The House of Favourite Newspapers

TATO Yatoa Shilingi Milioni 128 Kusaidia Waathirika Wa Janga La Hanang

0
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Angela Kairuki (katikati) akipokea msaada wenye thamani ya Tsh milioni 128 kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii nchini (TATO), Wilbard Chambulo (wa pili kulia) ili kusaidia waathirika wa janga la Hanang. Wengine kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Silayo Dos Santos, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dk.Jim Yonazi na Mtendaji Mkuu wa TATO, Sirili Akko.

CHAMA cha Mawakala wa Utalii nchini (TATO) kupitia wanachama wake kimetoa misaada yenye thamani ya dola za Marekani 51,200 ( takribani 128,000,000/-) kwa ajili ya kusaidia manusura wa janga la maporomoko ya udongo yaliyotokea katika eneo la Katesh katika wilaya ya Hanang, mkoani Manyara na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 80, majeruhi wengi na maelfu ya watu kukosa makazi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TATO fedha hizo zilikuwa zitumike katika maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo na kwamba sasa zimeelekezwa katika kuwasaidia waathirika wa Hanang.

“Tumeguswa na hali mbaya ya waathirika wa huko Hanang, ambapo wanachama wote kwa pamoja na kwa kauli moja tumeamua  kusitisha maadhimisho ya miaka 40 ya TATO ambayo yalipangwa kufanyika Desemba 9, 2023 ili tuwasaide ndugu zetu walioathirika huko Katesh”, alisema Mwenyekiti wa TATO, Wilbard Chambulo alipokuwa akikabidhi misaada hiyo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki.

Msaada huo ulijumuisha lita 37,800 za maji, lita 2,000 za mafuta ya kupikia, tani 10 za unga wa ngano na mabati 4,000, vyote vikiwa na thamani ya dola za Marekani 51,200 (sawa na takribani 128,000,000/-) ikiwa ni katika juhudi za TATO za kuwapa nafuu na faraja manusura hao.

“Mioyo yetu iko pamoja na wale wote waliopoteza wapendwa wao na pia tunaungana na ndugu na jamaa za wale walioathirika na janga hili kubwa”, alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema michango hiyo imelenga kutoa misaada ya haraka kwa wale wenye uhitaji mkubwa na wa haraka ili kujijenga upya baada ya kuathirika vibaya na janga hilo.

“TATO inatambua uhitaji na haraka ya uhitaji wa wale wote walioathirika, tunaahidi kuwa nao wakati wote katika mchakato unaolenga kurudisha maisha yao ya awali”, alisema.

Bw. Chambulo alieleza kuwa msaada huo utashughulikia mahitaji ya haraka ya lishe, usafi na mavazi kwa familia zilizoathirika.

Akipokea misaada hoiyo, Waziri Kairuki aliipongeza TATO kwa kuunga mkono juhudi za serikali zinazolenga kurejesha matumaini kwa waathirika wa janga hilo.

“Ninawashukuru sana wanachama wa TATO kwa moyo wenu wa ukarimu, nitoe wito kwa mashirika mengine kuungana na TATO katika kuunganisha nguvu na pia kushirikiana serikali ili kuwasaidia walionusurika katika janga hilo” Bi. Kairuki alisema.

TATO ni shirika linalolenga kutangaza, kukuza na kuimarisha sekta ya utalii nchini Tanzania ambacho kinajumuisha mawakala wa utalii hapa nchini ambapo majukumu yake ni pamoja kuhakikisha kuwa sekta ya utalii inakuwa endelevu na inayowajibika katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

Leave A Reply