The House of Favourite Newspapers

Straika mpya Yanga Apambwa Kila kona

0

 

WAKATI uongozi wa Yanga ukiendelea na harakati zake za kukisuka upya kikosi cha timu hiyo, kiungo wa zamani wa Simba, Mkenya, Jerry Santo, amesifu usajili wa mshambuliaji kutoka Gor Mahia ya Kenya ambaye ni raia wa Ivory Coast, Ghislain Yikpe Gnamien, akidai jamaa ni bonge la straika.

 

Yanga inadaiwa kuwa katika harakati za kutaka kumsajili Gnamien kwa ajili ya kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji wa timu hiyo. Tayari straika huyo yupo nchini kwa ajili ya kumalizana na Yanga.

 

Hata hivyo, licha kuwepo kwa taarifa kuwa Yanga imemalizana na mchezaji huyo lakini ukweli ni kwamba bado hajasaini mkataba wowote na timu hiyo kutokana na wahusika wanaosimamia mchakato mzima wa usajili kuwa nchini Afrika Kusini walipoenda kumalizana na kiungo wa Mamelodi Sundowns ambaye anacheza kwa mkopo UD Songo ya Msumbiji, Luis Jose Miquissone.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Santo alisema kuwa, Gnamien ni mshambuliaji mzuri ambaye anaweza kuwasaidia Yanga kama watamsajili.

“Jamaa ni mzuri kwani amekuwa akitusumbua sana katika ligi ya hapa Kenya, ana nguvu lakini pia anajua sana kukaa na mpira.

 

“Kwa hiyo, kama Yanga watamsajili naamini atawasaidia,” alisema Santo ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu ya Simba pamoja na Coastal Union ya Tanga.

Wakati Santo akisema hayo, Mtanzania anayecheza pale Gor Mahia, Dickson Ambundo naye amesema kuwa jamaa yuko poa huku akiamini ana nafasi ya kuwabeba Yanga.

“Jamaa yuko poa sana, ana uwezo na ataweza kuwabeba kama ambavyo alikuwa huku Gor Mahia,” alisema Ambundo ambaye kabla ya kwenda Kenya alikuwa Alliance ya Mwanza.

Naye kipa Mtanzania, David Kisu Mapigano, anayeidakia Gor Mahia, alisema mshambuliaji huyo ni hatari sana kwani anajua kufunga mabao lakini ana nguvu ambazo akikutana na mabeki wazembe huwa inakula kwao.

 

“Ni mchezaji mzuri sana, anajua kufunga, lakini pia huwa ana kasi mno huku akiwa amejaliwa nguvu, ukiwa beki mzembe atakusumbua sana kwani muda mwingi hutumia nguvu zake bila kuchoka katika kulazimisha kufunga au kutengeneza nafasi.

“Kwetu sisi wachezaji wa Gor Mahia tulikuwa tukimuona Yikpe kaingia na mpira kwenye boksi la maadui tulikuwa tunaanza kushangilia maana tunajua kuwa atafunga bao, mara nyingi imekuwa hivyo,” alisema kipa huyo.

 

Straika huyo katika mechi ya watani wa jadi wa Kenya kati ya Gor Mahia na AFC Leopards aliifungia mabao mawili kikosi chake katika ushindi wa mabao 4-1. Mechi hiyo ilipigwa Novemba 10, mwaka huu.

Kama straika huyo atasaini mkataba na Yanga atakuwa miongoni mwa nyota wapya ambao wamesajiliwa na kikosi hicho wengine ni Haruna Niyonzima, Adeyum Saleh, Ditram Nchimbi na Tariq Seif.

WAANDISHI: Sweetbert Lukonge, Lunyamadzo Mlyuka, Said Ally na Marco Mzumbe

 

Leave A Reply