The House of Favourite Newspapers

Trump Atangaza Hali ya Hatari Janga la Corona

0

RAIS wa Marekani,  Donald Trump,  ametangaza hali ya dharura kutokana na kuenea kwa virusi vya Corona, pamoja na upatikanaji wa karibu dola bilioni 50 kama msaada zaidi wa serikali ya shirikisho kupambana na ugonjwa huo.

 

Trump ametoa tangazo hilo katika mkutano na waandishi wa habari na kusema kwamba hali nchini humo inaweza kuwa mbaya zaidi na kwamba “wiki nane zinazofuata zinaweza kuwa mbaya sana”.

 

Trump amekabiliwa na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya wataalamu juu ya hatua za kujivuta na zisizo na ufanisi katika kushughulikia janga hilo. Hatua za hivi karibuni za Marekani zimekuja siku mbili baada ya Trump kupiga marufuku watu kuingia nchini humo hususan wa kutokea Ulaya.

 

Trump ambaye hapo awali alionekana kusimama kando ya afisa wa Brazil ambaye ameambukizwa COVID-19, amesema kwamba hata mwenyewe atafanyiwa vipimo haraka iwezekanavyo, lakini akaongeza kwamba hatojiwekea karantini kwa sababu hana dalili zozote.

Wakati huohuo shirika la afya ulimwenguni (WHO) limesema Ulaya sasa ndio kitovu cha janga la virusi hivyo ya China ambako virusi hivyo vilianzia, kupungua. Kulingana na shirika hilo vifo duniani kote vimefikia watu 5,000.

 

Televisheni ya taifa ya Iran imetangaza kwamba vikosi vya usalama vitaisafisha mitaa katika juhudi za kukabiliana na maambukizi zaidi. Kenya, Ethiopia, Sudan na Guinea nazo zimethibitisha visa vya kwanza vya COVID-19 na kuzifanya jumla ya nchi Afrika zilizoathirika kufikia 18.

Athari za mripuko wa virusi hivyo katika maisha ya kila siku zimezidi kuongezeka duniani kote. Shule, biashara vimefungwa kwenye nchi kadhaa kujaribu kupunguza kuenea mripuko, huku pia sekta ya michezo nayo ikiathirika.

 

Viongozi mbali wa dunia, nyota wa michezo na watu maarufu ni miongoni mwa maelfu ya watu walioambukizwa. Umoja wa Ulaya umeahidi kutoa Euro bilioni 37 kama sehemu ya mpango wa kusaidia juhudi za kukabiliana na mripuko wa virusi vya Corona. Fedha hizo zitakuwa kwa ajili ya kusaidia katika uchumi na huduma za umma zinazotolewa kwenye ngazi ya kitaifa.

 

Nchini Ujerumani jimbo la North Rhine Westphalia limetangaza kuwa shule zake zote zinapaswa kufungwa ifikapo Jumatano ijayo hadi mwishoni mwa likizo ya Pasaka. Na mshambuliaji wa klabu ya Paderborn ya Ujerumani, Luca Kilian, amegundulika kuambukizwa virusi vya Corona, akiwa ni mchezaji wa kwanza katika ligi ya Bundesliga kuathirika.

 

Taarifa hizo zimetolewa muda mfupi baada ya shirikisho la soka Ujerumani (DFL) kuahirisha michezo ya wikiendi hii ya ligi kuu na ligi ya pili. Ujerumani sasa inaungana na England, Hispania, Italia, na Ufaransa kusitisha ligi yake kutokana na maradhi hayo.

Leave A Reply