The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-33

0

ILIPOISHIA WIKIENDA
Siku ile sikutoka tena nyumbani. Ilipofika usiku mke wangu alimpigia mama yake aliyekuwa akiishi Kinondoni. Akazungumza naye na kukubaliana kuwa mama huyo angekuja kukaa kwetu wakati Suzana akijifungua. SASA ENDELEA…

Katika juma lile nikafanya jambo moja zuri. Nilinunua nyumba moja iliyokuwa inauzwa eneo la Mwananyamala.

Ilikuwa nyumba ya zamani. Baada ya kuinunua niliifanyia ukarabati ionekane ya kisasa.
Baada ya hapo nikaiacha. Sikutaka kuingiza mpangaji ingawa watu wengi walikuwa wakiiulizia.

Niliiweka mlinzi ambaye alikuwa akiiangalia saa ishirini na nne.
Ujauzito wa mke wangu ulipofikia miezi tisa alimuita mama yake ili akae naye kwani alishuku kuwa wakati wowote angeweza kuumwa uchungu.
Siku hiyo nilikuwa ofisini kwangu, mama mkwe akanipigia simu na kunijulisha kuwa mke wangu ameanza kuumwa.

“Sasa mnataka kwenda hospitali?” nikamuuliza.
“Nimempigia dereva anakuja kutuchukua.”
“Na mimi nakuja hukohuko.”
Kwa kihoro nilichokuwa nacho niliacha kazi niliyokuwa naifanya nikatoka ofisini. Dereva akanirudisha nyumbani.

Nilimkuta mke wangu yuko kwenye kibaraza cha nje ya nyumba yetu akigaragara.
Nikapatwa na kiwewe kidogo.
“Unajisikiaje?” nikamuuliza mbele ya mama mkwe.

Mke wangu hakunijibu kitu. Alikuwa amekishika kiuno chake akiugua. Pengine hakunijibu kwa kuona nilimuuliza swali la kipumbavu kwani nilishaambiwa kuwa anaumwa uchungu.

Nilipoona sikujibiwa nikamtazama mama mkwe.
“Dereva hajafika?” nikamuuliza.
“Ndiyo tunamsubiri”
“Mmechukua kila kitu?”
“Vitu vyote vimo ndani ya mfuko.”
Hapo hapo dereva akatokea.

“Hebu harakisha uwawahishe hospitali,” nikamwambia huku nikiinama ili nimuinue mke wangu.

Nilichofanya hakikuwa wema, mkono wangu ulisukumwa, mke wangu akainuka mwenyewe na kwenda kujiingiza kwenye gari.
“Haya mama nenda kajipakie na wewe mwende,” nikamwambia mama mkwe.
Wakati mama mkwe anakwenda kujipakia nikakumbuka kitu.
“Sijui mmechukua pesa za kutosha?” nikamuuliza. Niliogopa kumuuliza mke wangu kutokana na hali aliyokuwa nayo.

“Amechukua,” mama mkwe akanijibu.
“Haya nendeni…dereva endesha taratibu si unajua…”
Nikamgeukia tena mama mkwe ambaye alikuwa ameshajipakia kwenye gari:
“Basi mtanijulisha kila kitakachotokea, mtanipigia simu.”
“Haya baba, tutakujulisha,” mama mkwe akaniambia.

Gari likaondoka. Nikasimama na kulitazama kwa nyuma huku nikisali kumuombea mke wangu azae salama.

Hawakuwa wakienda Muhimbili wala hospitali yoyote ya serikali, walielekea Mikocheni katika hospitali binafsi ambako mke wangu alikuwa akienda katika kipindi chote cha ujauzito wake.

Baada ya gari hilo kuondoka niliingia ndani. Nilipoona sikuwa na chochote cha kufanya nikatoka. Dereva wangu akanirudisha ofisini.
Kusema kweli sikujua ilikuwa ni kwa sababu ya ulimbukeni au nini, sikuweza tena kuendelea kufanya kazi. Mawazo yangu yalikuwa kwa mke wangu.
Mawazo tele yalinijia kichwani. Kubwa nililokuwa nikiliwaza ni juu ya mtoto atakayezaliwa. Nilikuwa nikijiuliza mke wangu atanizalia mtoto wa kiume au wa kike kama aliyekuwa akimtaka yeye?

Muda ukazidi kupita, sikupigiwa simu kujulishwa chochote, nikaanza kupata wasiwasi. Nikajiuliza sijui nimpigie mama mkwe nimuulize au niache.”
Nikaamua nimpigie. Nikampigia lakini simu yangu haikupokelewa jambo ambalo liliniongezea wasiwasi zaidi.

Nikasubiri kwa robo saa hivi kuona kama ningepigiwa, nikaona kimya. Nikapiga tena.
Safari hii simu yangu ikapokelewa na mama mkwe.
“Habari ya huko?” nikamuuliza mama mkwe.

“Huku ni salama. Mke wako ameshajifungua.”
Nikashtuka.
“Amejifungua mtoto gani?” Ndilo swali la kwanza nililomuuliza.
“Amejifungua mtoto mwanaume.”

Ilibaki kidogo tu nipige kelele za furaha kwa jinsi moyo wangu ulivyopata faraja kwa kusikia habari ile.
“Amejifungua salama?”

“Amejifungua salama.”
“Ni sasa hivi au ni muda uleule mliofika?”
“Tulipofika hakukaa sana akaingizwa kizimbani.”
“Kuna kipindi nilipiga simu lakini haikupokelewa.”
“Nilikuwa nikishughulika na yeye.”
“Sawa, basi nitakuja kuwaona.”

Leave A Reply