The House of Favourite Newspapers

The World You Left Behind 23

0

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, unasababisha waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa kuwa mkali kama pilipili na anaahidi kuwachukulia hatua kali wote waliotajwa kwenye ripoti ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali.

Hata hivyo, kazi haiwi nyepesi kwake, muda mfupi baada ya kuvujishiwa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za serikali na rafiki yake kipenzi, CAG Mwampashi, tukio baya linamtokea rafiki yake huyo zikiwa ni saa chache kabla ya kusoma ripoti hiyo hadharani.

CAG Mwampashi anauawa kikatili akiwa nyumbani kwake na ofisi yake inateketezwa na kubaki kuwa majivu. Kama hiyo haitoshi, Magesa ananusurika kwenye majaribio kadhaa ya kutaka kuukatisha uhai wake, hali inayolazimu awe anatembea na walinzi kila anakokwenda.

Upande wa pili, ndoa ya waziri huyo inakumbwa na migogoro ya hapa na pale. Baadaye Magesa anapenyezewa taarifa za kushtua mno juu ya mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake. Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kuinusuru nafsi yake.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Kama alivyoambiwa na Grace, muda mfupi tu baada ya kuwasili nyumbani kwake, alianza kupokea wageni.

Wa kwanza alikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Manuel Kwame ambaye licha ya ukweli kwamba asubuhi ya siku hiyo walikuwa pamoja ofisini, alidai amekuja kumtembelea yeye na familia yake.

“Karibu sana, vipi familia haijambo?” alihoji Magesa huku akijitahidi kuisoma saikolojia ya katibu mkuu wake, kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa chake, akajua huyo naye ni miongoni mwa wabaya wake japokuwa hakuwa na ushahidi wa moja kwa moja.

Walizungumza mambo mbalimbali yahusuyo maisha na kazi na baada ya Kwame kuondoka tu, simu ya mezani ya Magesa ilianza kuita, akaenda kuipokea.

“Haloo! Tumepokea ujumbe kwamba mkutano wa bodi ya wakurugenzi wa benki kuu umeahirishwa mpaka siku tatu baadaye,” ilisikika sauti ya mratibu wa mkutano huo, Magesa akashusha pumzi ndefu mithili ya mtu aliyetua mzigo mzito aliokuwa amejitwisha kichwani.

Muda mfupi baadaye, mkewe aliyekuwa akiandaa chakula cha jioni, alikuja na kukaa pembeni ya mume wake.
“Vipi habari za kazi?”

“Nzuri mke wangu,” alisema Magesa, mkewe akamwambia kwamba jioni hiyo alikuwa na mazungumzo nyeti naye.

“Hakuna tatizo mke wangu, ukiwa tayari niambie,” alijibu Magesa kwa sauti ya upole, mkewe akaondoka na kwenda kuendelea kuandaa chakula cha jioni. Japokuwa Magesa alikuwa akiilazimisha furaha kwenye uso wake, bado hofu kubwa ya kufa ilikuwa ikijionesha waziwazi usoni kwake.

Taarifa alizozipata muda mfupi uliopita kwamba mkutano wa bodi ya wakurugenzi uliokuwa ufanyike siku inayofuatia, Posta jijini Dar es Salaam ilizidi kumchanganya.

Ikabidi aende chumbani kwake kwa lengo la kutaka kuzungumza na Grace na kumueleza kilichotokea.

Akapiga namba mpya ya simu ya Grace aliyompa na muda mfupi baadaye, mwanamke huyo alipokea simu, akawa anazungumza kwa sauti ya utulivu kabisa. Magesa alipomueleza kuhusu kuahirishwa kwa mkutano huo, kwanza alicheka kisha akamjibu:

“Kilichowakwamisha ni kwamba mpango wa kukuua bado haujakamilika. Nimepata taarifa za siri kutoka kwenye kikao cha dharura walichokuwa wamekaa muda si mrefu uliopita, wameshindwa kuafikiana juu ya aina ya kifo unachotakiwa kufa.

“Wanataka kusibaki alama au dalili zozote zinazoweza kuwatia watu wasiwasi, pole sana Magesa ila kila kitu kitakuwa sawa,” alisema mwanamke huyo, Magesa akawa anatetemeka kuliko kawaida.

Kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo alivyokuwa anazidi kuyahofia maisha yake. Japokuwa mwanamke huyo alikuwa akimtuliza mara kwa mara na kumtaka asihofu, bado hakuwa na imani kama kweli anaweza kumsaidia kukikwepa kifo hicho.

