The House of Favourite Newspapers

Simba: Sasa Tunataka Kombe la FA

0

BAADA ya kufanikiwa kutetea kwa mara ya nne kombe la Ligi Kuu Bara, sasa uongozi wa klabu ya Simba umeweka wazi kuwa malengo yao kwa sasa ni kuhakikisha wanatetea tena Kombe la Shirikisho ‘FA’ Julai 25, mwaka huu mbele ya Yanga.

 

Simba Jumapili iliyopita iliutangaza rasmi kwa mara ya nne mfululizo ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union, na kufanya wafikishe pointi 79 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye ligi ya msimu huu.

 

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana katika fainali ya Kombe la Shirikisho, itakayochezwa katika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma Julai 25, mwaka huu.

 

Huu utakuwa mchezo wa pili ndani ya mwezi mmoja kwa Simba na Yanga kukutana msimu huu, huku Yanga wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa kiporo cha Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar Julai 3, mwaka huu.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema: “Malengo yetu ni kutwaa makombe kwenye kila michuano tutakayoshiriki, tumefanikiwa kwenye ligi, na sasa shabaha yetu ni kutetea ubingwa wetu wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga.

 

Tunajua walitufunga katika mchezo wetu uliopita wa ligi, lakini nikuhakikishie kuwa tutajipanga vizuri kushinda Kombe la Shirikisho Julai 25, mwaka huu.”

Stori: Joel Thomas

Leave A Reply