The House of Favourite Newspapers

Unapojisahau kwa maisha ya mjini, ipo siku utaaibika kijijini kwenu!

0

Ni ukweli kwamba asilimia kubwa ya watu hutoka vijijini kwao na kwenda mijini, lengo likiwa ni kutafuta maisha. Kwa mfano, jijini Dar kila siku watu wanamiminika kutoka mikoa mbalimbali kufuata fursa na hakika wengi wamefanikiwa.
Lakini sasa, jambo ambalo linanisikitisha wapo watu ambao wakishafanikiwa huko mjini, husahau walikotoka.

Wanawasahau ndugu na jamaa zao waliowaacha kijijini, hawawasaidii kwa namna yoyote, kitu ambacho hakika si kizuri.
Nasema hivyo kwa sababu haliwezi kuwa jambo zuri wewe ukawa na maisha mazuri mjini, unakula ukitakacho, unabadili magari ya kifahari wakati ndugu zako kijijini wana hali mbaya.

Furaha ya wewe kufanya matanuzi hayo inakamilikaje? Yaani unakula na kusaza lakini wazazi wako uliowaacha kijijini wanashindia mlo mmoja. Umepanga jumba la kifahari lakini mama yako mzazi anaishi kwenye kibanda ambacho mvua ikinyesha kinavuja halafu wala hujali.

Kwenda kwenyewe kuwatembelea mpaka utokee msiba, eti uko bize mjini unasaka pesa. Kuwasaidia kwako ni siku mojamoja na hakuendani kabisa na kile ambacho mtu anastahili kuwafanyia wazazi wake.

Sasa, unaweza kufanya hivyo kisha ukaona ni sawa lakini kama ulikuwa hujui, kwa kufanya kwako hivyo unajiandalia maisha mabaya ya baadaye. Nasema hivyo kwa sababu wapo watu ninaowajua waliokuwa na maisha mazuri sana, wakasusa kwao, wakawasusa wazazi wao lakini leo hii wanaishi maisha duni sana.

Hii yote ni laana ya wazazi! Mzazi ambaye alitarajia kwamba kwa mafanikio yako atanufaika halafu akaona unampotezea, itamuuma na atasononeka sana lakini hatakuwa na la kukufanya zaidi ya kumuachia Mungu.

Mungu naye hawezi kukuacha hivihivi, yaani hawezi kukuona amekupa mafanikio halafu wewe ukajiona mjanja, unatumbua pesa na familia yako pamoja na washkaji zako kisha akakuacha! Ni lazima ‘atakupiga kibao’.

Utarudi kwenye umaskini na inawezekana kabisa kwa uwezo wa Mungu, akawapa baraka wale uliokuwa umewasusa. Matokeo yake unarudi kijijini na huko unakwenda kusaidiwa na ndugu zako uliokuwa umewatupa, uko tayari hayo yakutokee?
Kingine ambacho nataka kukikumbusha hapa ni ile tabia ya baadhi yetu kujenga majumba ya kifahari mjini halafu tunasahau kujenga vijijini kwetu. Kuna tajiri mmoja hivi karibuni alipata aibu kubwa.

Ilikuwa hivi; siku zote maisha yake yalikuwa mjini, amejenga nyumba kibao huku akiishi kitajiri. Kajisahau kujenga kijijini kwao Mlalo, Wilayani Lushoto, mkoani Tanga. Ikawa hata kukiwa na tatizo, anakwenda kwao lakini halali pale alipokulia, anaenda zake hotelini.

Siku moja akapata msiba wa mama yake ambao uliwagusa marafiki zake wengi wa mjini, wakasafiri hadi kijijini kwake. Ilikuwa ni aibu, mazingira yaliyokutwa nyumbani kwa wazazi wa tajiri huyo hayakuwa yakiendana na maisha aliyokuwa akiishia mjini. Aibu ikawa ni kwake. Je, wewe uko tayari kupata aibu hiyo? Jibu unalo!

JIUNGE SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

KUNUNUA MAGAZETI YA GLOBAL PBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave A Reply