The House of Favourite Newspapers

STEVE NYERERE: BONGO MOVIE NI KIWANDA KIKUBWA

0
Steve Nyerere.

KAULI mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ya Tanzania ya viwanda, inaelekea kuanza kueleweka miongoni mwa makundi mbalimbali ya kijamii. Wiki iliyopita, mmoja wa wasanii wa vichekesho nchini, ambaye pia ni muigizaji nyota, Steve Mengere maarufu kama Steve Nyerere aliwakutanisha mastaa wenzake katika viwanja vya Makumbusho jijini Dar es Salaam na kuzungumza nao mambo kadhaa, kubwa likiwa ni kutambulisha projekti mpya, iitwayo Uzalendo Kwanza ambao ndani yake umebeba mambo mbalimbali ya wasanii.

Uzalendo kwanza ni mradi unaowajumuisha watu wa kada mbalimbali wakiwemo wasanii, watangazaji, wanasoka na mastaa wengineo. Katika siku hiyo ya Stori uzinduzi, jambo moja la kushangaza ni pale msanii huyo alipoweza kuwakutanisha wanandoa walioachana, Mike Sangu na Salome Urassa ‘Thea’ na wawili hao wakakumbatiana na kupiga picha ya pamoja, licha ya kuwa Mike, alikuwa na mkewe mpya ambaye pia alikumbatiana na Thea, Ummy.

Walikuwepo pia wasanii ambao walijijengea bifu kwa sababu ya ‘kushare’ mabwana katika siku za nyuma, lakini siku hiyo walimaliza matatizo yao na kuwa kitu kimoja kuonyesha uzalendo, ikiwa ni pamoja na Steve mwenyewe kumaliza tofauti zake na Wastara Juma.

Akizungumza juu ya suala hilo, Steve ambaye ndiye mwanzilishi wa Uzalendo Kwanza, alisema sababu za kuwakutanisha watu wote waliokuwa na bifu ni kuendeleza tasnia ya filamu ambayo mwisho wa siku ni ajira inayowaingizia kipato.

“Unajua mimi nilipewa jukumu la kuwaunganisha watu wote waliokuwa hawaongei kwa ajili ya kuleta uzalendo kwanza na kuwasaidia wale wanaoitegemea sanaa hii kwa sababu unaweza kukuta wanagombana watu wawili, lakini wanawaumiza watu wote hasa wale walioko chini,” alisema Steve. Steve alisema alikuwa akipata taabu kubwa alipokuwa akikutana na vigogo wa serikali katika matamasha mbalimbali, walipomuuliza kuhusu Bongo Movies, kwani alikosa majibu sahihi ya
kuwapa.

“Uzalendo kwanza ni mradi wenye nia ya kumuunga mkono Rais Magufuli, tasnia yetu ya filamu ni kubwa na hiki ni kiwanda kikubwa mno. Watu wote wa tasnia hii wanatengeneza kiwanda kikubwa sana ambacho ni chanzo cha mapato.

“Tasnia hii haiwezi kufanikiwa kama watu watakuwa si wazalendo, tunataka kuzunguka nchi nzima ili kuwahamasisha watu wawe wazalendo kwa nchi yao, wanunue kazi za filamu za nyumbani, wanunue vitu vinavyotengenezwa na watanzania wenzao, hapa ndipo kauli mbiu ya Rais Magufuli itakapotimia.

“Ndiyo maana mradi huu unakutanisha wadau wa aina mbalimbali, tunao wachezaji wa mpira, tuwashabikie  wachezaji wetu, tuwape kipaumbele, projekti hii ni endelevu, tutasafiri mikoa mbalimbali kuwaunganisha watu kisanaa, kikazi pamoja na wana uzalendo kwa ujumla,” alisema.

Pia watawasaidia watu mbalimbali wenye matatizo, ikiwa ni pamoja na kupita katika hospitali tofauti kutoa msaada kwa wagonjwa na wale waliopo majumbani wakisumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.

Katika kulinda maadili na uhalali wa mradi huo kamambe, Steve aliwaonya wasanii wa filamu kulewa hovyo na kufumaniwa kwani muungano huo wa sasa hauhitaji skendoskendo za ajabu.

“Skendoskendo za ajabu itabidi tuziache jamani kwani uzalendo kwanza huwezi kuhamasisha wakati na wewe si mzalendo, maana itakuwa ni kichekesho kwa kuwa mzalendo halisi ni yule ambaye hana skendo za ajabu na ambaye hana chuki na mwenzake,” anasema Steve.

STORI: IRENE MNYITAFU| RISASI

 

William Ngeleja: Seduce Me ya Alikiba Sio Level ya Tanzania

Leave A Reply