The House of Favourite Newspapers

Tanasha Kumburuza Mondi Mahakamani

0

PICHA lilelile kwa wanawake tofauti! Kama ilivyokuwa kwa mwanamitindo na msanii wa Bongo Fleva, Hamisa Mobeto ‘Misa’ na mwanamama mwenye pesa zake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss’, sasa ni zamu ya video vixen na msanii wa muziki nchini Kenya, Tanasha Donna.Wanawake wote hao wamezaa na mwanamuziki kinara wa Afro-Pop kutoka nchini Tanzania, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Tanasha aliyezaa mtoto mmoja wa kiume na Diamond au Mondi aitwaye Naseeb Junior, naye yupo mbioni kumburuza mahakamani jamaa huyo kwa kushindwa kutoa matunzo ya mtoto.

 

TANASHA ALALAMIKA

Mapema wiki iliyopita, Tanasha alilalama alipokuwa kwenye ziara ya vyombo vya habari nchini Kenya kuwa, Mondi amemtelekezea mtoto na kwamba anahangaika mwenyewe kumlea mtoto wao huyo, yapata miezi sita tangu walipotengana mapema mwaka huu.Habari zinazosambaa kwa kasi kwenye vyombo hivyo vya habari tangu juzi, ni juu ya Tanasha kunuia kumshtaki jamaa huyo.

 

TANASHA ATAFUTA NJIA

Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, baada ya kulalamika na kuona bado Mondi yupo kimya, ameamua kutafuta njia nyingine ya kufuata mkondo wa kisheria baada ya kukabidhi ishu hiyo kwa wakili wake.Imeelezwa kuwa, wakili wa Tanasha yupo tayari kufungua kesi muda wowote kwenye Mahakama ya Watoto jijini Nairobi, Kenya.

 

KUDAI FIDIA, MATUNZO

Miongoni mwa madai ya Tanasha kupitia wakili wake, ni kudai fidia ya matunzo ya mtoto huyo kwa miezi sita iliyopita, kisha kuomba kulipwa kwa mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto.Katika madai yake ya awali, Tanasha alisema kuwa, Mondi hana lolote na hajawahi kuwa msaada kwa mwanamke aliyezaa naye, ndiyo maana amemtekelezea mtoto wao huyo tangu walipotengana mapema mwaka huu.Tanasha alidai kwamba, Mondi hana huruma na damu yake mwenyewe, ndiyo maana amekuwa akiwatelekezea watoto wanawake aliozaa nao.

 

“Nimekuwa nikilea mwanangu mimi mwenyewe, huo ndiyo ukweli.“Nitakuwa mkweli kwa asilimia mia moja, siwezi kusema kitu ambacho siyo cha kweli.“Ukweli ni kwamba hanisaidii, mimi ninafanya hivyo mwenyewe,” alisema Tanasha ambaye anatamba na Wimbo wa Sawa.

SIYO TUHUMA NGENI KWA MONDI

Tuhuma za Tanasha kwa Mondi, siyo ngeni, kwani mama wa watoto wake wote kuanzia Zari, raia wa Uganda ambaye amezaa naye watoto wawili; Tiffah Dangote na Prince Nillan, naye aliwahi kulalamika kiasi cha kumuita mwanaume suruali.Lakini kwa upande wake Mobeto aliyezaa naye mtoto mmoja wa kiume aitwaye Dyllan, yeye alikwenda mbali zaidi kwa kumburuza Mondi katika Mahakama ya Watoto Kisutu jijini Dar.

Katika kesi hiyo ya Mobeto, Mondi aliamuriwa kulipa shilingi milioni tano kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mwanaye.Hata hivyo, wakati Tanasha akiwa mjamzito, Zari alimtahadharisha kwamba ajiandae kulea mwenyewe au kwenda kudai matunzo mahakamani, jambo ambalo ndilo linalofuata kwa Tanasha.

 

Kwa mujibu wa Tanasha, kilichomfanya aondoke kwa Mondi ni kutokana na mama mzazi wa jamaa huyo, Sandra Kassim ‘Mama Dangote’ kumfanyia mambo ambayo ndivyo sivyo.Tanasha alisema kwamba, alijaribu kuwa mpole akimpa nafasi mama mkwe wake atawale himaya yote na kwamba, hakutaka kufanya lolote litakaloonesha utovu wa nidhamu.

Tanasha alisema Mondi hakuwa anasimama upande wake hata alipobaini kuwa mama yake hakuwa sahihi wakati mwingine.Taarifa ya kuachana kwao iliwashtua mashabiki wao kwani ilikuwa wakati ambapo wimbo wao wa Gere ulikuwa unafanya vizuri, huku ukiwa kama ishara ya mafanikio zaidi ya penzi lao, lakini ghafla mambo.

STORI: SIFAEL PAUL, DAR

Leave A Reply