Tshabalala: Huyu Onyango Siyo Mtu Poa, Watakiona!

BEKI wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, amempigia saluti beki mpya wa timu hiyo, Mkenya, Joash Onyango kwa kusema haitakuwa kazi nyepesi kwa washambuliaji wa timu pinzani kupenya kwenye ngome yao kutokana na uwezo mkubwa wa kukaba alionao.

 

Tshabalala ametoa kauli hiyo kufuatia mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Vital’O ya Burundi ambao umepigwa juzi Jumamosi kwenye tamasha la Simba Day lililofanyika Uwanja wa Taifa, Dar.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Tshabalala amepongeza kiwango cha beki huyo baada ya mchezo huo huku akiwatahadharisha washambuliaji kuwa siyo jambo jepesi kuweza kupata nafasi ya kufunga mbele ya beki hiyo.

 

“Nadhani kila mmoja ambaye amefika uwanjani leo (Jumamosi iliyopita), ameweza kuona kila mchezaji na wamefurahishwa juu ya ubora wao kwa sababu ndiyo kitu ambacho kama timu tulichokuwa tunahitaji ili tuendelee kutetea makombe yetu kama ilivyokuwa msimu uliopita.

 

“Kuhusu Onyango kwangu ni beki mzuri na bora kwa sababu ana kila ambacho kinaweza kufanya mshambuliaji ashindwe kufunga, naamini uwepo wake kwetu kwa kuwapa ugumu washambuliaji wa timu mpinzani na ndiyo jambo kubwa ambalo litatusaidia kuendelea kuwa bora,” alisema Tshabalala.

IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam

Toa comment