The House of Favourite Newspapers

Simba Usajili Huu Mahitaji ya Kocha?

0
Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog.

KWENYE mitandao ya kijamii mtu mmoja jana alikuwa anapitisha ujumbe kwa njia ya utani akipanga kikosi kizima cha Simba tena kikionekana kuzidi kabisa na wote aliopanga ni wapya.

Utani ule ulikuwa unafanana na ukweli maana wachezaji wapya wanaotajwa ndani ya Simba mpaka jana walikuwa 12, ni sawa na kikosi kipya na wa akiba mmoja. La kujiuliza hapa haya ni mahitaji ya Kocha Joseph Omog au ni kusajili kwa utashi tu, tena wa watu?

Hebu ona utani wa mtu huyu katika mtandao jana alikipanga hivi kikosi cha Simba kuanzia makipa Aishi Manula na Said Mohamed ‘Nduda’, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Salim Mbonde, Yusuf Mlipili, Emmanuel Mseja, Haruna Niyonzima, Jamal Mwambeleko, Ally Shomari, John Bocco na Emmauel Okwi.

Emmauel Okwi.

Ukikiangalia kikosi hicho maana hao ni wote wanaotajwa kusajiliwa na Simba utakiona ni kikosi kipya kabisa. Hakuna wa zamani hata mmoja katika kikosi cha kwanza. Unajiuliza Simba inaunda timu mpya? Kwa mahitaji ya kocha?

Hakuna kocha yeyote duniani anayekuja msimu wa usajili akasajili timu yote mpya. Inawezekana hii ikawa ni hapa tu Tanzania. Maana kusajili wachezaji hawa wote inamaana ni kuwaweka kando wale uliokuwa nao kabla. Kwa Mwalimu anayejenga kikosi cha ushindani kama Omog sidhani kama anaweza kufanya hivyo.

Siku zote mwalimu anasajili kwa kuona mahitaji yake sehemu fulani za timu na hawezi kupangua kikosi kizima maana kufanya hivyo ni kama kuanza moja katika kazi ya ualimu wa soka. Kwa kikosi alichokuwa nacho Omog kilikuwa siyo cha kupanguliwa chote, bali kuongezea kwenye sehemu zinazohitajika.

Haruna Niyonzima

Kinachofanyika sasa ni kama Simba inaunda kikosi kipya kabisa na kama hivyo ndivyo, hiyo itawasumbua msimu ujao licha ya kujaza majina. Imefika wakati tuache makocha waamue wachezaji wanaowataka badala ya kumlundikia wachezaji mwisho wa siku ni kuua vipaji vyao maana inawezekana kocha asiwaweke katika mipango yake.

Klabu za Simba na Yanga ndiyo zinaongoza kwa kuua vipaji vya wachezaji wengi maana wamekuwa wakisajili wachezaji bila kuwa na mahitaji nao ilimradi tu ana jina matokeo yake wachezaji hao wanashindwa kupata nafasi katika vikosi vyao na hatimaye kipaji vyao kuanza kupotea. Tuache haya yanayohusu ufundi yafanywe na wataalam wenyewe badala ya kuwaingilia na kuwajazia wachezaji.

Mbaya zaidi watu wanaofanya usajili huu ni wale waliojipambanua kwamba wanajua mambo ya soka, hakiki hili si suala la kulifumbia macho kwa maana ni hatari kwa maendeleo ya soka letu.

Kama nilivyosema hapo juu, kama kweli wanafuata matakwa ya kocha, basi Omog raia wa Cameroon atakuwa kocha wa ajabu anayeweza kusajili kikosi kizima na kuacha kile cha msimu uliopita.

Kumbuka msomaji kwamba, kikosi kilichopita cha Simba ndicho kilichotwaa ubingwa wa Kombe la FA na nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara, hivyo si vizuri kukibeza kikosi hicho.

Tusimalize maneno mengi hapa kwa kukosoa, tungoje tuone kitakachotokea katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Shirikisho Afrika ambako Simba itapambana kuwania ubingwa.

Stori: Maurid Kitenge | Championi

Leave A Reply