The House of Favourite Newspapers

Ugonjwa Sugu wa Figo (Chronic Kidney Disease)-2

Dk. MARISE RICHARD| RISASI JUMATANO| AFYA

KATIKA makala iliyopita tulieleza visababishi mbalimbali vya maradhi haya. Moja wapo ni kile kiitwacho kitaalamu Atherosclerosis;  husababisha upungufu mkubwa wa damu katika figo husika, kwa kitaalamu hali ambayo inaweza pia kusababisha madhara zaidi kwa figo na hatimaye ugonjwa sugu wa figo na hata CRF.

Tuliona kuwa magonjwa kama vijiwe katika figo, kuvimba tezi dume, kuziba kwa njia ya mkojo pamoja na saratani, vyote vinaweza pia kusababisha madhara katika figo na hatimaye ugonjwa sugu wa figo.

Tunaendelea kueleza kuwa vyanzo vingine vya ugonjwa sugu wa figo ni pamoja na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ambayo husababisha hali inayoitwa HIV Nephropathy , ugonjwa wa Sickle Cell unaoweza kusababisha kuziba kwa mirija inayosambaza damu kwenye figo au upungufu wa damu kwenye figo. Pia matumizi ya madawa ya kulevya, maambukizi sugu katika figo na saratani za figo.

VIHATARISHI VYA UGONJWA SUGU WA FIGO

Mtu aliye na mojawapo ya vitu au magonjwa haya ana hatari kubwa ya kupata ugonjwa sugu wa figo na hatimaye CRF (Glomerular Filtration Rate). Wenye matatizo haya, hawana budi kuhakikisha kuwa figo zao zinafanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kuangalia utendaji kazi wake. Magonjwa hayo ni kisukari aina zote mbili, shinikizo la damu, kiwango cha juu cha Kolestroli au lehemu katika damu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya ini, magonjwa yanayohusiana na aina mbaya ya  protini (Amyloidosis), ugonjwa wa seli mundu, kitaalamu huitwa Sickle cell disease, na ugonjwa wa mzio au mcharuko mwili wa lupus kitaalamu Systemic Lupus erythematosus.

Magonjwa mengine ni ugonjwa wa mishipa ya damu kama vile magonjwa ya mzio katika artery (arteritis) au vasculitis, matatizo katika njia ya mkojo ambapo mkojo badala ya kutoka nje, kushuka chini, hupanda kurudi ndani ya figo kitaalamu hali hiyo huitwa Vesicoureteral reflux, matumizi ya mara kwa mara ya madawa ya kutuliza mcharuko mwili au mziona kuwa na historia ya magonjwa ya figo katika familia.

Mpenzi msomaji wa safu hii,  figo zina uwezo wa ajabu wa kukabiliana na hali ngumu na matatizo katika utendaji kazi wake kwa muda mrefu. Kwa sababu hiyo basi, mgonjwa sugu wa figo anaweza kudumu katika hali yake kwa muda mrefu bila kuonesha dalili zozote zile.

DALILI ZA UGONJWA WA FIGO

Dalili za ugonjwa sugu wa figo hujitokeza pale utendaji kazi wa figo unapokuwa umeshuka na kufikia kiwango cha chini kabisa. Dalili hizo ambazo baadhi tulizikata katika toleo lililopita ni pamoja na kukojoa sana hasa wakati wa usiku, kuvimba uso na macho, kuvimba miguu, ongezeko la shinikizo la damu, uchovu na udhaifu wa mwili kutokana na upungufu wa damu au kurundikana kwa uchafu na sumu mwilini, kupoteza hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika na mwili kuwasha.

Dalili nyingine ni kupata michubuko kirahisi katika ngozi na ngozi kuwa nyeupe kwa sababu ya upungufu wa damu. Dalili nyingine ni kupumua kwa tabu kutokana na mrundikano wa maji katika mapafu, kichwa kuuma, kujihisi ganzi miguuni au mikononi, kupata shida ya kupata usingizi au kulala usingizi wa mang’amung’amu, mabadiliko katika uwezo wa utambuzi kwa sababu ya madhara katika ubongo yanayosababishwa na mrundikano wa uchafu na sumu za urea, maumivu ya kifua kwa sababu ya mzio katika gamba la juu la moyo, kutokwa damu kwa sababu ya ukosefu wa chembe zinazosaidia damu kuganda, maumivu ya mifupa na kuvunjika kirahisi na pia kukosa hamu ya tendo la ngono kwa wanaume.

Leo mpenzi msomaji tunaishia hapa, usikose kuungana nasi wiki ijayo ambapo pamoja na mambo mengine tutaeleza vipimo na matibabu ya ugonjwa huu sugu wa figo. Daima tukumbuke kuwa miili yetu ni tunu na baraka kubwa kutoka kwa Mungu, hivyo tuilinde kwani kufanya hivyo mbali na kutuepushia matatizo, maumivu maradhi mbalimbali pia ni njia mojawapo ya kumshukuru Mungu kwa neema nyingi alizotujaalia.

Comments are closed.