The House of Favourite Newspapers

Unaijua tofauti ya wewe na waliofanikiwa? Soma hapa!

0
Successful businesspeople raising hands upward.
Successful businesspeople raising hands upward.

Wapo ambao wamekuwa wakisema maisha ni magumu na wanafikia hatua ya kukufuru kwamba bora hata wajifie tu kuliko kuendelea kuishi maisha ya kifukara yasiyo na nyuma wala mbele.

Fikira hizi zimekuwa zikinishangaza sana hasa zinapotoka kwa mtu ambaye unamuona amekamilika, yaani siyo kilema, siyo mgonjwa na ana nguvu za kutosha kabisa.

Mimi sikubaliani na haya maneno kwamba maisha ni magumu na nadiriki kusema kwamba, wapo ambao wanautengeneza ugumu wenyewe na kujiweka kwenye mazingira ya kukata tamaa.

Kiukweli maisha siyo magumu bali itategemea wewe umeamua kuishi vipi. Ukijaribu kufuatilia utabaini kuwa, wakati wewe ukisema maisha ni magumu, wapo ambao wanaishi maisha ya raha mustarehe.

Wanakula vizuri, wanaishi kwenye mazingira mazuri na kila wanachokihitaji wanakipata. Hawa nao ni binadamu ambao wana kichwa kimoja kama wewe, wana miguu miwili na mikono miwili kama wewe, sasa iweje wao wawe na mafanikio katika maisha yao, wewe uishi maisha yasiyo na mbele wala nyuma?

Hili ni jambo ambalo unatakiwa kulitafakari kama kweli unataka kuwa na mafanikio. Huwezi kufanikiwa kama utakuwa ni mtu wa kuona wao ni wao na wewe ni wewe. Ukiwa na dhana hiyo, hakuna miujiza inayoweza kutokea. Utaendelea kuogelea kwenye dimbwi la ufukara na wenzako wataendelea kufanikiwa na kuyafurahia maisha kila siku.

Siku zote wanaofanikiwa ni wale wenye hasira na maisha. Wale ambao wanachukia maisha ya kutegemea watu wengine, wanaoamini kwamba mafanikio ni kwa kila mtu. Hawa hata kama siyo leo, kesho ya mafanikio ni yao.

Watataabika, watajaribu mbinu zote ambazo ni halali na wakati mwingine watashindwa lakini hawatakata tamaa, watapambana hadi watakapofikia pale wanapopahitaji. Wewe kwa nini usiwe mmoja wao?

Ifike mahali tusifanye makusudi kumkasirisha Mungu aliyetuumba na kutuleta hapa duniani kwa kupingana na dhamira yake. Umeletwa hapa duniani ukiwa umekamilika ili upambane na ufanikiwe. Kubweteka kwako na kuridhika na maisha duni uliyonayo ni jambo linalomkera Mungu. Ni vyema ukaamka sasa na kuanza kupambana.

Ni kweli kufanikiwa siyo rahisi, mafanikio yapo kwa wale wanaofanya kazi kwa bidii, wasiokata tamaa, wanaoamini wao ni mabilionea watarajiwa. Hayo yana uwezo wa kuyabadili maisha yako.

Jiulize tu kwamba, wao waweze wana nini na wewe ushindwe una nini? Hakika waliofanikiwa siyo malaika wala hawana kitu cha ziada ambacho wewe huna. Unachokikosa wewe ni dhamira ya kufanikiwa. Kama huna dhamira hiyo, huwezi kufanikiwa.

Leo hii ukifanikiwa kukutana na matajiri wakubwa unaowajua wewe utabaini ni watu wa kawaida sana, hawana vichwa viwili na mikono minne. Wako kama wewe kwa kila kitu ila tofauti yako na wao ni jinsi mnavyowaza.

Wao waliwaza mafanikio kila wakati. Wakilala, wakiamka wakitembea, wanafikiria kipi ambacho wanaweza kukifanya na kuzidi kuwa juu kimaisha. Wanazisumbua akili zao kila wakati.

Sasa wakati wao wakiwa katika hali hiyo, wewe upo upo tu! Unajiona huwezi, wao ndiyo wanaweza! Unachukulia eti kwenye orodha ya watu waliopangiwa mafanikio, wewe humo! Achana na mawazo hayo, amka, pambana na uamini kwamba hata wewe siku moja utakuwa ni mtu wa tofauti kuliko ulivyo leo.

Leave A Reply