The House of Favourite Newspapers

TRA Yalikana Gari La Mobeto

0

 

AMA ulikuwa na taarifa za mitandaoni kuwa gari la mwanamitindo maarufu Hamisa Mobeto limekamatwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa kudaiwa kodi na kutokuwa na vibali halali, taarifa hiyo imekanushwa.

 

Aliyekanusha madai hayo ya gari aina ya Toyota Land Rover aliyodai Mobeto kuwa amejizawadia kwenye siku yake ya kuzaliwa ni kigogo mmoja wa TRA Wilaya ya Kinondoni.

 

KIGOGO TRA: “We hizo habari umezipata wapi.”

MWANDISHI: “Zinaenea kwenye mitandao ya kijamii.”

KIGOGO TRA: “Kwamba limekatwa na TRA?”

 

MWANDISHI: “Ndiyo, kwamba linadaiwa kodi na halina vibali.”

KIGOGO TRA: “Ngoja nicheki kwenye mtandao na kufuatilia, nipigie baadaye kidogo.”

Baada ya muda wa dakika kama arobaini hivi, mwandishi wetu alipomtafuta tena kigogo huyo ambaye hakupenda kutaja jina lake alisema:

 

“Nimetafuta taarifa hizo sijazipata, inawezekana ni habari za huko kwenye mitandao.”

Sakata la ‘gari la Mobeto’ limekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii tangu alipotangaza kuwa amejipa raha mwenyewe.

 

Baada ya kujimwambafai hivyo, kizazi cha udaku kwenye mitandao ya kijamii kiliibuka na hoja kuwa gari hilo lilikuwa ni kanya boya na kwamba mhusika ni mfanyabiashara aitwaye Juma na kwamba mwanamitindo huyo alikuwa anajitekenya mwenyewe.

 

Mambo yalipokuwa mengi gazeti ndugu na hili, Risasi Mchanganyiko wiki hii lilimtafuta mama wa Mobeto, Shufaa Rutiginga kupitia kwa meneja wa mwanaye huyo ambapo alitoa kauli inayoenda kinyume na ile ya mwanaye huyo.

 

Mama huyo alisema: “Hilo gari ni la Mobeto na amepewa na mtu.”

Jambo ambalo lilitofautiana na kile alichosema mwanaye.

Wakati mambo yanazidi kuwa moto, ikavuja taarifa nyingine kwamba gari hilo liko mikononi mwa Serikali kwa kukwepa kodi, jambo ambalo lilizua upya vijembe na maneno kwenye mitandao ya kijamii.

 

Chanzo chetu kilisema kuwa mbali na gari hilo kukamatwa mtu anayedaiwa kuliingiza nchini ambaye ni Juma naye anatafutwa na dola na kwamba hajulikani alipo.

 

Juma alipotafutwa kwa namba zake za simu hakupatikana hata mtu anayetajwa kuwa ni rafiki yake wa karibu kwa maana ya msanii Mwijaku anayedaiwa kujua mchezo mzima wa gari hilo la Mobeto naye hakupatikana kwa njia ya simu.

 

Hata hivyo chanzo chetu kingine kiliendelea kuthibitisha kuwa gari la Mobeto limekamatwa na kama kigogo wa TRA amesema halioni kwenye mtandao inawezekana taarifa zake zimefichwa ili kupisha uchunguzi.

Leave A Reply