The House of Favourite Newspapers

Tabia Ndogondogo Zinavyoweza Kuvunja Penzi Ndoa!

0

LEO kwenye safu yetu hii tutaangalia tabia ndogondogo ambazo zinafanywa na wanandoa au wapenzi lakini wengi wao hawajui kuwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu uhusiano au kuvunja ndoa.

Kila kukicha napata ujumbe kutoka kwa wanandoa ambao hulalamika kuwa hawawaelewi wenza wao kwani wamebadilika lakini malalamiko mengi yanaelekezwa kwenye tabia hizi ambazo nitakueleza hapa na kama zinakuhusu, kabla ndoa yako haijapinduka unatakiwa kuzifanyia kazi.

Tabia hizo unaweza kuzipitia moja baada ya nyingine, yawezekana ukawa huna zote lakini ukawa na moja au mbili ambazo zinakuhusu. Fuatilia hapa chini;

 

Kukosa muda wa kubadilishana mawazo na mwenza wako

Wanandoa wengi au wapenzi hawana muda wa kupumzika na wapenzi wao na kubadilishana mawazo. Hii ni kutokana na maisha ya sasa yanavyoenda. Tatizo hili au tabia hii inaweza kukusababishia mwenza wako kukukosa na kuona kuwa hana muda na wewe. Kwa maana hiyo inaweza kusababisha yeye kuvunjika moyo na kuizoea tabia ambayo kimahusiano inafifisha mapenzi.

Usishangae, hilo unaweza kuliona dogo lakini linaweza kuvunja ndoa au kuwepo kwa migogoro ya mara kwa mara kwa sababu tu mume au mpenzi hana muda na mkewe.

 

Kusema uongo, kuvunja ahadi

Hakuna anayependa kudanganywa hasa pale ambapo hapastahili lakini pia hakuna ambaye anapenda kuahidiwa kitu kisha asitimiziwe. Baadhi ya tulio kwenye uhusiano tunapenda kudanganya sana, kitu ambacho unaweza kukidharau lakini mwenza wako kikamuumiza sana.

Lakini pia hili la kuahidi halafu unapotezea. Kumbuka uliyenaye ni mtu mzima, ukimwambia nikirudi safari nitakuletea zawadi halafu unarudi mikono mitupu bila kuwa na maelezo lazima mwenza wako atakuona unamchukulia kama mtoto. Vijitabia hivi ni vyema ukaviweka pembeni.

 

Kuonesha kutokumuamini

Kuwa na wasiwasi na mwenza wako kila wakati ni tabia mbaya ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuivunja ndoa, ni sawa tu na kutokumuamini unayeishi naye. Jenga imani hata kama unatilia shaka jambo f’lani, lifanyie kazi kwa makini na usimuoneshe umpendaye kuwa una mashaka naye mara kwa mara.

 

Hulalamiki, kila analokufanyia poa tu

Kama mwenza wako hakulalamikii kwa jambo baya unalomfanyia au unalomnyima ni rahisi kujisikia vibaya. Unapokuwa unajaribu kumwambia mpenzi wako kuhusu jambo ambalo amekuumiza na limekuchanganya ni vema ili uweze kukupa furaha.

Ni vizuri kama atafahamu unahitaji nini na unataka nini lakini usipolalamika atakushangaa kwani moja kwa moja atahisi huna upendo naye. Wanandoa wengi huhisi wanapendwa kama watalalamikiwa jambo, hasa wanandoa wanawake wao wakilalamikiwa na waume zao huamini wanapendwa.

 

Kupuuza tendo la ndoa

Mara nyingi wapendanao penzi hujengwa na tendo la ndoa hasa pande zote zikishiriki ipasavyo. Sasa ikitokea wewe ni mtu ambaye una tabia ya kupenda kupuuza tendo hilo hasa anapokuhitaji mpenzi au mumeo/ mkeo, unamkatisha tamaa mwenza wako. Kumbuka kuwa uhusiano bila ya tendo utaenda pabaya.

Kuwa bize mara kwa mara na mambo yako au maisha yanayokufanya uwe na sababu ya kukosa muda wa kutosha wa kucheza na mwenza wako ni tatizo, kumbuka tendo ni muhimu kuliko chochote.

 

Wakati wote unatanguliza kazi yako

Kuwa na kazi kwa ajili ya kuwaendeleza kimaisha ni muhimu hasa kwa maisha ya sasa lakini linapokuja suala la uhusiano au ndoa ukiendekeza kazi wakati wote unaweza kujikuta ukivunja ndoa au uhusiano kwa jumla.

Kutumia pesa bila hekima

Pesa ni kitu muhimu sana kwa maisha ya binadamu lakini isipotumiwa kwa umakini inaweza kuleta balaa.

Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unakuwa na matumizi mazuri ya pesa hata kama mnazo nyingi.

 

RISASI JUMAMOSI | LOVE STORY

Leave A Reply