The House of Favourite Newspapers

Simba vs Yanga Mwisho wa Ubishi!

0

KUNA ubishi huko mtaani unaendelea kwa mashabiki wa Simba na Yanga ambao kila upande unasema timu yake itaibuka na ushindi na kutinga fainali ya Kombe Azam Sports Federation (ASFC).

 

Ubishi huo unakuja ikiwa zimebaki siku mbili kabla ya timu hizo hazijapambana katika mechi ya nusu fainali ya michuano hiyo itakayochezwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Wenyeji wa mchezo huo ni Simba ambapo mwisho wa ubishi utakuwa baada ya dakika tisini kukamilika. Kumbuka mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 11:00 jioni.

 

UBISHI ULIPO

Yanga wanaamini kwamba, rekodi nzuri waliyonayo msimu huu dhidi ya Simba ndiyo itawafanya kuwabeba na kuibuka na ushindi katika mchezo huu.

Rekodi ambayo Yanga wanatamba nayo ni ile ya kutopoteza mechi yoyote msimu huu ilipocheza dhidi ya Simba.

 

Timu hizo zimekutana mara mbili msimu huu katika mechi za Ligi Kuu Bara. Mara ya kwanza ilikuwa Januari 4, mwaka huu ambapo matokeo yalikuwa 2-2. Hapa Simba iliongoza kwa mabao 2-0, Yanga ikasawazisha.

 

Mechi ya pili ilikuwa Machi 8, mwaka huu ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na nyota wake, Bernard Morrison kwa faulo ya moja kwa moja kipindi cha kwanza.

 

Kwa upande wa Simba, wenyewe wanaamini kwamba kitendo cha kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa ni kwa mara ya tatu mfululizo, wana timu imara ambayo hivi sasa haiwezi kuzuiwa na yeyote yule.

 

VITA YA KIMATAIFA

Ugumu wa mchezo huu upo sehemu moja tu, katika kuweka heshima, lakini pia kusaka nafasi ya kucheza kimataifa.

 

Upande wa Simba, yenyewe ina nafasi tayari kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kutokana na kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, hivyo inataka kuikomoa Yanga.

Yanga yenyewe ili ishiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, lazima iwe bingwa wa michuano hii kwani inafahamika kwamba bingwa wa Kombe la Azam Sports Federation atashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

 

WATAKAOKOSEKANA

Mpaka sasa, kuna uhakika wa kuwakosa Mapinduzi Balama upande wa Yanga na Shomary Kapombe wa Simba ambao wote walipata majeraha hivi karibuni.

 

Balama aliumia mazoezini kwa kuvunjika kifundo cha mguu, huku Kapombe akiumia katika mechi ya robo fainali ya michuano hii ambapo alikanyagwa na kiungo wa Azam, Frank Domayo. Katika mchezo huo, Simba ilishinda 2-0.

Wakati hao wakikosekana kwa asilimia zote, Yanga kuna hatihati ya kuwakosa Haruna Niyonzima na Papy Tshishimbi ambao imekuwa ikiripotiwa hawapo fiti.

Simba wenyewe ukiondoka Kapombe, wengine wapo fiti, hivyo wana wigo mpana wa kikosi chao.

 

LAZIMA MTU ACHAPWE

Utamu wa mchezo wenyewe unakuja pale ambapo lazima mshindi apatikane baada ya dakika tisini kukamilika.

Hiyo inakuja kutokana na mchezo wenyewe ni wa mtoano, muda wa kawaida ukimalizika kwa sare, penalti zitahusika katika kusaka mshindi. Hivyo lazima mtu achapwe.

 

SAFARI ZAO

Hadi kufikia nusu fainali, Yanga imecheza mechi nne ambapo matokeo ya mechi hizo ni;

Yanga 4-0 Iringa United, Yanga 2-0 Prisons, Yanga 1-0 Gwambina na Yanga 2-1 Kagera Sugar.

Simba yenyewe nayo imecheza mechi nne hadi kufikia nusu fainali. Matokeo ya mechi zake ni;

Simba 6-0 Arusha FC, Simba 2-1 Mwadui, Stand 1-1 Simba (Simba ikashinda kwa penalti 3-2) na Simba 2-0 Azam.

Wakati Simba na Yanga zikicheza kesho Jumapili, leo Jumamosi inapigwa mechi ya kwanza ya nusu fainali kati ya Sahare All Stars dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

JIMMY MICHAEL, Dar es Salaam

Leave A Reply