Na Dr. Chale| GAZETI LA IJUMAA | AFYA
Tatizo la mwanamke kutopata hedhi yake kama kawaida kitaalamu inaitwa Amenorrhea au inatamkwa Amenorea. Tatizo hili ni kubwa na huwasumbua wanawake wengi.
Kufunga kupata hedhi kumegawanyika katika makundi matatu; Kwanza ni hali kitaalamu iitwayo ‘Physiologic Amenorrhea’. Hii inatokea kabla msichana hajavunja ungo au baada ya mwanamke kukoma hedhi, wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha, yaani ni hali ya kawaida, hapa siyo tatizo.
Endapo mwanamke alikuwa anapata siku zake kama kawaida, halafu ghafla zikasimama asipate tena kwa muda wa mwezi au miezi kadhaa na hana mimba basi hali hiyo kitaalamu inaitwa Pathologic, yaani kuna tatizo linahitaji uchunguzi wa kidaktari.
Katika aina hizi mbili za kufunga kupata hedhi pia tunaweza kuzigawa tena katika makundi madogo mawili ambayo ni; ‘Primary Amenorrhea’, hapa msichana ameshakuwa mkubwa, amepita umri wa kuvunja ungo lakini anaweza kuwa na tatizo kubwa katika maumbile yake ya kike au katika mfumo wake wa homoni mwilini.
Pia tuna hali nyingine iitwayo ‘Secondary Amenorrhea’. Hapa mwanamke alishawahi kupata damu ya hedhi miezi iliyopita au hata mwaka lakini hajaona tena, wengine tayari wana historia kuwa walishawahi kuzaa lakini baada ya hapo wakafunga kabisa kupata hedhi. Hili ni tatizo la kiugonjwa linalohitaji uchunguzi wa kina.
Tatizo lingine la kufunga hedhi ambalo ni la tatu katika kundi la matatizo haya tunaita ‘Functional Amenorrhea’. Mwanamke mwenye tatizo hili ana historia ya kuruka miezi ya kupata damu ya hedhi.
Atasema anaweza kupata damu ya hedhi baada ya miezi miwili au mitatu hadi sita, yaani mara miezi mingine apate au miezi mingine asipate. Mwingine aidha hadi atumie dawa ndipo apate hedhi, asipotumia hapati siku zake au mwingine hata asipotumia dawa anaweza apate hedhi au asipate.
CHANZO CHA TATIZO
Hali ya kufunga kupata hedhi iitwayo ‘Pathologic’ kama tulivyokwishaona ambayo pia ina makundi madogo mawili ya ‘Primary’ na ‘Secondary’ ambapo aidha mwanamke tayari ashapata hedhi baadaye zikapotea au ameshafikisha umri mkubwa lakini hajawahi kupata hedhi, linasababishwa na mambo makubwa manne ambapo mwanamke huyu anaweza kuwa na yote au mojawapo.
Kwanza ni kasoro katika viungo vyake vya uzazi kwa kutokuwa na baadhi ya viungo na hivyo kutokuendelea kukua baada ya kufikia umri stahiki wa kuvunja ungo.
Kasoro hizi ni katika mfumo wa uzazi, vifuko vya mayai, uke au kuziba njia ya uke. Chanzo cha pili ni tatizo katika maumbile au mwilini kwa ujumla.
Hapa pia inaweza kuwa kasoro katika viungo husika vya uzazi, kimojakimoja au matatizo katika mfumo wa mwili inayosababishwa na unene au uzito mkubwa, lishe duni na kukonda sana hasa kwa warembo wanaotaka wawe na umbile dogo na jembamba na maradhi mengine kama ugonjwa wa kisukari.
Vilevile maambukizi sugu husababisha tatizo hili la hedhi, mfano ugonjwa wa kaswende, kifua kikuu na HIV.
Chanzo cha tatu ni hali ya kisaikolojia ambayo anaweza akawa nayo mwanamke mwenyewe au inasababishwa na hali ya mazingira anayoishi au kukutana nayo. Matatizo hayo ya kisaikolojia yanaweza kutokana na migogoro mbalimbali ya kiuhusiano, kifamilia na kijamii, mishtuko kutokana na matatizo na kukufanya akili isikae sawa.
Pia kupoteza hamu ya kula kutokana na kuogopa kunenepa au kupata hali fulani unayohisi inaweza kutokana na kula chakula, kwa hiyo unakuwa na woga kula chakula au unachagua aina ya vyakula.
Chanzo cha nne ni matatizo katika mfumo wa homoni au vichocheo vya mwili vinavyoendesha na mfumo wa uzazi.
UCHUNGUZI NA TIBA
Tatizo hili huchunguzwa na kutibiwa katika kliniki za magonjwa ya kinamama kwenye hospitali za mikoa. Vipimo mbalimbali hufanyika kutegemea na historia ya ugonjwa. Vipimo vya damu, X-ray, Ultrasound na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa utashauriwa.
Comments are closed.