The House of Favourite Newspapers

TIZEBA AIPINGA TAARIFA YA POLISI KUHUSU AJALI YA WATUMISHI 5 SINGIDA

Waziri wa Kilimo na Chakula, Eng. Dkt. Charles Tizeba (Mb) akiwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dkt. Charles Mwijage wakati wa kuaga miili ya watumishi watano wa Wizara ya Kilimo waliofariki kwa ajali ya gari juzi tarehe 21 Octoba 2018 katika Kijiji cha Njiri Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida.

 

Waziri wa Kilimo na Chakula, Eng. Dkt. Charles Tizeba (Mb) jana Jumanne tarehe Oktoba 23, 2018 aliongoza mamia ya waombolezaji kuaga miili ya watumishi watano wa wizara yake waliofariki kwa ajali ya gari juzi tarehe Oktoba 21, 2018 katika Kijiji cha Njiri Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida wakiwa safarini kutokea Jijini Dodoma kuelekea mkoani Shinyanga na Mwanza kikazi.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Bi. Hilda Kinanga akieleza hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Kilimo tangu kutokea ajali iliyoua watumishi hao.

Ajali hiyo iliyolihusisha lori la mizigo na gari ya serikali STK 8925 iliyokuwa na watumishi hao watano ambao walikuwa safarini kuungana na Ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) kwa maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa kuanzisha viwanda vya kusindika mazao (Stage Agro Processing Zone).

 

Dkt. Tizeba amelitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida kutoa taarifa zilizo sahihi tofauti na taarifa walizozitoa awali za ajali hiyo kwani zinakinzana na maelezo ya dereva wa lori ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni vilevile kukinzana na maelezo yanayotolewa na mashuhuda waliopo katika eneo la ajali hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Eng. Mathew Mtigumwe akitoa taarifa za miili ya marehemu wakati wa zoaezi la kuaga miili ya watumishi hao.

“Naomba Kauli iliyotolewa na Jeshi la Polisi irudiwe tena waende wakafanye utafiti wa kweli kwani kumekuwa na lawama kwa dereva wa serikali ambazo hazistahili maana taarifa zinasema kuwa dereva wa lori alikuwa anaingia barabarani pasina kufuata taratibu jambo lililopelekea kutokea kwa ajali hiyo.

“Ninaomba sana Jeshi la Polisi kutenda haki katika tukio hili lenye kuacha maumivu kwa familia, wizara na Taifa zima,” alisema Dkt. Tizeba.

 

Tizeba amewataka wananchi kuacha kulaumu na kutoa hukumu kwa dereva wa serikali kwa kusababisha ajali hiyo badala yake kuwaombea marehemu wapumzike kwa amani kwani hakuna binadamu anayeweza kusababisha ajali na vifo vya watu wengi kwa makusudi.

Dkt. Tizeba akizungumza wakati wa kuaga miili ya watumishi hao.

Watumishi hao walioagwa kwa kupoteza maisha kwa ajali ya gari ni Dereva Mwandamizi wa wizara ya kilimo Ndg Abdallah Seleman Mushumbusi (53), Afisa kilimo wa Wizara Ndg Charles Joseph Somi (33), Mkemia daraja kwanza Ndg Erasto Isack Mhina (43), Mtakwimu daraja la kwanza Bi Ester Tadayo Mutatembwa (36) na Mhasibu daraja la pili Bi Stella Joram Ossano (39).

 

Aidha, Mhandisi Tizeba ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na watumishi wote wa wizara ya kilimo kwa kupoteza nguvu kazi ya Taifa tena watumishi hao wakiwa safarini kutekeleza majukumu ya kiserikali. Vilevile amewashukuru wabunge wa kamati ya kudumu ya maji, kilimo na mifugo kwa kuacha kikao kazi ili kuungana na waombolezaji kuaga miili ya watumishi hao.

Sehemu ya waombolezaji walioshiriki kuaga miili ya watumishi hao.

 

Viongozi wengine walioshiriki katika zoezi la kuaga miili hiyo ni pamoja na waziri wa fedha na Mipango Mhe Philiph Mpango, Waziri wa Viwanda, Bishara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage, Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdallah Ulega na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya kilimo Prof Siza Tumbo.

Dkt. Tizeba akiongoza zoezi la kuaga miili ya watumishi hao, wengine pichani ni Waziri wa fedha na Mipango Mhe Philiph Mpango, Naibu Waziri wa kilimo Mhe Mary Mwanjelwa, na Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdallah Ulega. (Picha Na Mathias Canal, WK).

Kwa upande wake katibu Mkuu wa wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe amewataja watumishi hao waliofariki kuwa walikuwa wachapakazi hodari, wapole, wacheshi na waadilifu hivyo kufuatia mauti iliyowakumba Wizara imepata pengo kubwa.

 

Alisema kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma mwajiri anagharamia misiba hiyo na kuahidi kushirikiana na ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu nyingine za kupata haki na mafao yao.

LIVE: Taarifa ya Habari Kutoka TBC1 (Oktoba 24, 2018 – Asubuhi)

Comments are closed.