The House of Favourite Newspapers

The Beginning of my End (Mwanzo wa Mwisho wangu-09)

0

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba au maarufu zaidi kama Ben, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.
Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chake kufanya mauaji hayo na kilichokuwa kikisubiriwa ilikuwa ni hukumu tu.
Wakati kila mtu akiamini kwamba Ben ameua, Jordan Rwechungura, wakili aliyekuwa akimtetea katika kesi hiyo ambaye ukiachilia mbali kazi yake pia alikuwa rafiki mkubwa wa Ben, waliyecheza pamoja tangu wakiwa watoto wadogo, anakuwa mgumu kuamini kwamba ni kweli rafiki yake huyo ameua.

Historia ya makuzi ya Ben, inamfanya Jordan ahisi kwamba Ben hajaua ila ameamua kukubali kwa sababu ambazo yeye mwenyewe ndiye anayezijua. Jitihada zake za kutaka kuufahamu ukweli ili amnasue rafiki yake huyo kutoka kwenye kitanzi kilichokuwa kinamsubiri, zinagonga mwamba kutokana na Ben kukataa kutoa ushirikiano, muda wote aking’ang’ania kwamba ni yeye ndiye aliyeua.

Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anaingizwa mahakamani huku mamia ya watu, wakiwemo waandishi wengi wa habari wakifuatilia kwa umakini kesi hiyo iliyogusa hisia za watu wengi.
Upande wa pili, historia ya maisha ya Ben inaelezwa, tangu akiwa kijana mdogo kabisa, akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake, Mtaa wa Maporomoko kwenye mji mdogo wa Tunduma. Anahitimu kidato cha sita na kuanza kufanya kazi ya kufundisha kwa kujitolea na twisheni.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Fedha alizokuwa anapata, kwa kiasi kikubwa zilimsaidia sana yeye na familia yake, wakawa hawahangaiki tena kuhusu mahitaji madogomadogo ya familia, ikiwemo chakula.
Siku zilizidi kusonga mbele na hatimaye matokeo ya kidato cha sita yalitangazwa nchi nzima ambapo kama ilivyotegemewa na wengi, shule iliyoongoza kwa ufaulu, ilikuwa ni Mzumbe iliyochuana vikali na shule nyingine za seminari.

Benjamin Semzaba, kwa mara nyingine akitangazwa kuwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora nchi nzima na kubwa zaidi, katika orodha hiyo ya wanafunzi kumi bora, yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza.
“Ben amekuwa TO (Tanzania One), ni heshima kubwa kwa shule yetu na kila mtu anayesoma hapa, tunafikiria kuandaa sherehe maalum ya kumpongeza, kwa sasa kila mmoja aendelee kufurahia ushindi mkubwa uliopatikana,” Mkuu wa Shule ya Sekondari Mzumbe, Aloyce Chilongani aliwatangazia wanafunzi wa shule hiyo, muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo.

Kwa waliokuwa wanamfahamu Ben na jinsi alivyokuwa anajituma katika masomo, hilo halikuwa jambo la ajabu kwao kwani walishamtabiria kung’ara kwa kiwango cha juu kabisa. Shamrashamra zikaendelea shuleni hapo.
Ben akiwa darasani katika shule aliyosoma, Tunduma, akifundisha kwa kujitolea somo la Bailojia kidato cha nne, alishtushwa na ujio wa ghafla wa mkuu wa shule hiyo, mwalimu Tungo’mbe ambaye aliingilia kipindi chake na kuwatangazia wanafunzi kwamba alikuwa akimhitaji mwalimu wao mara moja, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.

Ilibidi Ben akatishe kipindi, akatoka na kumfuata mwalimu huyo ambaye aliendelea kuchekacheka kwa furaha huku akilitaja jina lake, akaenda naye moja kwa moja mpaka ofisini kwake ambapo Ben alipoingia, alipigwa na mshangao baada ya kukuta walimu karibu wote wakiwa ndani ya ofisi hiyo.
Alipoingia tu, walianza kuimba wimbo wa kumpongeza huku wengine wakitingisha shampeni, akazidi kupigwa na butwaa, mwalimu Tung’ombe alichukua ‘laptop’ yake iliyokuwa imeunganishwa na mtandao wa ‘internet’, akamgeuzia  Ben na kumuonesha tovuti ya Baraza la Mitihani aliyokuwa ameifungua, akatulia na kuanza kusoma huku walimu wengine wakiendelea kuimba nyimbo za kumpongeza.

