The House of Favourite Newspapers

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume-12

0

ILIPOISHIA WIKIENDA
Sasa mawazo yangu yote yakawa kwenye kufungwa. Nilijiambia penzi langu na Eddy sasa linanipeleka jela!
Wakati ule mawazo yangu yanatangatanga nikapata wazo la kumpigia simu dada yangu nimueleze yaliyonikuta.

SASA ENDELEA…

Nikasimama chini ya mti uliokuwa kando ya barabara nikampigia simu dada yangu. Nilishukuru kwamba simu yangu ilikuwa na salio.
Dada yangu alipopokea simu aliniuliza:
“Umeshafika Unguja?”
“Nimefika lakini kumetokea matatizo.”
“Matatizo gani tena?”
Nikamueleza. Dada alishituka sana.
“Sasa dada nimekwama, naomba unitumie nauli nirudi Dar.”
“Nikutumie kiasi gani sasa?”
“Nitumie japokuwa elfu hamsini.”
“Ngoja nikutumie.”
Simu ikakatwa.

Wakati nainua uso, nikaona polisi wawili wanakuja huku wamenikodolea macho. Nikahisi kama walikuwa wananifuata mimi. Moyo wangu ukashituka ukawa unapiga kwa kasi. Nikahisi miguu yangu ikitetemeka.
Nikajiuliza nifanye nini, nisimame hapohapo polisi hao wanikamate, au nitoke mbio?
Nilikuwa tayari nimeshakusanya nguvu za kukimbia nilipobadili mawazo ghafla. Niliona nisikimbie, Nilijiambia nikikimbia nitajionesha wazi kuwa ni mwenye hatia. Na pia mimi ni mwanamke nisingeweza kushindana na wanaume wawili kwa mbio. Kwa vyovyote vile ningekamatwa kabla ya kufika popote.
Nikainamisha tena uso wangu na kuuelekeza kwenye ile simu, nikawa nabonyezabonyeza vitufe huku nikiwatazama polisi hao pembeni mwa macho.

Nikaona wanapita. Kumbe hawakuwa na shughuli na mimi. Waliponipa mgongo tu nikafyatuka na kukatiza njia nyingine. Wakati natembea kwa mwendo wa haraka nikasikia simu yangu ikitoa mlio wa kupokea meseji.
Nikaitazama huku nikiendelea kwenda. Nikaona meseji ya pesa kutoka kwa dada yangu. Alinitumia zile shilingi elfu hamsini nilizomuomba.

Sasa nikawa natafuta sehemu iliyokuwa na wakala ili nitoe zile pesa. Baada ya kupita kwenye maduka mawili matatu nikaliona duka lililokuwa na wakala wa mtandao niliokuwa nautumia. Nikaenda kutoa zile shilingi elfu hamsini.
Baada ya kupata pesa hizo nikakodi teksi iliyonipeleka bandarini. Nilipofika nilikwenda kuulizia kama kulikuwa na usafiri wa boti wa kwenda Dar.
Nikaambiwa kulikuwa na boti inaondoka saa kumi na mbili jioni, nikakata tiketi na kusubiri. Wakati nasubiri dada yangu akanipigia simu.
“Umeshatoa hiyo pesa?” akaniuliza  baada ya kupokea simu yake.

“Nimeshatoa, niko bandarini.”
“Umepata boti ya kurudi?”
“Nimepata lakini inaondoka saa kumi na mbili.”
“Hakuna inayoondoka muda huu?”
“Hakuna.”
“Sasa umeshakata tiketi?”
“Nimekata, nasubiri huo muda.”
“Basi jihadhari, usianze kutangatanga huku na huku.”
“Nitangetange wapi dadaa’ngu, mwenyewe nimenywea kama maji ya mtungi.”
“Nitakupigia baadaye.”
Dada akakata simu. Nikaendelea kusubiri pamoja na abiria wenzangu hadi muda wa kujipakia kwenye boti ulipofika. Tukajipakia. Saa kumi na mbili juu ya alama safari ikaanza.

Kabla ya kufika Dar, dada alinipigia simu mara tatu tukiwa baharini. Alikuwa akitaka kujua kama nilikuwa salama. Mara zote nilimjibu kuwa nilikuwa salama na safari ilikuwa inaendelea.
Tulifika Dar es Salaam usiku. Kabla ya kushuka kwenye boti nikampigia simu dada kumjulisha kuwa tumeshafika.
“Mwambie shemeji anifuate bandarini na gari,” nikamwambia.
“Anakuja. Msubiri.”
Nikakata simu.

Nilishuka kwenye boti nikatoka nje kabisa ya bandari kumsubiri shemeji.
Wakati naangazaangaza macho kila upande nikiwa na tamaa ya kuliona gari la shemeji likitokea, simu yangu ikaita. Nikajua ni dada. Nilipotazama namba nikaona si ya dada bali ni ya yule jini mzungu. Moyo wangu ulishituka!
Vile nilivyokuwa nimeduwaa nikiitazama, ile simu ilijipokea yenyewe ikajiongezea sauti. Nikaisikia sauti ya Smith ikiniambia:
“Kama unajaribu kunikimbia mimi utapata matatizo mengi.”
Sikujibu kitu nikanyamaza kimya huku nikijiona wazi kuwa nilikuwa natetemeka.

“Hivi sasa polisi wanakutafuta kwa mauaji ya Eddy na Eddy nilimuua mimi kwa sababu uliniambia huna mpenzi,” sauti ya Smith ikaendelea kuniambia.
Nikaendelea kunyamaza.
“Usalama wako ni kuwa na mimi. Ukiwa na mimi matatizo yote yatakwisha na kesi yako ya Zanzibar pia itakwisha. Sasa niambie kama uko tayari kuwa na mimi.”

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.

Leave A Reply