The House of Favourite Newspapers

Maambukizi katika viungo vya uzazi vya mwanamke (PID)

1

Blausen_0732_PID-Sites

Wiki hii mpenzi msomaji wangu namalizia aina za magonjwa yanayohusiana na mwanamke kupata muwasho na kutokwa na majimaji ukeni, Pelvic Inflammatory Diseases ‘PID.’

Ugonjwa huu hushambulia viungo vya ndani vyote vya uzazi vya mwanamke na kusababisha mwanamke apate maumivu chini ya kitovu na maumivu wakati wa kujamiiana kwa muda mrefu.

Maambukizi katika tabaka la ndani la kizazi huitwa ‘Endometritis’, maambukizi ya mirija ya uzazi huitwa ‘Salpngitis’ na pia mwanamke anaweza kupata uvimbe ndani ya kizazi ambao unakuwa umejaa usaha uitwao ‘Tubo-ovarian abscess’ na maumivu makali ya muda mrefu ya tumbo kuanzia usawa wa kitovu kushuka chini ‘Pelvic Peritonitis’.

Ugonjwa huu zaidi huenezwa kwa njia ya kujamiiana na husababishwa na bakteria ‘Neisseria Gonorrhoea’ na ‘Chlamydia Trachomatis’. Wengine wanaoweza kusababisha ni ‘Gardnella Vaginalis’, Haemophilus Influenza’, ‘Enteric gram negative rods’ na ‘Streptococcus agalactiae.’
Pia wapo wengine wengi inabidi kufanya uchunguzi ili kuthibitisha.

USHAURI
Ni kama ilivyo katika maambukizi mengine ambayo tumekwishaona. Vipimo ni vilevile vya ukeni na ambavyo daktari ataona vinafaa.

FANGASI UKENI
Tatizo hili pia huitwa ‘Vaginal Candidiasis’. Mwanamke hulalamika muwasho mkali ukeni, uke huvimba au huumuka, uchafu hutoka mweupe na mzito kama maziwa ya mgando na kuhisi moto ukeni, mkojo pia huwa wa moto na kuchomachoma njia ya mkojo.

Maumivu wakati wa kukojoa huwa makali endapo utajikuna sana ukeni na kupata michubuko. Mashavu ya ndani ya uke huwa mekundu na maumivu.

Ugonjwa huu hufanana na ugonjwa wa malengelenge ukeni ‘Genital herpes’ na husababisha ugonjwa wa kubana mlango wa uke kwa kuvimba na maumivu ya uke ‘Vulvodynia’.
USHAURI

Ugonjwa huu huchunguzwa kama yale mengine ili kupata uhakika.

NINI CHA KUFANYA?
Magonjwa haya ya ukeni hushabihiana na saratani za ukeni na shingo ya uzazi. Kwa kuwa vyanzo vikuu ni ngono basi ni vema ukapima magonjwa yote ya zinaa na Ukimwi.
Athari za magonjwa haya ni katika mfumo wa uzazi, hayo nayo uchunguzwa kwa makini na uchunguzi hufanyika kwa mwanaume na mwanamke, pia athari ziangaliwe na kwa mwanaume kwani mfumo wake wa uzazi pia huathirika.

Vipimo vya awali kwa mwanamke ni mkojo, vipimo vya ukeni na shingo ya kizazi, vipimo vya damu na Ultrasound na hata kupima mirija ya uzazi.

Mwanaume atapimwa mkojo, damu na manii zake kuangalia ubora na uwezo wa mbegu za kiume. Muone daktari katika hospitali ya mkoa kwa uchunguzi wa kina na tiba.

1 Comment
  1. Angela says

    Nashukuru sana kwa haya mafunzo. Watu wengi wana haya matatizo lakini huogopa ku share. Swali langu ni je kuna tiba Ya haya magonjwa?

Leave A Reply