The House of Favourite Newspapers

Taharuki! Chanjo Corona Kudaiwa Kuongeza Maumbile ya Kiume

0

WAKATI mataifa yaliyoendelea yakihaha kusambaza kwa wingi chanjo ya maambukizi ya Virusi vya Corona, taharuki imeibuka baada ya taarifa kusambaa kuwa mojawapo ya chanjo hizo zinaongeza maumbile ya kiume.

 

Hatua hiyo imekuja katika kipindi cha wiki tatu zilizopita baada ya chanjo tatu, kuidhinishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani-(FDA) kisha kuanza kusambazwa katika nchi za Amerika pamoja na Ulaya.

 

Hadi sasa virusi hivyo vimeathiri zaidi ya watu milioni 80.2 na kusababisha vifo vya watu milioni 1.7 duniani, ilihali Marekani ikiwa ndio nchi inayoongoza kwa kupigwa na janga hilo duniani baada ya watu milioni 19.2 kuathiriwa kati yao 338,263 wakipoteza maisha.

 

CHANJO ZILIZOPITISHWA

Pfizer / BioNTech; Ni chanjo iliyotengenezwa kwa pamoja kati ya kampuni za Pfizer kutoka Marekani na BioNTech ya Ujerumani. Chanjo hiyo imedhinishwa Disemba mwaka huu na nchi za Marekani, Ujerumani na Uingereza, hata hivyo nchi nyingine nyingi duniani zimeagiza shehena ya chanjo hiyo ambayo imedaiwa kuonesha ufanisi wa asilimia 95 katika kuzuwia maambukizi ya Covid-19.

 

Mordena; Ni chanjo ya pili iliyoidhinishwa huko Marekani kwa matumizi ya kuzuia virusi vya corona. Chanjo hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya Mordena imefungua njia ya kupatikana mamilioni ya dozi kuisaidia nchi hiyo iliyoathiriwa vibaya na janga la COVID-19.

 

Nchi nyingine kama vile Canada tayari zimeagiza shehena ya chanjo hiyo na kuongeza idadi ya chanjo ambazo zimeelezwa kudhibiti virusi vya Corona.

 

Oxford-AstraZeneca; Ni chanjo iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford huko nchini Uingereza. Tayari chanjo hiyo imepitishwa na mamlaka za nchi hiyo na sasa ndio inayoongoza kwa kusambazwa katika miji mbalimbali iliyoathirika nchini humo.

 

Nchi za Afrika ikiwamo Kenya tayari imedhibitisha kuagiza chanjo hizo zaidi ya dozi milioni 24 sambamba pia na chanjo ya Pfizer.

 

CoronaVac; ni chanjo iliyotengenezwa na Brazil kwa kushirikiana na China taifa ambalo mlipuko wa virusi hivyo ulitokea Disemba mwaka jana. Chanjo hiyo inatumika kwa watu wa China pekee.

 

Sinopharm; Hii nayo ni chanjo iliyotengenezwa huo nchini China, licha ya kwamba tayari imekwishaanza kutumika kwa raia wa nchi hiyo, baadhi ya nchi za Uarabuni pamoja na Bahrain zimeagiza shehena ya chanjo hiyo.

 

Sputnik V; Urusi nayo haikubaki nyuma baada ya Agosti mwaka huu kutangaza kuidhinisha chanjo hiyo huku mataifa shindani yakilalamika kuwa chanjo hiyo haijapitia taratibu za chanjo kwa kufanyiwa majaribio mara tatu.

 

Shirika la Afya Duniani nalo limeungana na mataifa mengine zaidi ya 172 katika mpango huo wa kusaka chanjo ya Corona.

Hadi sasa shirika hilo halijaidhinisha chanjo yoyote licha ya kwamba nchi husika tayari zimeanza kutumia chanjo zilizoandaa zenyewe.

 

TAHARUKI YATANDA

Watalaam wa masuala ya afya wanabainisha kuwa suala la upatikanaji wa chanjo, linahusisha gharama kubwa ambazo kila nchi inayohaha kusaka chanjo ya Corona, huwekeza nguvu kubwa kiuchumi na kisiasa ili ipate uungwaji mkono.

