The House of Favourite Newspapers

Sina Shaka na Kamati, Wakati Mwingine Tuanze Mapema

Mwenyekiti wa Kamati Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda.

MACHI 22, mwaka huu, Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itakuwa na mchezo wa mwisho na muhimu wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2019) dhidi ya Uganda. Mchezo huo unaoatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Taifa Stars inatakiwa kushinda ili kuwa na nafasi hiyo ya kufuzu Afcon kwa mara ya pili katika historia yake.

 

Si kushinda tu kwamba itatosha Taifa Stars kufuzu Afcon, pia iombe Cape Verde na Lesotho zitoke sare ya aina yoyote ile kutokana na timu hizo kuwa na mchuano mkali na Taifa Stars.

 

Ukiangalia Kundi L ambalo lina timu za Uganda, Taifa Stars, Lesotho na Cape Verde, Uganda tayari imekata tiketi baada ya kujikusanyia pointi 13. Lesotho na Tanzania zina pointi 5, lakini Lesotho ipo juu, huku Cape Verde ikiburuza mkia na pointi zake nne.

Huu ni mchezo muhimu kwetu kuona ile ndoto ya kushiriki Afcon kwa mara ya pili baada ya kupita takribani miaka 39. Mara ya mwisho kwa Tanzania kushiriki michuano hiyo ilikuwa mwaka 1980 ilipofanyika kule nchini Nigeria. Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, nimeona Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeunda kamati ya watu 14 ya kuisaidia Taifa Stars ishinde dhidi ya Uganda.

 

Sina shaka na kamati hiyo kwa sababu ina watu wengi wanaolifahamu soka na wana uchungu na nchi yao katika kufikia mafanikio kisoka.

 

Kamati hiyo imeundwa kwa malengo tofauti lakini kuu ni kutoa hamasa kwa Watanzania kuipa sapoti timu yao kwa kwenda uwanjani siku ya mchezo ili wachezaji waone nyuma yao kuna watu wanahitaji kupewa furaha. Imeundwa kamati kipindi hiki ambacho Watanzania wanahitaji kupata furaha kutoka kwenye timu yao ya taifa, furaha ambayo imepotea kwa muda mrefu.

 

Kikubwa hiyo kamati ifanye kazi yake kiukweli ili kukata kiu ya Watanzani wengi ambao hivi sasa wameonyesha kuipinga kwa kuona haina jipya zaidi ya kuingiza siasa kwenye soka letu ambalo bado lina safari ndefu kufikia kwenye mafanikio. Kama TFF imeona kuunda kamati hii ni sehemu ya kuifanya Taifa Stars ipate mafanikio, basi mliopewa dhamana mfanye kweli.

 

Lakini mbali na hilo, ishu za kuweka mikakati ya kuifanikisha timu ya taifa ifanye vizuri kwenye mashindano mbalimbali inapaswa kufanyika tangu mwanzo. Hii kuweka mkazo mwishoni ni nadra sana inatoa matokeo chanya. Kama tutakuwa tumefeli kipindi hiki, basi iwe fundisho kwetu kwa wakati ujao.

 

Mikakati iwepo kuanzia mwanzo hadi mwisho, sidhani kama ikiwa hivyo tutashindwa kufikia malengo yetu. Hebu tazama kundi letu, kama tungekuwa na mipango kabambe tangu mwanzo na kuiwekea mkazo, leo hii tungekuwa tunakamilisha tu ratiba tukiwa tayari tumefuzu.

 

Lakini hapo kati kuna kitu kama kujisahau na kuridhika kilipita, tukapoteza pointi kirahisi hasa zile ambazo tuliona kabisa uhakika wa kukusanya pointi tatu upo. Nikiachana na hilo, nirudi kwa vijana wetu wa Serengeti Boys ambao Aprili 14 hadi 28 watakuwa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana chini miaka 17 (Afcon U17) ambayo itafanyika hapa nchini.

 

Michuano hiyo inazishirikisha timu nane na makundi yapo mawili, Serengeti Boys ikiwa imepangwa Kundi A, ina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha inalibakisha kombe hilo hapa nyumbani. Kabla ya kushiriki michuano hiyo, kwanza itakwenda Uturuki kushiriki mashindano maalum ambayo yameandaliwa na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

 

Michuano hiyo itakayofanyika mwezi ujao, ni sehemu ya maandalizi ya Serengeti Boys. Hivi sasa kikosi cha timu hiyo kipo Arusha ambapo kimeweka kambi ya muda kabla ya kwenda Uturuki na kurejea nchini tayari kwa mashindano ya Afcon.

 

Tunapaswa kuwa nao vijana wetu hao bega kwa bega kuhakikisha wanaipeperusha vema bendera yetu ya taifa katika michuano hiyo ya Afcon. Kufanya kwao vizuri ni heshima kwao na taifa kwa jumla. Itapendeza sana kama kombe litabaki hapa nchini. Hatuwezi kufanikisha yote hayo kama hatutakuwa nao sambamba. Niwaombe tu Watanzania wenzangu tuwashike mkono hawa vijana ambao baadaye watakuja kuifanya Taifa Stars kuwa imara zaidi ya hapa ilipo.

Comments are closed.