The House of Favourite Newspapers

TRA Imekuja na Hii Mpya, Mpaka Tutaelewa Tu! – Video

Afisa Elimu kwa mlipa kodi, Rose Mahendeka akizungumza na waandishi wa habari.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema ipo katika mchakato wa kuweka elimu ya kodi katika mitaala ‘syllabus’ ya elimu nchini ili wanafunzi waanze kufundishwa maana ya kodi tangu wakiwa wadogo.

 

Hatua hiyo inatokana na kuwapo kwa uelewa mdogo katika masuala ya kodi ambao unachangia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara wengi hasa wanaoanzisha biashara kuona ulipaji kodi ni mzigo.

Akizungumza katika mafunzo ya kodi kwa wafanyabiashara wadogo na wakati, Afisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi kutoka TRA, Rose Mahendeka alisema mchakato huo unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

 

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya The Tanzanian Associate kwa kushirikiana na Kampuni ya Abel and Fernandes Communications, yalilenga kuwakuelimisha jamii kuhusu masuala ya kodi.

Aidha, Mahendeka alisema bado kuna changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara kutoelewa umuhimu wa kulipa kodi pamoja na kuweka kumbukumbu za mapato na matumizi katika biashara zao.

 

“Wafanyabiashara wengi hawana uelewa wa kodi ila tupo katika mchakato wa kuweka elimu ya kodi katika mitaala ya elimu waanze kupata wakiwa wadogo kabisa kule mashule ili waanze kupata uelewa wakiwa wadogo kabisa kwamba nini maana ya kodi, inahusu nini na jinsi gani kodi inalipwa Tanzania, tunaamini kwa njia hiyo watu wengi wataelewa,” alisema.

 

Naye Mshauri wa masuala ya Kodi, Petro Francis alisema ni muhimu sana kwa wafanyabiashara wa ngazi zote kuelewa maana ya kodi na umuhimu wa kulipa kodi.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Abel & Fernandes Communications, Fatma Fernandes akifafanua jambo kuhusu mafunzo ya elimu ya kodi kwa wafanyabiashara.

“Jamii inapaswa kufahamu kwamba kodi ndio chanzo kikuu cha mapato ya serikali, hivyo bila kodi huduma za kijamii haziwezi kupatikana, huduma za hospitali, barabara na madaraja, zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na kodi kutoka kwa wananchi wake,” alisema.

 

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Abel & Fernandes Communications, Fatma Fernandes alisema sheria za kodi zipo ila wajasiriamali wengi wanashindwa kuelewa namna kufanya ili kulipa kodi kwa wakati.

 

Wakati Mwanzilishi wa Taasisi ya The Tanzania Associates, Lucy Minde alisema wameandaa mafunzo hayo ili kuhamasisha watu wajifunze umuhimu wa kulipa kodi na kuzingatia sheria za biashara ili wasipate shida pindi wanapoanzisha biashara.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Kwigaya Mito alisema mfanyabiashara ni muhimu kujua ni wakati gani alipe kodi, wakati gani apate msamaha wa kodi na wakati gani aenende vizuri na sheria za kodi kwani kodi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

 

Naye Fahad Rajab ambaye pia ni mfanyabiashara alisema mafunzo hayo yamemfungua upeo lakini pia amejua kodi si kuionewa.

“Vijana tunapofanya biashara huona kama kodi ni mzigo, ila ukielimishwa na kupata ushauri, unaona kodi ni sawa na inatusaidia kuongeza pato la Taifa na kuleta maendeleo kiujumla,” alisema.

NA MWANDISHI WETU.

TRA Imekuja na Hii Mpya, Mpaka Tutaelewa Tu!

Comments are closed.