Tambwe: Kwa Falcao, Yanga Imelamba Dume

AMISSI Tambwe, juzi Jumatano alikuwa mbele ya runinga akiangalia mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting na ilivyoisha tu akaliambia Championi Jumamosi kuwa, David Molinga ‘Falcao’ ni bonge la straika na Yanga imelamba dume.

 

Tambwe raia wa Burundi ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga, kwa sasa yupo kwenye maandalizi ya mwisho kujiunga na Klabu ya Fanja ya Oman.

 

Tambwe ameliambia Championi Jumamosi kuwa, Falcao raia wa DR Congo aliyejiunga na Yanga msimu huu, kwenye mechi dhidi ya Ruvu alionyesha uwezo mkubwa na anaweza kuwa mmoja kati ya washambuliaji hatari msimu huu.

 

Tambwe aliendelea kusema kuwa, Falcao anahitaji kupata muda kidogo ili aweze kuwa sawa kwani inaonekana hajacheza kwa muda mrefu.

 

“Jamaa anajua ila sema tu inavyoonekana alikuwa hajacheza soka muda mrefu kama alivyokuwa Heritier Makambo wakati anakuja Yanga, wengi walimuona hafai ila baada ya muda akawa staa.

 

“Kwa namna nilivyomuona anaonekana ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira pia kutengeneza nafasi sasa hivi ni kati ya vitu ambavyo mshambuliaji aliyekamilika anatakiwa kuwanavyo.

 

“Zile pasi alizokuwa akiwatengenezea wenzake kwa kifua na kichwa hazina tofauti kabisa na zile alizokuwa akinitengezea Donald Ngoma wakati tulipokuwa wote Yanga, hivyo kama ningekuwepo basi ningefunga mabao mawili kwa pasi zake,” alisema Tambwe.


Loading...

Toa comment