The House of Favourite Newspapers

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (11)

0

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (11)

 

Tulikuwa katika mikono ya wanyang’anyi. Walikwisha tuamuru tushuke chini na tulitii kwa kuzihofia roho zetu kuondolewa na zile bunduki za majambazi.

 

“Haya, hatua ya kwanza weka simu katika mfuko. Ukikaidi utakiona cha mtema kuni!” aliamrisha jambazi mmojawapo. Kijana aliyebeba mfuko akaanza kukusanya simu zetu. Yangu niliiweka katika mfuko ule roho ikiniuma. Kuna mwanamume alikataa kutoa simu. Hakucheleweshwa, alipigwa usoni kwa kitako cha bunduki, simu akaitoa na maumivu akayapata.

 

Hatua ya kwanza ilikamilika. Simu zote zilikwenda. Ikafika hatua ya pili. Wote tulitakiwa kutoa fedha na kuziweka katika mfuko kama ilivyofanyika katika simu. Kijana yuleyule aliyekusanya mwanzo, akarudi tena akiwa na mfuko mwingine. Hakuona aibu! Ajabu sana!

 

“Weka fedha yote uliyonayo, ukipuuza utacheka na risasi!” jambazi aliamuru. Fedha zikaanza kuwekwa.

 

Ni bahati kwamba, fedha zangu nilizigawanya katika mafungu mawili. Fungu la kwanza lililokuwa na kiasi kikubwa nililiweka katika kaptura ndogo niliyovaa ndani. Fungu la pili, lilisheheni noti saba za shilingi 1000. Zote niliziweka katika mfuko wa suruali. Nilipofikiwa nilitoa kiasi chote kutoka mfuko wa suruali nikaweka katika mfuko wa jambazi.

 

“Ni hizi tu?” aliniuliza akinitazama kwa jicho la udadisi.

 

“Ndiyo mkuu,” nilijibu kwa nidhamu. Akaachana na mimi.

 

Walikusanya fedha wakatosheka. Jambazi aliyekuwa akitoa maelekezo mara zote akapiga risasi tatu juu, pengine kwa lengo la kututisha. Kisha kama mizimu, wakapotelea msituni.

 

Tuliondoa magogo yaliyotegwa njiani tukipeana pole. Wengi walilia. Nilikuwa miongoni mwao. Tofauti ni kwamba, wao walilia kwa sauti. Mimi nililia ndani kwa ndani. Hakuna aliyekisikia kilio changu.

 

Baada ya kusafisha barabara, nilimshuhudia dereva kwa mbali akitikisa kichwa. Akanyata kama mjinga, akakunja kona kali, akavuta ugoro kiasi kisha akapiga chafya ndefu iliyofanya mbavu zake saba zichomoze kama vijiti vya kuchokonolea meno! Huyo, akaingia ndani ya gari na kukaa nyuma ya usukani.

 

“Boboooooh!” ilipigwa honi. Tukaingia ndani ya gari. Nilimkuta yule dada jirani yangu amekaa kajiinamia. Nilitambua kilichomtesa. Muda wote wa safari alikuwa akichezea simu. Sasa simu ilichukuliwa na wajinga wale. Ili Kuepusha kuwa sehemu ya matatizo yake, sikumsemesha.

 

Safari ya Popo bado inaendelea… tukutane kesho.

 

NA: DAUD MAKOBA| GPL

Leave A Reply