The House of Favourite Newspapers

UNDANI BABU ALIYEDAIWA KUBAKA KATOTO

DAR ES SALAAM: Mkazi wa Mburahati Motomoto jijini Dar, Mohammed Hassan ‘Babu Komeni’ anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 65, anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mburahati kwa madai ya kumbaka mtoto wa kike wa miaka mitatu, Amani lina undani wa tukio hilo la kusikitisha.  

 

Mtoto huyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kimaadili inadaiwa alifanyiwa unyama huo Oktoba 31 mwaka huu, saa nne asubuhi ambapo mama wa mtoto huyo, Nasma Kumenya alikuwa ametoka na kumuacha na mama zake wadogo.

 

TUSIKIE SIMULIZI YA MAMA

Akizungumza na Amani juzi, mama wa mtoto huyo (pichani) alisema: “Siku ya tukio nilitoka kidogo kwenda kwenye mihangaiko yangu, niliporudi ndipo nikasikia taarifa za mwanangu kubakwa ambapo nilipofika tu nyumbani, nikakuta umati ukinisubiri.

 

“Baada ya kutokea ndipo nikaanza kupewa taarifa hizo na mdogo wangu niliyemuachia mwanangu ambaye aliniambia kwamba, alimuona mtoto akitoka chumbani kwa Babu Komeni akichechemea na sura ilikuwa ikionesha ana maumivu.

 

“Baada ya kugundua hilo mdogo wangu akamuuliza umefanywa nini, mbona kama anataka kulia halafu unashindwa kutembea vizuri? Mwanangu akabaki kimya lakini alipobanwa zaidi akasema kuwa kaingiliwa.

 

“Baada ya kueleza alichofanyiwa ndipo waliokuwepo walimkagua na kumkuta ni kweli ameshaingiliwa kimwili na kuumizwa vibaya sehemu zake za siri na hata mimi nilipotokea na kuambiwa hayo, jambo la kwanza ilinibidi nimkague tena mbele ya umati huo ndipo nami nikathibitisha kuwa ni kweli mwanangu amefanyiwa ukatili huo.

 

“Kufuatia hali hiyo ilinibidi wenzangu wanisindikize kwenda kwa mjumbe kumpa taarifa ambapo tulimgongea, naye alitupokea na baada ya kumuelezea tukio hilo alituhoji sana na alipotosheka na maelezo yetu alituuliza kama tunafahamu alipo mtuhumiwa kwa muda huo.

 

“Kwa kuwa muda huo mtuhumiwa alikuwa amejifungia chumbani kwake, tulimuambia mjumbe kuwa yupo amejifungia chumbani kwake kwenye banda la uani.

“Mjumbe akatupatia makamanda wake ambao tuliwapeleka mpaka kwenye chumba cha Babu Komeni ambapo walimkamata na kumpeleka Kituo cha Polisi cha Mburahati. Mimi nilifika kituoni hapo na kuwapa maelezo ya awali.

 

“Nilipewa PF3 na kuambiwa kwanza nimpeleke mtoto akaangaliwe na madaktari ndipo nirudi tena kufungua kesi na niambatanishe majibu ya daktari kwenye vielelezo vya kesi hiyo.

“Nilimpeleka mwanangu Kituo cha Afya cha Mianzini, walipomuangalia wakasema mtoto ameharibiwa sana hivyo nimuwahishe Hospitali ya Sinza (Palestina) kwani wao hawakuwa na uwezo wa kumshughulikia kutokana na hali aliyokutwa nayo.

“Nilimkimbiza pale Palestina ambapo walimfanyia uchunguzi na kumtibia kisha wakanipa dawa nyingine za kutumia nyumbani ndipo nikarudi polisi ambapo nilitoa maelezo tena na kufungua kesi yenye jalada namba MBT/RB/5395/2018 UBAKAJI. Kesi hiyo walipewa wapelelezi Koplo Deodatha na Koplo Fredrick.

MJUMBE ATOA MSIMAMO MKALI

Mwanahabari wetu akiwa nyumbani hapo lilipotokea tukio hilo, Mjumbe wa Shina wa eneo hilo, Mussa Kapogo naye alitokea na makamanda wake ambapo alitaka kukiona chumba cha Babu Komeni anachodaiwa kufanyia ukatili huo.

 

Mjumbe huyo alifikishwa kwenye chumba hicho lakini alikuta kimefungwa huku ikidaiwa kuwa babu huyo bado alikuwa mahabusu. Akathibitisha kutokea tukio hilo kwenye eneo lake na kusema watu wenye tabia kama hizo hawana sifa ya kuishi eneo lake.

Mtoto huyo bado anaendelea na matibabu wakati kesi ikitarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Muliro alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema: “Taarifa za kubakwa mtoto huyo tunazo, tunazishughulikia kwa mujibu wa sheria na tutahakikisha mtuhumiwa anafikishwa mahakamani.”

Comments are closed.