabla ya jana Jumatano kufika Morocco tayari kwa kambi hiyo.

 

Wakiwa huko Morocco, inaelezwa kwamba Simba wataishi kama wafalme kutokana na eneo lenyewe kuwa la kitalii na mambo yote yanayohusu mazoezi ikiwemo viwanja.

 

Kambi hiyo ambayo Simba wamefikia, mara kwa mara imekuwa ikitumiwa na Timu ya Taifa ya Morocco.

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Morocco, Simba walitarajiwa kufikia eneo la Nador lililopo pwani ya kaskazini mashariki mwa Mkoa wa Rif ambapo kutoka hapo hadi kufika Jiji la Melilla, Hispania ni umbali kwa kilomita 10.

 

Siku chache kabla ya Simba kufika huko, alitangulia Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez ambaye alikwenda kuweka mazingira sawa.

Kambi hiyo ya Simba ni mapendekezo ya benchi lao la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Didier Gomes ambaye ametaka sehemu yenye utulivu ambayo itawafanya wafanye maandalizi yao vizuri ili kutimiza malengo yao msimu wa 2021/22 ambapo watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na michuano ya ndani.

Simba imeenda Morocco ikiwa na baadhi ya wachezaji wapya na wa zamani, huku wengine wakiachwa Dar kukamilisha masuala mbalimbali ya vipimo kabla ya kuungana na wenzao.Wakati Simba wakiwa huko, Yanga nao wanatarajiwa kwenda Morocco kuweka kambi nao wakijiandaa na msimu mpya wa 2021/22.

NA MWANDISHI WETU, Dar es Salaam

Leave A Reply