“Kwa hiyo nifanyeje?”
“Inabidi uendelee kuwa mtulivu, usiache kwenda kazini hata siku moja ila epuka mizunguko isiyo ya lazima. Ukitoka kwako nenda ofisini na ukitoka rudi moja kwa moja nyumbani. Usikubali ‘appointment’ yoyote nje ya ofisini kwako au nje ya nyumbani kwako.

Hata hao walinzi wako unapaswa kuwa nao makini, usimuamini mtu yeyote.”

“Ahsante, kwa hiyo ile mipango mingine tuliyozungumza nifanyeje?”
“Endelea na mipango kama kawaida, na mimi naendelea na mipango yangu, hakikisha hakuna mtu yeyote anayefahamu kinachoendelea,” alisema Grace kisha simu ikakatwa.

“Ulikuwa unaongea na nani mume wangu?” sauti ya mkewe ndiyo iliyomzindua kutoka kwenye lindi la mawazo, akajiweka vizuri pale kitandani alipokuwa amekaa na kushusha pumzi ndefu, mkewe akamsogelea na kukaa pembeni yake.

“Nilikuwa nazungumza mambo ya kikazi mke wangu. Vipi chakula tayari?”
“Tayari lakini naomba kuzungumza na wewe kama nilivyokwambia,” alisema Vivian, mke wa Magesa na kujiweka vizuri pale kitandani. Akaanza kueleza dukuduku kubwa lililokuwa ndani ya moyo wake. Alimueleza mumewe jinsi anavyoshindwa kumuamini kutokana na nyendo zake na usiri uliotawala kwenye maisha yake.

Kadiri alivyokuwa anazidi kuzungumza ndivyo hasira zilivyokuwa zinazidi kumpanda kwa kuhisi kwamba mumewe anamzunguka.

icha ya kujaribu kujitetea kadiri ya uwezo wake wote, bado Vivian hakumuelewa kabisa mumewe.

Mazungumzo ambayo yalianza kama majadiliano ya kawaida kati ya mume na mke, yalibadilika na kuwa malumbano makali, ikafika mahali kila mmoja akawa ameshapandwa na jazba.

Vivian alikuwa akilalamika kwamba ameambiwa kwamba mumewe anamsaliti, maelezo ambayo tayari Magesa alishaambiwa na Grace kwamba awe makini kwani kuna mpango umeandaliwa wa kuivuruga ndoa yake.

Alipojaribu kumbana mkewe amueleze ni nani aliyempa taarifa hizo, alikataa katakata, malumbano yakaendelea kwa muda mrefu.
Magesa alipoona mkewe anamkosea adabu, alipandwa na hasira na kumkunja mkewe.

“Unataka kunipiga tena kama siku ile? Wewe si ndiyo kawaida yako, ukiona nimekushtukia usaliti wako unakimbilia kunipiga, safari hii sitakubali,” alisema mwanamke huyo, Magesa akajikuta akiishiwa nguvu, akamuachia mkewe na kuendelea kumsihi atulie lakini ilikuwa sawa na kazi bure.

Mkewe alikuwa mkali mno, alibadilika na kuwa mtu tofauti kabisa. Hakuwa Vivian yule aliyemuoa miaka kadhaa iliyopita, mwanamke mpole, msikivu na mwenye adabu kwa mumewe. Ilionesha kuwa lazima kuna kitu kinampa jeuri, vilevile kama Grace alivyomueleza Magesa.

Usiku huohuo, Vivian aliondoka kwa jeuri nyumbani hapo bila hata kumuaga mumewe. Awali Magesa alidhani ni hasira za kawaida tu lakini mkewe atarudi lakini haikuwa hivyo, mpaka inafika saa sita za usiku, Vivian hakuwa amerejea nyumbani na hakukuwa na dalili za kurejea, Magesa akazidi kuchanganyikiwa.

Mpaka kesho yake asubuhi, Vivian hakuwa amerejea nyumbani na kile mumewe alipokuwa akimpigia simu yake, alikuwa hapokei na wakati mwingine alikuwa akiikata na kuzima simu kabisa, jambo lililomsononesha mno Magesa.

Hata hivyo, hakuwa na cha kufanya zaidi ya kuendelea kuwa mtulivu. Siku hiyo pia ilipita bila kuwa na taarifa zozote juu ya mahali alipo mkewe, siku nyingine nayo ikapita na hatimaye siku ya tukio ikawadia.

Kama alivyokuwa ameelekezwa na Grace, Magesa alilazimika kutoa fedha nyingi kuwahonga wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Planet Link, akafanikiwa kupewa mwili wa mwanaume mmoja uliokuwa umekaa kwa zaidi ya wiki mbili mochwari bila ndugu zake kwenda kuuchukua.

Je, nini kitafuatia? Usikose IJumaa kwenye Gazeti la Uwazi Mizengwe ya Uchaguzi.

Leave A Reply