The House of Favourite Newspapers

Stevie Wonder: Alizaliwa Kipofu Lakini Sasa ni Bilionea

0

KWENYE maisha, kama binadamu, kuna kipindi unakata tamaa ya kuishi. Unapotazama mbele yako, hakuna tumaini, hakuna mwanga, giza nene limetawala. Una marafi ki unaowafahamu, hawajafanikiwa.

 

Hao hawawezi kukufanya ufanikiwe. Wengi watakurudisha nyuma na kukuvunja moyo. Nione mimi nimezaliwa kipofu, lakini ni bilionea. Amini kuwa lisilowezekana linawezekana.

 

Dunia ni mahali pa kupendana na kumjali kila mtu!” Haya maneno ya mwanamuziki mwenye mafanikio duniani, raia wa Marekani, Stevland Hardaway Morris. Dunia inamjua kwa jina la Stevie Wonder ambaye amezaliwa na tatizo la kutoona (kipofu), lakini hakujali ulemavu wake, badala yake ameweka alama duniani.

 

AWEKA REKODI ZA MUDA WOTE

Mwamba Stevie Wonder ambaye amezaliwa mwaka 1950 huko SaginawMichigan nchini Marekani amesikika mno kwenye nyimbo nyingi zilizoweka rekodi za muda wote na kugusa mioyo ya mabilioni ya watu duniani.

 

Baadhi yake ni From The Bottom Of My Heart, I Wish, All I Do, A Time To Love, My Eyes Don’t Cry, For Your Love, Living For The City, A Place In The Sun, Get It na nyingine zaidi ya 300, akishirikiana na wakongwe wengi wa muziki duniani kama Michael Jackson, Elton John na wengine.

 

AMEZALIWA NJITI

Stevie Wonder amezaliwa akiwa njiti, wiki sita kabla ya muda maalum wa kuzaliwa. Madaktari walipomwangalia, wakagundua alikuwa na tatizo ambalo kitaalam linaitwa Retinopathy of Prematurity (ROP). Hali inayoharibu ukuaji wa macho na kuifanya nuru iliyokuwepo machoni kutokufanya kazi. Hali hii ndiyo ilimpa Stevie upofu hadi leo.

ABADILISHWA JINA LA UBINI

Huyu mwamba alipokuwa na umri wa miaka minne tu, wazazi wake wakatengana hivyo mama yake akamchukua na kumpeleka katika Jiji la Detroit, Marekani. Huko akabadilishwa jina lake la ubini kutoka Lula Hardway na kuwa Moris. Japokuwa alikuwa kipofu, lakini maisha yake yote ya utotoni alikuwa mtu wa kupiga vyombo vya muziki vikiwepo magitaa, vinanda, piano, drums na vingine.

 

MWANGA WA MAFANIKIO

Akiwa na umri wa miaka 11, Stevie aliimba wimbo wake wa kwanza ulioitwa Lonely Boy. Kutokana na wimbo huo kuwa mkali, Mkurugenzi wa Lebo ya Motown, Berry Gordy, akaona kwamba dogo angechukuliwa na lebo nyingine hivyo fastafasta akazungumza na mama yake kisha akasaini naye mkataba.

 

Mkataba ambao ulimfanya Stevie kulipwa Dola za Kimarekani 2.5 kila siku (zaidi ya shilingi 5,000), fedha ambayo ilikuwa ni nyingi mno kwa kipindi hicho.

 

Hapo ndipo ilipoanza safari yake ya mafanikio makubwa kwani hakuishia hapo, bali aliendelea kutunga nyimbo kali na mwaka 1963 akiwa na umri wa miaka 13, akatengeneza albam yake aliyoipa jina la The 12 Year Old Genius ambayo ilikuwa na wimbo mkali wa Fingertips. Wimbo huu ulishika hadi namba moja kwenye orodha ya Billboard ya nyimbo kali 100 mwaka 1963.

 

MOTOWN YATAKA KUMTEMA

Japokuwa alikuwa na mafanikio, lakini alipoanza kukua, sauti yake nzuri ikaanza kubadilika, ikaanza kuwa mbaya kiasi kwamba Motown wakataka kusitisha mkataba wake ila akaambiwa ampe nafasi ya pili aone itakuwaje.

 

Stevie alipopewa nafasi ya pili, hakutaka kulala, hakuzubaa zaidi ya kufanya mazoezi ya sauti kwani aliamini ndicho ambacho kingemfanya kupambana na kufanikiwa japokuwa alikuwa na ulemavu wa macho. Kupambana kwake huko kukampa umaarufu mkubwa duniani. Kila aliposimama jukwaani, miwani ilikuwa machoni mwake, aliimba kwa hisia kali, nyimbo nzuri ambazo ziliendelea kuishika mioyo ya wanadamu.

 

FAMILIA

Stevie alioa, akaacha, akaoa tena. Mara baada ya kufanikiwa, mwaka 1970, Stevie aliamua kumuoa mpenzi wake wa muda mrefu, Syreeta Wright, lakini wala hakukaa naye sana, mwaka 1972, akaachana naye. Ndoa yake nyingine ilikuwa mwaka 2001 ambapo alimuoa mbunifu wa mavazi, Kai Millard ambaye naye aliachana naye mwaka 2012.

 

MAFANIKIO KIMUZIKI

Kama ilivyo kwa wanamuziki waliofanikiwa, basi naye Stevie amefanikiwa kwa kuchukua tuzo nyingi. Ana tuzo mbili za Academy. Ana tuzo 18 za American Music. Tuzo 3 za Golden Globes. Tuzo 17 za Grammy na nyingine nyingi. Mbali na tuzo hizo, pia amewahi kuwa miongoni mwa watu walioalikwa katika Ikulu ya Marekani (White House) na kukabidhiwa medali ya heshima na aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama.

 

MAFANIKIO KIFEDHA

Kwa sasa unapomzungumzia Stevie, kwanza unamzungumzia mwanamuziki mwenye mafanikio makubwa kimuziki. Pia unamzungumzia mtu mwenye utajiri wa Dola za Kimarekani milioni 110 (zaidi shilingi bilioni 220 za Kitanzania). Stevie anamiliki mjengo wa kifahari wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 2 (zaidi ya shilingi bilioni 4 za Kitanzania).

 

STEVIE WONDER ANA SOMO KUBWA

Stevie ana somo kubwa mno. Baadhi ya binadamu wanapowaona waliozaliwa na ulemavu au wao wenyewe kuwa walemavu, wanaamini ni vigumu kufanikiwa. Lakini Stevie anawaaminisha kwamba hata wao wanaweza kufanikiwa. Sasa kama wenye ulemavu wamefanikiwa, vipi kuhusu wewe? Unaweza kufanikiwa pia!

Makala: Amina Said, Bongo

 

Leave A Reply