The House of Favourite Newspapers

Tatizo La Nguvu Za Kiume Kwa Wanaume Wa Dar Linavyotikisa

0

KELELE zimekuwa nyingi na limetikisa kwenye mitandao ya kijamii na mitaani, ikiwemo kwenye migahawa, vijiweni, saluni na kwingineko kuhusu madai ya kuwa wanaume wa Dar es Salaam wanaongoza kwa kukumbwa na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi na vya haraka haraka (fast food).

 

Tatizo hilo liliwahi kuzua mjadala bungeni hivi karibuni baada ya Mbunge wa Jimbo la Konde, Zanzibar, Khatib Said Haji (picha ndogo juu) kutoa hoja kuhusu tatizo hilo na kumuomba Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tuliani Ackson kutoa japo nafasi kwa wabunge kujadili mjadala huo.

 

Gazeti la Uwazi lilizunguma maeneo mbalimbali ya viunga vya Jiji la Dar es Salaam na kuzungumza baadhi ya wakazi wake wakiwemo wanaume.

WASIKIE WANAUME WA DAR

Kwa upande wa kijana Godfrey wa Tabata Shule, alisema kuwa; “Baadhi ya vyakula vinachangia uwepo wa upungufu wa nguvu za kiume lakini pia msongo wa mawazo (stress) kutokana na maisha Dar na mfumo mzima wa mazingira nao unaweza kuwa tatizo.”

 

EMMANUEL WA SINZA KIJIWENI

“Hivi unadhani baba wa familia ambaye hana kazi, nyumba wanaoishi ni yakupanga, watoto nao zaidi ya watatu hivi unategemea nini kila baada ya muda wanapowaza mwenye nyumba anakuja kudai kodi yake unavyofikiri nguvu za kiume zitatoka wapi hapo?”

 

HAMAD WA MAGOMENI

“Huwezi kupafomu vizuri faragha kama una mastress kibao ya maisha, itaishi mjini lakini bado kijijini nako unategemewa!”

ISSA WA MABATINI

“Tatizo la wanaume wa Dar wanapenda kula vyakula vya fastafasta, vyakula ambavyo havina vitamini zinazotakiwa kujenga mwili. Eti mwanaume mzima anakula chipsi mayai, cha ajabu kuku na mayai vyote ni vya mashine, siyo orijino kama kuku au mayai ya kienyeji.”

JAKSON WA MWENGE

“Upungufu wa nguvu za kiume unachangiwa na kutokula lishe bora vyakula vinavyojenga mwili kama mboga mboga, nyama, mayai, maziwa na vyakula vinavyoongeza nguvu kama ugali wa dona, muhogo na matunda ya aina mbalimbali kama nanasi, tikiti maji, ndizi mbivu, chungwa, matango na mengine watu hawali kwa mpangilio.

SALUM WA MBEZI BEACH

“Uchumi nao unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa sababu unakosa kula chakula unachokihitaji ile diet unakuwa unaisika au kuiona kwenye filamu.

“Mazoezi nayo ni changamoto, kwa sababu ya ubize wa kusaka pesa unakuta mtu anakosa hata muda wa kufanya mazoezi ambayo yanasaidia pia kumuimarisha mtu, hivyo upungufu wa nguvu za kiume lazima utaupata tu.

WIZARA YA AFYA WAO WANASEMAJE?

Akijibu hoja hiyo ya tatizo la nguvu za kiume na uwepo wa matangazo mengi ya kuuzwa kwa dawa ya kuongeza nguvu za kiume, aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Hamis Kigwangalla alisema kuwa, hakuna jibu la moja kwa moja la kuweza kufahamisha umma ukubwa wa tatizo hili kwa sababu tendo la ndoa hufanyika kwa usiri wa wanandoa wenyewe.

“ Tendo la ndoa ni siri kwa hiyo hakuna jibu la moja kwa moja lakini wazee nguvu kupungua ni jambo la kawaida, kwa wanaume kadiri umri unavyozidi kuongezeka uwezo unapungua taratibu lakini pia huchangiwa na ukosefu wa afya njema.

“Tendo la raha linahitaji furaha, chagangamoto wanazozipata wanaume wa kisasa ni ukosefu wa furaha, magonjwa yasiyoyakuambukiza, kutokutulia, stress, uchovu wa kupitiliza huwezi kuwa na furaha na hamasa ya kushiriki tendo hilo ipasavyo. Nashangaa sana kwa wanaume ambao wamekuwa wakihangaika kutafuta dawa za kuongeza nguvu za kiume. Tendo la ndoa linataka afya njema, usitumie madawa kwa muda mrefu ambayo yanaweza kupunguza nguvu za kiume.

“Rai yangu kwa wanaume wote nchini na hata wanawake kushiriki kwa kiasi kikubwa kwenye mambo yanayoendana na kulinda afya zetu, kula vizuri, kupumzika, kufurahi, kucheka na kushirikiana na wenzako ili kuondoa msongo wa mawazo.”

Aidha, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alikazia kuwa dawa zote za asili au tiba mbadala lazima zisajiliwe na mamlaka husika baada ya kuthibitishwa na TFDA, TBS.

Mwalimu aliagiza kuwa mtu yeyote ambaye anauza dawa za tiba asili ambazo hazijasajiliwa watamkamata na kumchukulia sheria.

“Nawaagiza waganga wakuu wote wa mikoa na wilaya kuwachukulia hatua watu wote wanaouza dawa za nguvu za kiume bila kibali maalumu,” alisema.

Leave A Reply