The House of Favourite Newspapers

Sven: Nilikuwa Nawataka Yanga Kombe la FA

0

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, amesema kuwa alikuwa anataka akutane na Yanga, ndiyo sababu ya kuwafunga wapinzani wao, Azam FC, juzi.

 

Simba iliifunga Azam mabao 2-0 na kufanikiwa kufuzu Hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la FA ambapo watakipiga na Yanga, Julai 12, 2020.

Katika mchezo huo wa FA, Simba wataingia uwanjani wakiwa na hasira za kufungwa bao 1-0 na kutoa sare ya mabao 2-2 katika michezo ya Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo msimu huu.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Sven alisema kuwa alihitaji ushindi juzi na ndiyo sababu ya kupanga kikosi imara kitakachompa ushindi katika mechi hiyo iliyokuwa imejaa upinzani mkubwa.

Aliongeza kuwa anafahamu ubora wa Yanga, lakini hiyo haimpi hofu ya kuiogopa zaidi ataingia uwanjani katika mchezo huo kwa lengo la kupata matokeo ya ushindi ya kulipa kisasi na kufuzu hatua ya nusu fainali ya FA kwa kuwafunga watani wao hao.

 

“Simba kukutana na Yanga ni kitu nilichokuwa nakitarajia, hivyo nilitegemea kukutana nao baada ya wao kutangulia kufuzu nusu fainali ya FA, hivyo sina hofu.

 

“Nimefurahia kukutana na Yanga katika dabi ambayo ninatarajia mchezo utakuwa mgumu kwa pande zote mbili, kwetu Simba ni kutaka kulipa kisasi cha kufungwa katika ligi.

 

“Yanga, wao wanataka kutufunga ili watengeneze rekodi ya kutufunga mara mbili katika msimu huu, pia kutaka kufuzu nusu fainali, lakini wakati wapinzani wakizitaka rekodi hizo, naamini mchezo huo unasubiriwa na mashabiki wa timu zote hizi,” alisema Sven.

stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave A Reply