The House of Favourite Newspapers

Simulizi Baba Aliyeuawa na Mwanaye Moshi

0

HAI: Kuna methali ya Kiswahili isemayo; “Hii pweke ni uvundo, kuondokewa si kwema!”

Simulizi ya baba ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Muroma Kata ya Masama wilayani Hai, Moshi mkoani Kilimanjaro, Welanzari Kimaro (60), anayedaiwa kuuawa na mwanaye inatafsiri msemo huo.

Kimaro alipoteza maisha hivi karibuni kwa kukatwakatwa mapanga na mwanaye.

Waombolezaji kutoka ndani na nje ya kijiji hicho walihudhuria maziko ya Kimaro aliyefariki dunia papo hapo wakati akitengeneza ukuta wa miti inayozunguka nyumba yake iliyopo kwenye Kitongoji cha Kiduruni kijijini hapo.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, anayedaiwa kutekeleza mauaji hayo ni mtoto wa wanne kati ya watano aliowazaa Kimario.

Imeelezwa kwamba, mbali na kumsababishia umauti Kimario, pia alimjeruhi mama yake mzazi aliyekuwa akiandaa kifungua kinywa.

Mama huyo Joyce Swai (51) alijeruhiwa katika sehemu za mguu kabla ya kupiga kelele akiomba msaada kwa majirani ndipo kijana huyo akatoweka kusikojulikana ambapo anasakwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro.

Mashuhuda hao wameeleza kwamba, baada ya kujeruhiwa, mama huyo alikimbizwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC ii kuokoa uhai wake kisha kurejea nyumbani kwa mazishi ya mumewe kipenzi.

Akizungumza wakati wa tukio la kumpumzisha mumewe huyo, mama huyo alisema amejifunza kitu kupitia changamoto hiyo aliyoipitia.

Kama methali inavyosema; “Hakuna kilima bila kaburi!” Mwili wa marehemu ulilazwa kwenye nyumba yake ya milele katika shamba la ukoo wa Kimario, mbele ya waombolezaji takriban 400.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na IJUMAA, waombolezaji katika msiba huo walisema kutokea kwa tukio hilo kumewapa funzo juu ya malezi ya vijana wao na jamii kwa jumla.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Masama Kati, Kandata Kimaro alisema; “Msiba huu umeshtua wengi, umesikitisha wengi, haukuwa umepangika, lakini maandiko matakatifu yanasema kuweni tayari muda unaofaa na usiofaa.”

Hata hivyo, Kimaro alijitolea kumsomesha mtoto mmoja wa marehemu ambaye mwaka ujao atakuwa darasa la saba.

Naye Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), John Njau aliwataka waombolezaji kutambua kuwa hakuna kifo kizuri au kibaya, bali kifo ni kifo tu.

“Hakuna kifo kizuri au kibaya; kifo ni kifo tu, kifo ni adui, kinakutenga na wale uwapendao, baba yeye amekwenda, hatuwezi kuongeza zaidi,” alisema.

Njau ambaye alishirikiana na Mwinjilisti Onesmo Makere wa Usharika wa Muroma kuongoza ibada ya maziko alisema; “Naomba sana, watu wasiongeze chuki katika hili, funga mdomo wako katika hili, laaniwa huyu shetani, kijana huko aliko akutane na Yesu, arudi, amwombe msamaha mama yake na ninaamini atasamehewa.”

Stori: Mwandishi Wetu

SOMA HABARI kwenye Gazeti la Ijumaa Jan-01,
Kwa nusu bei tu

Gazeti la Ijumaa👉http://bit.ly/3o8t0Fy

Gazeti la Championi👉https://bit.ly/3rDT9hT

Pakua App ya Global APP kupiti👇
iOS👉 https://apple.co/38HjiCx
Android 👉 http://bit.ly/38Lluc8

 

Leave A Reply