The House of Favourite Newspapers

Tumekopi, tumepesti ‘Ngada’ inatunyoosha!

0

MOJA kati ya janga kubwa la vijana kwa sasa ni madawa ya kulevya (ngada). Kwa kipindi kirefu tumekuwa tukishuhudia vijana wakiangamia kwa madawa ya kulevya. Imedhihirisha kwamba udhibiti ni mdogo, madawa yanaingia nchini, vijana wanatumia.
Madawa ya kulevya si utamaduni wetu. Tumeiga. Nchi zilizotutangulia kimaendeleo ndizo zilionesha mfano, vijana wetu nao wakafuata.

Bahati mbaya sana dunia ni kama kijiji sasa hivi. Huko kwa wenzetu tuliowaiga, tunatambua madhara yaliyowapata. Mwanamuziki Muingereza Amy Winehouse, alijizolea umaarufu miaka ya 2000 lakini alifariki mwaka Julai 23, 2011 kwa kutumia madawa ya kulevya yaliyochanganywa kwenye pombe.

Juni 25, 2009, dunia ilihuzunika kwa kumpoteza mfalme wa Muziki wa Pop Duniani, kipenzi cha wengi, Michael Jackson. Alizidisha madawa aina ya Propofol na Benzodiazepine, kifo kikawa haki yake.
Wenye mapenzi ya nyimbo zake adimu kama vile Thriller, iliyobeba jina la albamu iliyouza nakala zaidi ya milioni 65 duniani kote, waliendelea kuzienzi kazi zake licha ya kuwa walitamani aendelee kuwepo duniani. Hakukuwa na jinsi, maisha yake ndiyo yaliishia hapo.

Februari 11, 2012, Whitney Houston, mwanamuziki bora wa wakati wote kifo chake kilitokana na madawa aina ya Cocaine. Licha ya mashabiki wake kuguswa na albamu zake kali kama Whitney Houston (1985), Whitney (1987), I’m Your Baby Tonight (1990), My Love Is Your Love (1998), Just Whitney… (2002), One Wish: The Holiday Album (2003) na I Look to You (2009) huo ndiyo ukawa mwisho wake.

Mpiga gitaa la besi maarufu Marekani, Allen Woody aliondoka kwa utumiaji wa madawa aina ya Heroin. Hiyo ilikuwa ni mwaka 2000. Wakati huo vijana wetu wa Bongo Fleva ndiyo ilikuwa inachanganya.
Kina Profesa Jay (Joseph Haule), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ndiyo walikuwa wakiendeleza harakati za kuutohoa muziki wa Marekani na kuuimba katika muktadha wa Kibongo.
Kama walivyokuwa wakikopi mashairi, baadhi ya wasanii walianza taratibu pia kukopi uvutaji wa madawa ya kulevya. Nasema baadhi maana si wote waliokopi ‘ujanja’ wa kuvuta madawa. Wale ambao nao walikuwa hawatumii, walikuwa wakiwajua wale wanaotumia lakini hakuna aliyethubutu kumshauri mwenzake aache.
Hata wale waliothubutu, nao hawakuweza kuwaambia kinagaubaga. Kulikuwa na kuoneana haya fulani. Usiri ulitawala na matokeo yake tukathubutu, tukakubali ngada itunyooshe.

Mwisho wa siku tukajikuta tumepoteza majembe katika muziki. Mungu azilaze roho za marehemu; Albert Mangweah, Langa Kireo na wengineo ambao maisha yao yalitawaliwa na skendo ya madawa ya kulevya.
Mbali na hao, wapo wengi ambao mpaka sasa wanaendelea kutumia madawa ya kulevya. Rashid Makwiro ‘Chid Benz’ ameonesha somo juzikati katika vyombo vya habari. Rehema Chalamila ‘Ray C’ alishakiri kutumia, akasema ameacha. Tatizo suala hili linafanyika kwa siri lakini ubaya ni kwamba tunakoelekea ni janga zaidi. Kuna hatari zaidi ya kuwa na kizazi kilichotopea kwenye madawa.
Kuna kila sababu ya kila mmoja kuamka na kuchukua hatua. Wasanii wenyewe muamke. Mkemee matumizi ya madawa hayo. Msaidiane wenyewe kwa wenyewe. Msioneane haya. Kwa wale ambao tayari wameshaanza kutumia, tuwape elimu ya kujikwamua.

Kwa wale ambao bado, tuwape elimu zaidi ya madhara ya madawa hayo ili wasithubutu. Kila mmoja awe askari wa mwenzake. Tupinge madawa ya kulevya kwa nguvu zote, wasanii wafanye muziki bila madawa.
Bahati nzuri serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ imeonesha dhamira ya dhati ya kushughulikia mianya ya madawa hayo hatari. Kila mmoja akiamua kukataa, madawa haya hayawezi kuingia nchini na kuathiri vizazi vijavyo!

Leave A Reply