Simulizi ya Christian Bella; Mambo yaanza kumwendea vizuri…

Christian Bella & Malaika Band - AmerudiTunazidi kusonga mbele na simulizi hii ya Maisha Halisi ya Christian Bella ‘King Of The Best Melody’, ambapo wiki iliyopita Bella aliishia kusimulia jinsi usiku wa kuamkia siku ya kufanya usaili ambao ungemruhusu kuingia au kutemwa kwenye Bendi ya Chateau du Soleil ulivyokuwa mgumu kwake kiasi kwamba ilikuwa vigumu mno kuupata usingizi usiku huo, mawazo yake yote yakiwa kwenye usaili huo tu.

Nini kiliendelea? Teremka nayo.

BELLA anaendelea kusimulia kuwa, hatimaye kulikucha na kwa haraka sana saa za kufanya usaili zilifika na kumkuta akiwa kwenye eneo la tukio ambako ndiko yalikuwa makao makuu ya bendi hiyo ya Chateau du Soleil.
“Nikiwa kwenye chumba cha usaili mapigo ya moyo wangu yalikuwa yanakwenda mbio sana, japo nilikuwa najiamini lakini nilifahamu lolote lingeweza kutokea, kuambiwa nimepita au la, nilijiandaa kupokea majibu ya aina yote lakini jibu la kupita ndilo nililitegemea zaidi.”
“Usaili ulianza, Frank Isekya na jopo la watu wake waliokuwepo kunisikiliza waliniuliza ikiwa niko tayari kuanza kuimba nikawaambiwa ndiyo, wakaniruhusu. Sikutaka kufanya makosa kabisa, nilihakikisha natumia uwezo wangu wote na kipaji Mungu alichonijalia, mwisho wa siku nilifanikiwa kupita,” anasema Bella na kuongeza kuwa;
Majibu ya yeye kupita yalimfurahisha sana kiasi kwamba yakaibua matumaini mapya katika kufikia malengo yake kwenye tasnia hiyo ya muziki Kongo.
Lakini kabla ya kusonga mbele zaidi anasema aliamua kurudi nyumbani kwao kwenda kuwaomba radhi wazazi wake kwa kitendo chake cha kuacha shule na kuondoka nyumbani huku akiwataka kummwagia baraka zao aendelee kukomaa kwenye kile alichohitaji kufanya kwa ajili ya maisha yake.
“Wazazi walinipokea na kusikiliza kile nilichowaomba, sasa kutokana na utamaduni wa kwetu Kongo, mzazi anapoamua kukupa baraka zake katika jambo lolote hutakiwa kukumwagia maua. Hicho ndicho baba yangu alichofanya, alinimwagia maua ikiwa ni ishara ya kunipa baraka na kuniruhusu kusonga mbele katika muziki.”
“Niliondoka nyumbani moyo wangu ukiwa mweupe, nikazidi kukaza kwenye muziki, ndani ya muda mchache nikatokea kukubalika sana kwenye bendi hiyo niliyoanza kufanyia kazi, wakanipa cheo cha kuwa kiongozi wa wasanii wenzangu, nikatakiwa pia kuongoza jahazi katika kutengeneza albamu mpya ambayo tuliipa jina la Yako Wapi Mapenzi kwa Kilingara.”
Bella anazidi kusimulia kuwa albamu hiyo ilikuwa na mapokezi mazuri pia ilichangia jina lake kuanza kusambaa jijini hapo Kinshasa na sehemu zingine za Kongo, watu wengi wakiwemo wasanii wakubwa wakaanza kumfahamu, anasema hata tajiri yake Frank Isekya alizidi kumpenda.
“Hongera sana aisee kwa mafanikio ya mwanzo,” nilimwambia nikimpa ‘time’ apumue kidogo na kubugia mafunda kadhaa ya kinywaji chake, alipotua glasi mezani na kupokea hongera zangu, nilimuuliza tena;
“Vipi kuhusu msichana wako ambaye mlikuwa mnapendana, wakati huo bado mlikuwa wote kwenye uhusiano?”
“Ndiyo bado nilikuwa naye. Lakini kama nilivyokwambia awali alikuwa bado anatia ngumu mimi na yeye kufanya mapenzi.”
“Unataka kusema hukuwahi kufanikiwa kutoka naye?”
“Hapana nilifanikiwa.”
“Ilikuwaje mpaka ukafanikiwa?”
“Ha! Ha! Ha! Haaa!,” Bella alicheka huku akiinua mkono wake wa kulia na kutengeneza kofia yake kichwani, baada ya hapo aliweka pozi na kuanza kufunguka.
“Kipindi fulani bosi wangu Isekya alirudi kutoka Ulaya na zawadi nyingi kwangu yakiwemo mavazi, simu na pesa. Aliponikabidhi zawadi hizo nilimuomba mpenzi wangu huyo tukakae hotelini kwa siku kadhaa, akakubali, sasa huko ndiko nilikofanikiwa kufanya naye mapenzi kwa mara ya kwanza.”
“Ni kweli ulikuta hajawahi kufanya mapenzi?”
“Ha! Ha! Haaa! Achana na hayo mambo bwana, lakini huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa safari yetu ya uhusiano katika muonekanano mpya maana mara kwa mara tulikutana na kufanya mapenzi, baadaye alifanikiwa kunasa ujauzito,” anasema Bella.

Je, nini kitaendelea? Bella amempa msichana ujauzito, wataishia wapi? Vipi Kuhusu mafanikio yake kimuziki mpaka anafika Tanzania? Usikose wiki inayokuja.

Loading...

Toa comment