 

Wachambuzi hao wanabainisha kuwa nguvu hizo zinaambatana na taarifa za uongo dhidi ya chanjo nyingine kama ilivyoibuliwa wiki iliyopita kuwa chanjo ya Pfizer inaongeza maumbile ya uume.

Taarifa hizo zilichapishwa na mtandao ‘Breakingyourownnews’ baada ya mmoja wa wachangiaji katika mtandao huo kudai kuwa chanjo hiyo imemsababisha mabadiliko hayo katika mwili wake.

 

Hata hivyo, baadhi ya mitandao inayohakiki taarifa mbalimbali imekanusha madai hayo ambayo yaliambatana na kichwa cha habari kuwa ‘Covid vaccine enlarge penis’.

Madai hayo yaliibua taharuki katika mitandao ya kijamii ikiwamo nchi za Afrika ambapo baadhi ya wachangiaji walieleza namna chanjo hiyo itakavyonunuliwa kwa wingi.

 

Kwa kuwa kampuni iliyotengeneza chanjo hiyo ya Pfizer haijatoa tamko lolote, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kiafya wanaona kuwa ni muendelezo wa ‘kuipa kiki’ chanjo hiyo ambayo imeanza kupata uungwaji mkono mkubwa katika nchi zilizoendelea duniani.

 

WACHACHE KUPATA CHANJO?

Licha ya kwamba Tanzania haina mpango wa kuagiza chanjo hiyo, nchi nyingine za Afrika ikiwamo Kenya, zimetangaza kuagiza chanjo mbalimbali za corona.

 

Chanjo hizo zilizotangazwa zimewahiwa na nchi tajiri duniani, jambo ambalo utafiti wa asasi yenye kujikita katika masuala ya afya ya John Hopkins Bloomberg, ukionesha kuwa nchi maskini hususani katika bara la Afrika zitakosa chanjo hizo kwa wakati.

 

Utafiti huo uliotolewa mwezi huu unaonesha kuwa nchi maskini zinaweza kupata dozi za chanjo hizo kuanzia mwaka 2022 .

Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani na wadau wengine walitoa hofu kuhusu taarifa hizo na kutangaza kuwa chanjo zitaanza kusambazwa mapema mwaka 2021.

 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema mwanga umeanza kuonekana na kwamba nchi 190 chini ya mkakati wa pamoja kudhibiti Corona (Covax) uliobuniwa kuhakikisha chanjo za COVID-19 zitanufaika na mgawanyo wa chanjo kwa usawa kote duniani.

 

….inasababisha upungufu wa nguvu za kiume

Wakati taharuki ikiibuka kwamba chanjo ya Pfizer inaongeza maumbile ya kiume, watalaam wamesisitiza kuwa ugonjwa huo wa COVID-19 unasababisha ukosefu wa nguvu za kiume.

Corona imesababisha madhara mengi miongoni mwa walioambukizwa baadhi wakilalamikia kupoteza uwezo wa kunusa au kujua ladha ya chakula.

 

Mtaalam wa masuala ya wanaume, Dk. Peter Mungai Ngungi kutoka nchini Kenya, alieleza kuwa matatizo ya nguvu za kiume hutokea wakati ambapo damu haitembei vizuri mwilini kufuatia kuziba kwa mishipa.

Alisema virusi vya corona hushambulia mishipa inayosambaza damu mwilini iitwazo endothelium inayosambaza damu mwilini na katika uume.

 

Mtaalam huyo aliongeza kuwa kupoteza nguvu za kiume kunatokea sana kwani COVID-19 inaathiri usambazaji wa damu mwilini kupitia mishipa na pia wanaothirika sana ni walio na magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu ambayo pia huchangia katika matatizo ya nguvu za kiume.Vilevile walio na umri wa miaka 50 kuendelea.

Dk. Mungai vilevile alisema mtu akiwa na wasiwasi pia anaweza kuwa na matatizo ya nguvu za kiume, ugonjwa wa COVID-19 ukiwa miongoni mwa magonjwa yanayochangia wasiwasi.

MAKALA; MWANDISHI WETU, UWAZI

 

Leave A Reply