The House of Favourite Newspapers

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume-6

1

ILIPOISHIA WIKIENDA
Nikaondoka. Smith akarudi kwenye kiti na kuendelea kunywa pombe yake.
Nilikodi teksi iliyonirudisha nyumbani. Wakati wote nikiwa kwenye teksi hadi nafika nyumbani, yule mzungu alikuwa ametawala akili yangu.

Zile milioni kumi alizonipa pamoja na maelezo yake mengine yakiwemo yale aliyonieleza kuwa nikienda huko hotelini anakokaa atanipa zawadi ambayo sitaisahau maishani mwangu, yalikuwa yamenihamasisha. SASA ENDELEA…

Nilipofika nyumbani niliketi sebuleni na kufungua mkoba wangu nikatoa zile pesa. Niliziweka kwenye kochi kisha nikaanza kuzihesabu.

Zilikuwa shilingi milioni kumi kamili. Nikapanga kesho yake niende nikaziweke benki. Nikazirudisha pesa hizo kwenye mkoba kisha nikaendelea kumuwaza yule mzungu.
Niseme ukweli kuwa sikuwa nimewahi kushika shilingi milioni kumi mkononi mwangu. Ile ilikuwa ni mara yangu ya kwanza.

Kwa pesa hizo na kwa ahadi nyingine alizoniahidi yule mzungu nikawa nimepata tamaa ya kuwa naye kwa kuamini kwamba angeweza kuyabadili maisha yangu.

Binafsi nilikuwa nikitamani kupata gari langu mwenyewe lakini sikujua ningeanzia wapi hadi niweze kulipata. Pia nilitaka kumiliki nyumba yangu niachane na nyumba za kupanga lakini sikuwa na uwezo.
Yule mzungu ameniahidi kuwa naweza kuvipata vyote kama nitakubali kuwa naye. Sikuona kama kulikuwa na kikwazo cha kuwa naye. Mwanaume ambaye tuliahidiana kuja kuoana hakuwa amenichumbia na inawezekana akapata msichana mwingine na akabadili mawazo yake. Mwanaume si wa kumtegemea sana.

Nikakumbuka ile methali ya Kiswahili isemayo “Hamadi kibindoni, silaha ni iliyo mkononi.” Nikajiambia kwa wakati ule Smith ndiye aliyekuwa mkononi na ndiye ambaye ningeweza kumtumia.
Baada ya kuwaza kwa dakika kadhaa nilinyanyuka na mkoba wangu uliokuwa na shilingi milioni kumi na kuingia nao chumbani. Nilizifungia zile pesa kwenye kabati. Wakati nataka kubadili nguo nilizokuwa nimevaa, simu yangu ikaita.

Nilipoitazama nikaona namba ya Smith, nikaipokea,
“Hellow Mr Smith…!”
“Ndiyo ninatoka hapa hoteli,” Smith akaniambia kwenye simu.
“Mimi niko nyumbani nimepumzika kidogo.”
“Nilidhani unanifikiri mimi.”

“Wewe nimeshakufikiria.”
“Kwa hiyo umeshapanga utakuja lini nyumbani kwangu?”
“Nitakuja kesho.”

“Nitafurahi sana kukuona. Utakuja saa ngapi?”
“Saa moja usiku.”
“Ukitaka kuja unifahamishe.”
“Nitakupigia simu.”
“Sawa.”
****
Asubuhi ya siku iliyofuata nilipotoka nyumbani nilikwenda benki nikaweka shilingi milioni saba katika akaunti yangu. Shilingi milioni tatu nilibaki nazo mkobani mwangu.

Nilipotoka benki nilizunguka katika maduka mbalimbali nikajifanyia manunuzi ya shilingi milioni mbili. Baada ya kununua kila kitu nilichohitaji nilikodi teksi iliyonirudisha nyumbani Sinza.

Niliingia chumbani mwangu nikazijaribu nguo nilizonunua pamoja na viatu. Nikaona zilikuwa sawa. Nilichukua wigi ambalo nililinunua kwa shilingi laki tatu nikaenda saluni kupachikwa wigi hilo.
Nilipotoka saluni nilikwenda kumtembelea dada nyumbani kwake. Baada ya kusalimiana naye aliniambia.

“Umependeza leo?”
“Kwa sababu ya hili wigi?” nikamuuliza.
“Nalijua bei yake, bila laki tatu hulitoi dukani.”
“Ni kama hivyo, nimepata mchumba wa kizungu ndiye anayenipendezesha.”
“Usiniambie!”

Nikamdokeza dada kuhusu uhusiano wangu na yule mzungu.
“Awe na nia kweli ya kukuoa, asikudanganye akakuchezea kisha akaja kukuacha,” dada akaniambia.
“Atanichezea mimi, atajichezea mwenyewe! Mi shida yangu nimle tu kwa sababu nimeona pesa yake iko njenje.”

“Kama ni kumla umle taratibu. Kama una pupa kama hivyo utajikuta unaliwa wewe!”
“Kwanza yule mtu mwenyewe naona kama ana nia njema na mimi, sijui lakini. Bado naendelea kumchunguza.”

Niliendelea kuzungumza na dada hadi jua lilipokuchwa nikaondoka kurudi nyumbani kujiandaa kwenda kwa mzungu wangu.

Baada ya kuvaa nguo nilizopenda nitoke nazo nikampigia simu kumjulisha kuwa ninakwenda kwake. Akaniambia kwamba ananisubiri.

Nakumbuka ilikuwa saa kumi na mbili na nusu nilipotoka nyumbani. Nilikodi teksi iliyonipeleka katika hoteli ya Lux ambayo mzungu huyo alikuwa amepanga chumba.
Nilipofika nilimpigia tena simu, akaniambia alikuwa chumba namba 35. Nikaenda. Kilikuwa ghorofa ya kwanza. Nilipomaliza kupanda ngazi nilianza kukitafuta chumba namba 35. Nikakiona. Nikaenda kubisha mlango.

Kitu kilichonishangaza ni kuwa licha ya kubisha mlango kwa sekunde kadhaa sikupata jibu. Nikaujaribu mlango ambao ulifunguka, nikaingia ndani. Smith mwenyewe hakuwemo chumbani ila niliona suti yake kwenye kitanda. Sikujua alikuwa ametoka au amekwenda wapi.

Nikajaribu kufungua mlango wa bafuni. Nilichokiona kwenye macho yangu kilipasua moyo na kunifanya niache mdomo wazi kwa mshituko.
Je, nini alichokiona bafuni? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.

1 Comment
  1. Aisha Chumo says

    Pesa za bwerere wigi laki tatu

Leave A Reply