The House of Favourite Newspapers

Ukorofi! Mobeto, Lulu Waishi Mtaa Mmoja

0

UKOROFI huo! Ndiyo maneno unayoweza kuyatumia kwa sasa kufuatia mwanamitindo maarufu wa kimataifa Bongo, Hamisa Hassan Mobeto, kudaiwa kwenda kuishi karibu kabisa na nyumbani kwa staa wa Bongo Movies, Elizabeth Michael almaarufu Lulu ambaye ni mke wa ndoa wa mzazi mwenzake, Francis Ciza au Majizzo, IJUMAA limedokezwa.

 

WALIWAHI KUJIBIZANA

Taarifa za ndani kabisa zililifikia Gazeti la IJUMAA kuwa, Mobeto ndiye aliyemfuata Lulu ambaye miaka kadhaa nyuma, waliwahi kuwa na majibizano yasiyo na afya mitandaoni.

Kwenye majibizano hayo, Mobeto aliyezaa mtoto mmoja wa kike na Majizzo aitwaye Fantasy, alimshutumu Lulu kumuibia baba wa mtoto wake, lakini sasa wanaishi mtaa mmoja maeneo ya Mbezi- Beach jijini Dar es Salaam.

 

MOBETO UKOROFI

“Jamani ninyi duniani kuna vituko na ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni; yaani wakati wewe unasema huwezi kuishi karibu na ex wako, ni tofauti kabisa kwa shoga yetu Hamisa (Mobeto).

“Huwezi kuamini, Hamisa (Mobeto) ameenda kupanga nyumba mtaa mmoja na nyumbani kwa Lulu na Majizzo (yaani ukuta ndiyo umewatenganisha), kama siyo ukorofi ni nini?

“Kifupi ni kwamba yakitokea matatizo pale mtaani kwao au shughuli yoyote ile, lazima wakutane kwa sababu wapo karibu sana, tunasema Hamisa ndiye amemfuata Lulu kwa sababu Lulu ndiye aliyeanza kuishi mtaa huo na awali Hamisa (Mobeto) alikuwa haishi hapa baadaye ndiyo akahamia.

“Halafu kitu kingine, hapa Lulu na Majizzo hawajapanga, ni wa muda mrefu,” anasema mtu wa karibu wa mastaa hao ambaye ameomba chondechonde jina lake lisitajwe popote.

 

WANAISHI KIZUNGU

Kuna msemo unaosema kuwa, mafahali wawili hawakai zizi moja; lakini hii imekuwa tofauti kwa Mobeto na Lulu.

Licha ya kwamba, wawili hao wanaishi karibu, lakini hata aina ya maisha yao ni tofauti (wanaishi kizungu) hili linathibitishwa na baadhi ya majirani zao ambao IJUMAA limefika na kuzungumza nao mtaani hapo.

 

“Ni kweli Lulu na Hamisa (Mobeto) wanaishi karibu sana, lakini kwa upande wangu sioni tatizo lolote lile kwa sababu kila mmoja yupo bize na maisha yake.

“Pia nadhani ni afadhali kwa mtoto wa Hamisa (Mobeto) na Majizzo, Fantasy maana anakuwa yupo karibu na wazazi wake wote hivyo hata akihitaji kuwaona inakuwa haimpi shida,” anasema jirani yao aliyenitambulisha kwa jina moja la Rose akiwa na wenzake.

MFANYAKAZI AFUNGUKA

Gazeti la IJUMAA lilibisha hodi kwenye nyumba hizo ambapo lilibahatika kuzungumza na mfanyakazi wa ndani wa Lulu ili kujua ukweli wa ukaribu wa wa wawili hao ambapo naye kwa upande wake alifunguka anachokijua;

IJUMAA: Mambo…

MFANYAKAZI: Poa, karibu.

 

IJUMAA: Asante, tumeona hapa Hamisa Mobeto na bosi wako, Lulu wanaishi pamoja, vipi hakuna shida yoyote?

MFANYAKAZI: Ni kweli Hamisa (Mobeto) anaishi hapa karibu na sisi, lakini hakuna shida yoyote kwa sababu kila mtu yupo bize na maisha yake; yaani hawaingiliani kwa chochote.

IJUMAA: Fantasy (mtoto wa Mobeto) huwa anakuja kumtembelea baba yake hapa kwa Lulu?

 

MFANYAKAZI: Ndiyo, huwa anakuja, halafu kama ikitokea Fantasy anataka kuja kwa baba yake, huwa anatumwa mtu anakwenda nyumbani kwao kumchukua au analetwa na wafanyakazi wa Hamisa (Mobeto) kuja kumsalimia baba yake.

 

MAMA MKUBWA WA MOBETO

Baada ya Gazeti la IJUMAA kumaliza kufanya mazungumzo na mfanyakazi wa Lulu, lilitia timu getini kwa Mobeto na kufanikiwa kukutana na mwanamke mmoja aliyejitambulisha kuwa yeye ni mama mkubwa wa Mobeto ambapo mambo yalikuwa hivi;

 

IJUMAA: Habari yako mama?

MAMA MKUBWA: Salama wanangu hamjambo?

IJUMAA: Sisi ni wazima kabisa, tulikuwa tunapita hapa kuwasalimia, tukaona kama mnahama nyumba!

MAMA MKUBWA: Hapana, wala atuhami, gari limekuja kuchukua vitanda tu, tunataka kuvibadilisha tuweke vingine, ninyi nanyi wambeya…vile si vitanda tu kwani mmeona kuna vyombo vingine?

 

IJUMAA: (waandishi wanacheka) Ooh! Tukajua labda mnahama, hamtaki kuendelea kukaa karibu na baba wa Fantasy…

MAMA MKUBWA: (anacheka) jamani naomba niingie ndani, kwanza huyo Hamisa (Mobeto) mnayemtafuta hayupo, ametoka muda si mrefu na mama yake, wameelekea mjini.

IJUMAA: Ahaa kwa hiyo watachelewa kurudi?

 

MAMA MKUBWA: Ndiyo, lakini mnaweza kuacha mawasiliano yenu ili akija nimjulishe awapigie (waandishi wanaacha namba kisha kuondoka na geti linafungwa).

MIJENGO YA KIFAHARI

Hata hivyo, Gazeti la IJUMAA limeshuhudia mijengo ya kifahari wanayoishi mastaa hao ingawa tofauti ni kwamba, Lulu hajapanga, lakini Mobeto yeye amepanga.

Waandishi: Memorise Richard na Khadija Bakari.

Leave A Reply