The House of Favourite Newspapers

Tausi; Wapuuze Wanaokubeza

0

MWISHONI mwa wiki iliyopita habari kubwa iliyotawala kwenye mitandao ya kijamii na mitaani ni kuhusu kujifungua kwa staa wa filamu za Kibongo; Tausi Mdegela.

Tausi ni mwigizaji na ni miongoni mwa wachekeshaji matata wa kike, mwenye umbo dogo ambaye alijaaliwa mtoto wa kike.

 

Hongera Tausi kwa kuitwa mama kwani siyo kazi rahisi. Kuna gharama kubwa mno. Kupata mtoto si jambo jepesi. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa sababu wapo wanawake wengi wanaotafuta watoto usiku na mchana, lakini hawapati, wamebaki wakimlilia Mungu na kutafuta kila kukicha bila mafanikio.

 

Mara baada tu ya Tausi kujifungua, gumzo la aina yake lilizuka kwa baadhi ya watu kushangaa na kumbeza kwamba imekuwajekuwaje kupata mtoto kutokana na maumbile yake yalivyo madogo.

 

Jamani walimwengu sijui wamekuwaje! Watu wengi wamekuwa wakiwakosoa wenzao kutokana na maumbile, sura na mengine mengi. Tabia hii kiukweli inakera mno.

Mungu amemjaalia Tausi mtoto, amempa furaha ya maisha yake, lakini kuna baadhi ya binadamu wanamkosoa hadi Muumba na kumbeza kwa jinsi alivyoumbwa.

 

Hivi wewe unayefanya hivyo, unaweza kujiumba mwenyewe au hivyo ulivyo mzima, huna kasoro yoyote, ulijiumba mwenyewe?

Siyo vyema kumbeza Tausi au wengine wenye kasoro mbal-imbali za kimaumbile kwa kuwa hawakujitakia, bali wamejikuta wam-ezaliwa hivyo na hawawezi kujite-ngeneza mnavyotaka ninyi.

 

Tausi ni mwanamke mwenye haki ya kuwa na mpenzi au mume, kupata watoto na haki nyingine zote za kibinadamu kwani hata aweje, bado ni BINADAMU!

Kwa hiyo sioni maana kwa baadhi ya watu kumbeza na kumsimanga mwanaume aliyejaaliwa naye mtoto huyo kuwa, eti hana huruma!

 

Mbona wewe una mume au mpenzi na mtoto au watoto, lakini watu wanakuona ni binadamu kama wao? Kwa nini kwa Tausi inaonekana ni nongwa au ni jambo la ajabu?

Hakuna lolote la ajabu kwa Tausi kupata mtoto kwa sababu ni haki yake kama mwanamke.

 

Ni upuuzi katika dunia ya sasa kumbagua mtu kutokana na umbile au mwonekano wake. Zaidi sana inashangaza kuona kuwa wanaokosoa zaidi ni wasichana wadogo wasiojua kama nao Mungu atawabariki kupata mtoto au wanawake ambao hata hawajazaa yaani hawajui uchungu wa mtoto ni nini.

Niwaulize tu, hivi mnajua kama mkija kuzaa mtazaa watoto wa aina gani?

 

Mkija kuzaa watoto wenye ulemavu au kasoro yoyote mtamlaumu nani wakati mnajitakia wenyewe kwa kuwabeza wenzenu walioumbwa na Mungu? Huko siyo kujitafutia laana?

Kwa mliombeza Tausi mnapaswa kutubu na kumuomba Mungu wenu awasamehe.

 

Baada ya kutubu na kuomba Mungu awasamehe, kinachofuata ni kubadilika na kuachana na tabia za kuwatoa kasoro wenzenu kwa kuwa aliyewaumba ninyi ndiye aliyewaumba wao. Kama vile huwezi kujibadilisha yaani ukiwa mfupi ukajibadili na kuwa mrefu, basi na wao hawawezi kujibadilisha vile walivyo.

 

Tausi anastahili kupongezwa kwa hatua hiyo ya kuwa mama kwani amethubutu na ameweza, tofauti na baadhi ya mastaa wengine wa kike wanaoendekeza starehe na pale wanapopata ujauzito wanachoropoa kwa kile wanachodai kuwa wakizaa watazeeka na kupoteza mvuto.

 

Nikutie moyo Tausi kwamba wewe ni shujaa, usiwasikilize wale wanaokubeza, ziba masikio, endelea kusonga mbele katika kumlea mwanao huyo.

 

Kubwa zaidi, mshukuru Mungu wako kwa kuwa uko salama na mwanao yupo salama kwani wengine hupoteza maisha wakati wa kujifungua, lakini wewe umetoka salama, hivyo ni maombi yangu kwa Mungu akutunze wewe na mwanao, akue akimpendeza yeye na wanadamu!

MAKALA: GLADNESS MALLYA

Leave A Reply