The House of Favourite Newspapers

STAMICO Waanika Siri ya Ushindi Maonesho Sabasaba

0
Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Dk. Venance Mwasse akiwa ameshika tuzo ya ushindi wa jumla katika maonesho ya sabasaba yaliyofikia tamati wiki hii.

 

 

UBUNIFU wa kipekee na uanzishwaji wa viwanda vya kisasa katika sekta ya madini, ni mojawapo ya siri ya ushindi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo limejinyakulia tuzo ya ushindi wa jumla katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam maarufu kama sabasaba.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa STAMICO, Lukas Selelii akiwa ameshika tuzo ya ushindi pamoja na wafanyakazi wengine baada ya shirika hilo la madini kuibuka mshindi katika maonesho ya sabasaba.

 

 

Katika maonesho hayo ya 45 ambayo yalifungwa Julai 13 mwaka huu na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, STAMICO iling’ara kwa ushindi huo kutokana na ubora wa huduma zake kuenenda sawasawa na kauli mbiu ya maonesho hayo ambayo ilikuwa ni ‘Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu’.

 

 

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Dk. Venance Mwasse, Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala, Deusdedith Magala alisema kukamilika kwa ujenzi na uzinduzi wa kiwanda cha kisasa cha kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery Ltd kilichopo jijini Mwanza ni mojawapo ya siri ya ushindi wa STAMICO.

Kiwanda hicho cha kusafisha Dhahabu cha Mwanza kina uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa kiwango cha Kimataifa kwa ubora wa asilimia 999.9 purity.

Aidha, Mkurugenzi huyo alisema kiwanda hicho kilichozinduliwa rasmi Juni 13 mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan, ni fursa ya kipekee kwa makampuni ya uchimbaji wa dhahabu na wachimbaji wengine kutoka ndani na nje ya nchi kusafisha dhahabu yao katika kiwanda hicho.

Pia alisema ubunifu wa kipekee wa bidhaa ya Rafiki briquettes ambayo ni mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe, pia imekuwa kivutio cha kipekee kwa wananchi waliotembelea banda la STAMICO katika maonesho hayo ya sabasaba.

Akifafanua kuhusu Rafiki briquettes, Magala alisema mkaa huo unafaida lukuki ikiwamo kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na miti hasa ikizingatiwa matumizi yake yamekuwa yakiharibu mazingira.

Alisema mkaa huo ambao ni rafiki kwa mazingira, hauharibu chombo cha kupikia yaani sufuria lakini pia unatumika kwa muda mrefu kabla ya kubadilisha mwingine.

Aidha, alisema licha ya kuwepo kwa sampuli za mkaa huo, kuanzia mwezi wa Septemba na Oktoba mwaka huu ndipo uzalishaji wa majaribio utakapoanza baada ya kupokea mitambo itakayokuwa na uwezo wa kuzalisha tani mbili kwa saa.

Alisema kwa awamu ya kwanza, STAMICO kwa kushirikiana na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), itasimika mitambo hiyo jijini Dar es Salaam kisha baada ya muda italetwa mitambo mingine itakayokuwa na uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa na kusimikiwa huko Itungi mkoani Mbeya.

Pamoja na hayo, Magala pia alitoa wito kwa kampuni mbalimbali za uchimbaji wa madini, kutumia mitambo uchorongaji ya shirika hilo kwa kuwa ni mojawapo ya mitambo yenye teknolojia ya kisasa zaidi kuwahi kutumika hapa nchini ikiwamo  mtambo wenye uwezo wa kuendeshwa kwa kutumia kompyuta.

Leave A Reply