The House of Favourite Newspapers

Ujenzi Nyumba za Kisasa Wahimizwa Monduli

0
Baadhi ya vijana wakishirikia katika shughuli za kijamii za kusomba mawe Wilayani Monduli.

 

Baada ya serikali kupitia wizara ya ya Afya, maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto kuandaa mwongozo wa uhamasishaji ujenzi wa nyumba bora ngazi ya jamii kwa nchi nzima,wananchi wa kijiji cha EMAERETE wilayani Monduli mkoani Arusha wameanza kunufaika na mpango huo.

Chuo cha maendeleo ya jamii Monduli,(CDTI)kwa kushirikiana na wanajamii wa eneo hilo wanatekeleza kampeni hiyo kwa kuanza kujenga nyumba ya mfano kwa mmoja wa mkazi wa eneo hilo, Anna Mollel, ambae amekiri kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, imeanza kuathiri maisha yao ya kutumia rasilimali kama miti ,nyasi na udongo katika kujenga nyumba zao kama walivyozoea.

“Mimi kwanza nilianza kustuka baada ya kugundua miaka ya hivi karibuni katika mzingira tunayoishi tumeona athari kubwa ya uharibifu wa mazingira kwa maana ya mabadiliko ya tabianchi kwa sasa miti na nyasi hazipatikani hivyo nikajiongeza nikaona nijenge nyumba bora ambayo ni ya kudumu na sio ya miti wala kuezeka kwa nyasi”alisema Anna.

Anna alisema katika jamii yao hakuna wivu wa maendeleo kutokana na kuishi kwa mazoea kwani tangu wamezaliwa wamekuwa wakiishi katika nyumba hizo hivyo imekuwa ni changamoto kubwa kuwabadilisha kwa kuwa hakuna mwananchi mwenye nyumba bora Zaidi ya nyumba za nyasi,miti na udongo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli, Elibariki Ulomi alisema kampeni hiyo inalenga kufanya mageuzi  ya kifikra na mtizamo wa jamii kuhusu makazi bora kwa wananchi kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika eneo hilo kwa kuhakikisha wanajenga nyumba bora ambazo zinatumia rasilimali rahisi na sahihi katika ujenzi huo.

 

Alisisitiza kuwa suala la maendeleo ni la jamii nzima na kuwataka wananchi wa wilaya ya monduli kukitumia Chuo cha maendeleo Monduli kupata ushauri wa mambo mbalimbali ya kijamii ili waweze kuboresha maisha yao.

“Suala kubwa ni kuiwezesha jamii kujiletea maendeleo,na nimewaambia wananchi kuwa serikali haituletei fedha,serikali haitujengei nyumba nyumba bora tutajenga wenyewe”

Mkuu wa wilaya ya Monduli kamishna msaidizi wa polisi Edward Balele amesema lengo kuu la serikali ya awamu ya tano ni kuleta maendeleo ya pamoja kwa wananchi wake jambo ambalo linaenda sambamba na makazi na afya bora.

 

Alisema wananchi wa kata ya monduli juu tofauti na kata nyingine wamebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba na wamekuwa wakilima mazao kama ngano,shayiri,maua na wana mifugo ya kutosha hivyo suala la ujenzi wa nyumba bora ni la lazima.

“Mtu ukiishi katika nyumba bora inamaana utakuwa na afya bora na ukiwa na afya bora utakuwa na uwezo wa kuchapa kazi na kujiletea maendeo yako binafisi na serikali kwa ujumla”Alisema ACP Balele.

 

Kwa upande wake makamu mkuu wa chuo taaluma  Monduli CDTI Maryam Juma amesema tafiti zilizofanywa katika eneo la kata ya Monduli juu zinaonesha kuwa asilimia 16.3 tu ya wananchi wa eneo hilo ndio wananishi kwenye makazi au nyumba bora na asilimia 83.3 wanaishi kwenye makazi duni.

 

Kampeni hii inatarajiwa jamii kuwa na nyumba bora zilizojengwa katika mpangilio mzuri na kutumia vifaa vya ujenzi vyenye ubora,yenye madirisha yanayopitisha mwanga na hewa ya kutosha,iliyoezekwa vizuri na yenye choo bora.

Leave A Reply