“Ooh! Ahsante Mungu, siamini macho yangu,” alisema Ben huku akipiga magoti na kuinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake, machozi ya furaha yakimtoka kwa wingi. Mwenyewe alijua kwamba atafaulu lakini hakuhisi kama anaweza kuwa mwanafunzi wa kwanza kitaifa, akaendelea kutokwa na machozi mengi ya furaha.
Baadaye wanafunzi wote wa shule hiyo nao walitangaziwa kuhusu mafanikio aliyoyapata Ben ambaye chimbuko lake lilikuwa ni kwenye shule hiyo, nao wakafurahi sana kwani shule yao ilipata heshima kwa mara nyingine, siku hiyo ikapita kila mmoja akiwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake.

Hali ilikuwa hivyohivyo kwa familia ya kijana huyo ambapo licha ya umaskini wao, walifurahishwa mno na mafanikio aliyokuwa akiendelea kupata Ben. Hata ile huzuni ya kuondokewa na mmoja wa wanafamilia kwa sababu ambazo zingeweza kuzuilika, ilifutika kabisa na sasa kila mmoja akawa na mategemeo makubwa kwamba miaka michache baadaye, wataishi maisha bora na ya kifahari kutokana na juhudi za Ben.

Kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata, Ben na wanafunzi wenzake walioingia kumi bora kwenye mtihani wa taifa, walipewa wito maalum wa kwenda mpaka mjini Dodoma, kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuonana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Waziri Mkuu, mawaziri wengine pamoja na wabunge katika tafrija maalum ya kuwapongeza.

Siku chache baadaye, Ben akasafiri huku akilipiwa kila kitu na serikali, mpaka mjini Dodoma alikoenda kukutana na wanafunzi wenzake na kupata nafasi ya kuonana na viongozi wa ngazi za juu serikalini, jambo ambalo lilimfurahisha sana moyoni mwake. Katika hafla ya kupongezwa, Ben alikabidhiwa hundi ya shilingi milioni tatu pamoja na cheti, jambo lililozidisha furaha ndani ya moyo wake.

Siku tatu baadaye, walitawanyika na kurudi makwao, wakiwa wameshajifunza mambo mengi kuhusu bunge lilivyokuwa linaendesha shughuli zake. Alipofika nyumbani kwao, aliwasimulia kila kitu kilichotokea kwenye safari yake, familia yake ikazidi kufurahi na kumshukuru Mungu.

Miezi michache baadaye, Ben alikamilisha mipango yote ya kujiunga na chuo kikuu. Kwa kuwa kiwango chake cha ufaulu kilikuwa kikubwa kuliko mwanafunzi yeyote, alipata mkopo kutoka serikalini kwa asilimia mia moja. Akafunga safari kuelekea jijini Dar es Salaam kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mlimani).
Huku nyuma, familia yake aliiacha ikiwa na ahueni kubwa kwani fedha alizokuwa akizipata baada ya kulipwa na uongozi wa shule alikokuwa anajitolea kufundisha pamoja na zile alizokuwa anakuzisanya kwenye masomo ya ziada (tuition), alikuwa akitumia na kiasi na kuweka akiba nyingine.
Ni akiba hiyo pamoja na zile alizopewa kama zawadi bungeni mjini Dodoma ndiyo alizozitumia kuiachia familia yake kwa ajili ya matumizi katika kipindi ambacho yeye atakuwa chuoni.

***
Septemba 28, 2009
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mlimani),
Dar es Salaam.
Wanachuo wapya wa mwaka wa kwanza, waliendelea kuripoti kwa wingi kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kuanza rasmi kwa muhula mpya wa masomo.
Vijana kutoka sehemu mbalimbali za nchi, wenye historia tofautitofauti, wengine kutoka familia za kifukara na wengine kutoka familia za kitajiri, wote walichanganyikana pamoja.
“Kaka mambo?”
“Salama dada,” alijibu Ben kwa kifupi kwani hakuwa na ujasiri wa kukabiliana na wasichana, hasa wa rika kama lake, tena warembo kama alivyokuwa huyo aliyekuwa akimsemesha.
“Mh! Samahani, sijui nimekufananisha? Wewe ndiyo Benjamin Semzaba yule Tanzania One?” alihoji msichana huyo akimaanisha mwanafunzi bora wa Tanzania.
“Yaah! Umenijuaje? Sikumbuki kama tumewahi kukutana.”
“Nilikuona kwenye vyombo vya habari siku ile mkiwa Dodoma kwenye tafrija ya kupongezwa na wabunge na mawaziri,” alisema msichana huyo, Ben akamkubalia kwani ni kweli siku hiyo kulikuwa pia na waandishi wengi wa habari.
“Ooh! Hongera sana jamani,” alisema msichana huyo na kumkumbatia Ben bila kujali kwamba walikuwa kwenye kantini ya chuo, mahali ambapo palikuwa na mkusanyiko wa wanachuo wengi. Ben akabaki amepigwa na butwaa kwani ukiachilia mbali mambo mengine, hakuwahi kukumbatiwa na msichana hata mara moja katika maisha yake, mapigo ya moyo wake yakawa yanamuenda mbio kuliko kawaida.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply