The House of Favourite Newspapers

Ufahamu Ugonjwa wa Moyo wa Mfumo wa Umeme (Atrial Fibrillation)

0

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema sababu ya kifo cha Rais John Magufuli ni tatizo la moyo la mfumo wa umeme (atrial fibrillation) alilokuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10.

 

 

Magufuli amefariki dunia jana Jumatano Machi 17, 2021 saa 12 jioni katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

 

Machi, 2020 daktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Peter Kisenge wakati huo akiwa mkurugenzi wa tiba ya moyo alieleza kuhusu ugonjwa huo na video yake kuweka katika mtandao wa Youtube wa taasisi hiyo.

 

 

Katika maelezo yake, Dk Kisenge alisema tatizo la umeme wa moyo ni pale mapigo ya moyo yanapokuwa chini sana au juu sana hali ambayo si ya kawaida.

 

“Mapigo ya moyo yanakuwa chini ya 40 kwa dakika. Mgonjwa anapata shida anapokuwa anafanya shughuli zake anachoka au wakati mwingine anaanguka na anapata shida sana,” amesema Dk Kisenge.

 

 

Kuhusu umeme huo, alisema husaidia kusukuma damu na kupeleka kwenye viungo mbalimbali. Akiseleza sababu ya kutokea ugonjwa huo, Dk Kisenge alisema kwanza kuna wagonjwa wanaotokana na umri mkubwa na wengine wenye magonjwa ya mishipa ya damu.

 

“Huo umeme ambao Mungu ametutengenezea unakuwa haufanyi kazi vizuri, au unafanya kwa kiwango cha chini sana au kwa kasi sana. Inatokea kutokana na maumbile au umri.”

 

 

“Wengine wanapata kutokana na magonjwa ya mishipa ya damu, kwamba mishipa ya kulia nayo inapata shida mtu anapata tatizo la umeme wa moyo. Matatizo haya yanapata watu wenye umri wa miaka 55 na kuendelea. Wengi tunaowatibu hapa ni miaka 70 na kuendelea,” alisema.

 

 

Hata hivyo, alisema ugonjwa huo huwapata watu wenye umri mdogo wenye magonjwa ya kurithi au wenye kasoro kimaumbile.

 

 

Aliwashauri watu kubadili mitindo ya maisha ikiwa pamoja na kuacha uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe uliokithiri na kuepuka vyakula vyenye mafuta hasa ya wanyama na vyakula vya wanga.

 

Aliwataka wahudumu wa afya kuwaelekeza wagonjwa wenye dalili za ugonjwa huo kufika kupata tiba kwenye taasisi hiyo.

 

 

“Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye taasisi hii ikiwemo mashine iliyogharimu Sh4 bilioni. Rais Magufuli aliwekeza Sh4.5 bilioni kwa ajili ya kununua mtambo wa kutibu moyo kwa mapigo yanayokwenda kasi sana.”

 

 

“Mtambo uliopo unasaidia kufanya upasuaji wa moyo bila kupasua kifua, pia unasaidia madaktari kupima shikizo za moyo na kuzibua mishipa ya damu kwa watu wanaopata shambulio la moyo.

 

 

“Mtambo huo pia unawezesha kuweka betri za moyo (pacemaker). Kwa mwaka jana tumeweka betri 200 kwa wagonjwa waliokuwa wanahitaji betri ya moyo. Kama mgonjwa huyo akienda India angelipa Sh20 milioni,” alisema.

 

Pacemaker ni betri ndogo ya kuendesha mapigo ya moyo ambayo huhisi (sense) iwapo mapigo ya moyo yanakwenda si kawaida ama yanakwenda polepole. Hupeleka taarifa kwenye moyo na kufanya mapigo ya moyo yaende kawaida (sawa sawia).

 

Pacemakers za kisasa zina uzito mdogo sana wa 1 ounce (sawa na gramu 28). Peacemakers nyingi zina sehemu mbili:

  1. Generator ambayo imebeba betri na taarifa za kudhibiti mapigo ya moyo.
  2. Leads ambazo ni nyaya ndogo sana zinazounganishwa kwenye moyo kwenda kwenye generator ili kubeba taarifa katika mfumo wa umeme kwenda kwenye moyo.

Pacemaker hupandikizwa kwenye ngozi ya mwili ambapo upasuaji huo unaweza kuchukua takribani saa moja.

 

Leave A Reply