Sure Boy Mbadala wa Aucho Yanga

RASMI sasa kiungo mchezeshaji wa Azam FC, Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ anatua Yanga kuwa mbadala wa Mganda, Khalid Aucho.

 

Hiyo ni katika kuelekea usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu
katika usajili wa msimu huu.
Sure Boy ni kati ya wachezaji ambao walisimamishwa kwa muda
usiojulikana kutokana na utovu
wa nidhamu alioufanya pamoja na wenzake Mudathiri Yahya
na Aggrey Morris.


Chanzo cha habari kutoka
kwa rafiki wa karibu ndani ya Azam, kimeliambia Championi Jumatano
kuwa, Yanga wapo katika
hatua za mwisho kwa ajili ya kufanikisha usajili wake.


Kilisema kuwa Yanga
wanataka kumsajili Sure Boy kwa ajili ya kuongeza kiungo mwingine mzawa mwenye uwezo wa kukaa na mipira, kuchezesha timu ndani ya wakati mmoja kama ilivyo kwa Aucho.

 

Kiliongeza kuwa katika michezo miwili iliyopita ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting na Namungo FC, alikosekana Aucho kutokana na majeraha na timu kuonekana kushindwa kumiliki mpira kwa muda mrefu kabla ya kuchukua maamuzi ya kuongeza mbadala wake.


“Kocha amependekeza
tumsajili kiungo mmoja mzawa mwenye uwezo mkubwa wa kuchezesha timu, kukaa na mipira na kutuliza mashambulizi wakati tukishambuliwa.


“Yapo baadhi
ya majina yaliyofika katika kamati ya usajili na kati ya hayo, lipo la Sure Boy ambaye tupo katika hatua za mwisho za kufanikisha usajili wake.


“Timu imeonekana kukosa
umakini katika kukaa na mipira pale anapokosekana Aucho, hilo lilionekana katika michezo miwili ya ligi dhidi ya Namungo na Ruvu,” kilisema chanzo hicho.


Alipotafutwa Mjumbe
wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Injinia Hersi Said kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Suala la usajili lipo kwenye benchi la ufundi, sisi kama uongozi kazi yetu ni kufanikisha usajili kwa kutoa pesa pekee, hivyo kama jina lake lipo huko basi tutafanyia kazi.”


Ofisa Habari wa Azam,
Zakaria Thabiti alisema kuwa: “Sisi hatumzuii mchezaji yeyote kusajiliwa na timu nyingine, kikubwa timu husika inahitajika kufuata taratibu za usajili.”

Wilbert Molandi na Musa Mateja


Toa comment