The House of Favourite Newspapers

TFF Kuivunja Kamati ya Saa 72

0

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa litaivunja Kamati ya Saa 72 ya shirikisho hilo kama watabaini kuna uzembe unaofanyika katika kutoa maamuzi.

 

Kamati ya Saa 72, ikijulikana pia kama Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, ni chombo maalumu kilichopo chini ya TFF na Bodi ya Ligi ambacho hushughulikia masuala mbalimbali ambayo yanahusu ukiukwaji wa kanuni na sheria ambazo zinaendesha ligi zote nchini, ikiwemo ishu za wachezaji, viongozi wa timu na marefa wa ngazi zote.

 

Uamuzi huo unakuja mara baada ya kuibuka malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali wakidai chombo hicho kinachelewa kutoa maamuzi ya matukio mbalimbali yaliyotokea michezoni, huku baadhi ya matukio hayo yakishindwa kutolewa ufafanuzi licha ya kuonekana kuwa kuna makosa ya wazi yamefanyika.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau, alisema kuwa wapo katika mpango wa kuichunguza Kamati ya Saa 72, ili kujua kama kuna watu hawafanyi kazi ipasavyo na kuzua malalamiko, ambapo aliongeza kuwa endapo watabaini upungufu wowote basi wataivunja kamati hiyo na kuijenga upya ili kuepusha malalamiko ambayo siyo ya lazima.

 

“Tunaandaa utaratibu wa kuichunguza Kamati ya Saa 72 ya Bodi ya Ligi na TFF, hii inatokana na malalamiko yaliyojitokeza hivi karibuni juu ya kuwepo kwa ucheleweshaji wa kutoa ufafanuzi juu ya matukio fulani.

 

“Kwa kawaida kamati hiyo hukutana kila Jumatatu ya kila wiki, hivyo tunataka tuijenge upya ili iwe inakutana kila siku baada ya mechi kuchezwa ili kuchunguza kama kuna lolote limetokea na kisha kutolea ufafanuzi na ikibidi adhabu kama kutakuwa na tukio la namna hiyo,” alisema Kidau.

ISSA LIPONDA, Dar es Salaam

Leave A Reply