The House of Favourite Newspapers

Umoja wa Afrika, Marekani Walaani Shambulio la Al Shabaab Kenya

 

MWENYEKITI wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat amelaani vikali shambulio lililofanywa katika hoteli ya kifahari ya DusitD2 jijini Nairobi, Kenya.

 

Katika taarifa yake, Faki amevisifu vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya kwa kuchukua hatua za kuwahudumia haraka watu walioathirika na tukio hilo na kupambana na wahalifu mapema iwezekanavyo. Pia amesema tukio hilo linaonyesha umuhimu wa kupitia upya mipango ya kuongeza nguvu ya kupambana na vikundi vya kigaidi barani Afrika.

 

 

“Mwenyekiti wa Tume anathibitisha utayari wa AU kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na nchi wanachama katika kupambana na ugaidi na harakati za kuleta amani nchini Somalia, na kuzidisha mapambano dhidi ya kundi al-Shabaab kupitia vikosi vyake vya AMISOM.

 

Balozi wa Marekani anayemaliza muda wake nchini Kenya, Bw Robert Godec, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa Marekani inashutumu vikali shambulio hilo.

 

 

Amesema maofisa wote wa ubalozi wa Marekani wako salama na kwamba Marekani iko tayari kusaidia iwapo itahitajika kufanya hivyo.

 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imethibitisha kuwa raia wake mmoja ni kati ya watu waliopoteza maisha kwenye mkasa huo.

 

 

Kuna ripoti kuwa mpaka sasa watu sita wamethibitishwa kupoteza maisha, watano kati yao walifariki wakiwa ndani ya mgahawa mmoja ulio ndani ya viunga hivyo na mwingine alipoteza maisha baada ya kufikishwa hospitali.

 

 

Bado idadi rasmi ya watu waliofariki haijatolewa na mamlaka husika, hata hivyo, mfanyakazi mmoja wa chumba cha  kuhifadhi maiti jijini humo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kuna miili 15 iliyohifadhiwa kutokana na shambulio hilo.

 

Kundi la al-Shabab ambalo linadai kutekeleza shambulio hilo limetoa taarifa kuwa watu 47 wameuawa.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

 

Comments are closed.