The House of Favourite Newspapers

Simba Yajichimbia Jeshini Kujiandaa na Ligi Kuu

0
Kikosi cha Simba

Sweetbert Lukonge | Championi Jumatano | Habari

BAADA ya Jumamosi iliyopita Simba kutinga fainali ya Kombe la FA, jana Jumanne kikosi cha timu hiyo kiliingia kambini kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya African Lyon utakaochezwa Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Simba imeingia kambini katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Dege Beach iliyopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi la Simba, aliliambia Championi Jumatano kuwa, kikosi chao kitakuwa kikifanya mazoezi yake mara mbili kwa siku ambapo asubuhi kitakuwa katika uwanja uliopo ndani ya kambi hiyo na jioni kitakuwa kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Polisi kilichopo Kurasini Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana na taarifa hizo Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alikiri na kusema: “Ni
kweli tumeingia kambini kwa ajili ya maandalizi yetu ya mechi zetu zilizobakia.

“Kusema kweli hatutaki mchezo kabisa katika mechi hizi kwani tunataka tushinde zote ikiwa ni pamoja na ile ya fainali ya Kombe la FA, ndiyo maana uongozi wetu umeamua kutuleta jeshini ambako kuna utulivu zaidi,” alisema Mayanja. Kwa sasa Simba inaongoza katika msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 59 na ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 56.

Leave A Reply