The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Mpoto: akumbuka baba yake alivyotaka kumuua

0

????????????????????????????????????

MPENZI msomaji wa simulizi hii tamu na ya kusisimua ya Mrisho Mpoto inayoelekea ukingoni, wiki iliyopita katika gazeti hili tuliishia pale Mrisho alipoanika kwa mara ya kwanza kuwa hajawahi kukutana na skendo yoyote ya maisha kutokana na malezi aliyopitia kwa mama yake.

Mrisho alienda mbali zaidi na kuanika sababu zilizomfanya kukwepa skendo hizo huku akimuhusisha mke wake, Mariam ambaye ni mtu wa swala (swala tano) kumfanya awe mtakatifu.

Songa nayo mwenyewe sasa…

Mrisho ni tukio gani kubwa ambalo huwezi kulisahau maishani mwako ambapo ukikumbuka huwa unaumia sana? Namuuliza kichokozi…

“Kabla sijajibu swali hilo na kuendelea na simulizi hii ya kweli ya maisha yangu, ni kwamba nimepokea simu nyingi za kila mmoja kuongea yake baada ya kuongelea skendo. Ukweli utabaki palepale kwamba sijawahi maishani kukumbana na skendo ya kuniumiza na kushindwa kufanya kazi zangu.

“Baada ya kusema hayo tunaweza kuendelea na simulizi hii ni kwamba miongoni mwa matukio ambayo bado yapo akilini mwangu na ni ngumu kutoka yaani nalikumbuka mara nyingi ni lile la baba yangu mzazi kumuamuru mama anipeleke porini nikafie huko sababu ikiwa ni kuzaliwa na alama ya ajabu niliyonayo shingoni.”

(anarefusha mkono wake hadi shingoni na kunionesha alama hiyo).

“Kiukweli ni jambo lililokuwa linanikosesha raha lakini baada ya kupata mafanikio niliyonayo hadi sasa, baba yangu alinitafuta kama nilivyoelezea hapo awali na kuniomba msamaha ambapo nilimkubalia na kumuunganisha na mama (marehemu) na baada ya hapo alianza kufariki dunia mama kisha akafuatia baba.”

Pole sana Mrisho kwa simulizi hii, labda ujumbe kwa vijana wanaohitaji kufikia mafanikio uliyonayo unawaambia nini?

“Kikubwa ni kutokata tamaa katika maisha, pili ni kujiamini kwa kile unachokifanya bila kujali umesoma ama hujasoma, kama nilivyoelezea katika simulizi yangu hii mambo niliyopitia sikukata tamaa, mafanikio niliyonayo sasa mpaka namiliki kampuni kubwa zaidi ya tatu ambazo ni Mpoto Foundation, Mpoto Arts and Gallery, International Market (IM) na nyingine nyingi ambazo zote hizi si mtu niliyesoma, elimu yangu ni darasa la saba lakini niko sawa na mtu mwenye elimu ya juu kabisa.

MWISHO.

Leave A Reply